Kasomi
JT Founder
Kilomita 1100 zimetumika katika kuisafirisha boti maalum ya uokozi (Ambulance) iliyotoka mkoani Mtwara kwenda jijini Mwanza kwa ajili ya uokozi ikiwa ni juhudi za Serikali katika kuimarisha shughuli za uokoaji katika Ziwa Victoria.
Boti hiyo imewasili mkoani Morogoro leo Juni 19,2025, ambapo Dereva wa gari linaloisafirisha, Hamadi Mwashamu ameeleza hadi sasa ametembea kilomita 1100 kutoka Mtwara hadi kufika Morogoro mjini.
Aidha, amebainisha changamoto ya miti na nyaya za umeme zilizopo barabarani zinapelekea kutembea umbali wa kilomita chache kwani kuna baadhi ya maeneo hulazimika kukata miti ili kuzuia athari kwa boti hiyo.
Kwa upande wake, Afisa Mwandamizi wa Mahusiano kutoka Shirika la Meli Tanzania (TASAC), Mariam Mwayela amesema ujio wa boti hiyo utaongeza hali ya usalama wa wavuvi na wakazi wa maeneo ya karibu na ziwa pamoja na kuimarisha huduma za haraka za uokoaji na afya kwa jamii inayozunguka ziwa Victoria.
Boti hiyo ina vifaa vyote vinavyopatikana Hospitali ikiwa na uwezo wa kuwahudumia wagonjwa 12 kwa wakati mmoja huku ikiwa na chumba maalum cha wagonjwa mahututi (ICU).
Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM, Fikiri Juma ameeleza boti hiyo ni mkombozi katika masuala ya Afya na maenedeleo ya kiuchumi.
Boti hiyo maalum hadi sasa imepita katika mikoa ya Mtwara, Ruvuma, Njombe, Iringa na Morogoro huku ikiwa imetumia jumla ya siku 14 tangu kuanza safari.
Tazama video hapa jinsi Boti hiyo inasafirishwa