Advertise here

Samaki wasio na mapezi na magamba hawaruhusiwi kuliwa

Samaki wasio na mapezi na magamba hawaruhusiwi kuliwa

Maandiko katika kitabu cha Mambo ya Walawi 11:9-12, yanasema:
9 Katika hao wote walio ndani ya maji mtakula hawa; kila aliye na mapezi na magamba, ndani ya hayo maji, na ndani ya bahari, na ndani ya mito, mtakula hao.
10 Na hao wote wasio na mapezi na magamba, ndani ya bahari, na ndani ya mito, katika hao waendao majini, na katika wote wenye uhai, waliomo majini, hao ni machukizo kwenu,
11 watakuwa machukizo kwenu; msiile nyama yao, na mizoga yao itakuwa machukizo kwenu.
12 Kila asiye na mapezi wala magamba aliye ndani ya maji ni machukizo kwenu.

Mapezi ya samaki ni nini
Hivi ni vile vitu kama mbawa ngumu zenye mfano wa miiba zinazokaa kwa juu, au pembeni, au nyuma mwa mwili wa samaki. Ukitazama samaki kama perege, sato au sangara, utaona mapezi yao.
Faida za mapezi hayo ni kuwa yanasaidia kuogelea, kuelea vema kwenye maji, kukunja kona, kuongeza kasi, kusimama au kugeuka kwa haraka.

Magamba ya samaki ni nini
Halikadhalika, samaki waliokuwa na magamba ndio tu walioruhusiwa kuliwa. Magamba yaliwasaidia kujilinda na maadui au wadudu wavamiaji kwenye mwili. Ngozi ya samaki ni laini, hivyo isipofunikwa na magamba magumu kama yale, meno makali ya maadui katika njia wanapopita, ni rahisi kujeruhiwa. Yanakaa kama vile dirii (kinga/shield) kifuani mwa askari.

Lakini si samaki wote walikuwa na haya mapezi na magamba. Wengine hawakuwa nayo, mfano wa hao ni kama kambale, kamongo, papa, pomboo, pweza.

Kwa nini samaki hao wakatazwe kuliwa na ufunuo wake ni upi rohoni?
Kama tunavyofahamu, agano la kale ni kivuli cha agano jipya. Siyo kwamba viumbe hivyo vikiliwa vitamkosesha mtu kwenda mbingu, au vitamnajisi roho, hapana. Kuwa najisi siyo kutokwenda mbinguni, bali kunahitaji nguvu ya ziada ili kumpendeza Mungu, kama vile utakaso, nk.

Vilifanywa vile kwa makusudi ili kutupitishia sisi ujumbe wa rohoni katika agano jipya. Kwamba na sisi kama tutafanana na mojawapo wa viumbe hivyo rohoni, basi tunakuwa najisi mbele za Mungu.

Samaki mwenye magamba ni mwenye ulinzi wa kutosha dhidi ya mashambulizi ya maadui. Na sisi tunapokosa ulinzi wa rohoni, mfano wa yule askari anayezungumziwa katika Waefeso 6:13-16, mwenye dirii ya haki kifuani, ngao ya imani mkononi na chepeo ya wokovu kichwani, tunakuwa ni dhaifu, kiasi cha kutoweza kusimama mbele ya adui yetu shetani.


Hivyo, ni kuhakikisha kuwa umesimama imara katika wokovu wako, lakini pia utambue haki uliyopewa katika msalaba wa Yesu Kristo na imani yako timilifu ndani ya wokovu wako.

Hapo utakuwa umejidhatiti vya kutosha, mfano wa samaki mwenye gamba gumu, au mamba aliyefunikiwa na ngozi yenye gamba.
Ayubu 41:13 anasema: “Ni nani awezaye kumbambua magamba yake? Ni nani atakayepenya dirii yake maradufu?
14 Ni nani awezaye kuifungua milango ya uso wake? Meno yake yatisha kandokando yake. 15 Magamba yake yenye nguvu ndiyo fahari yake, Yamefungamana pamoja kama kwa kufungwa kwa muhuri. 16 Jinsi yalivyoshikamana Hata upepo hauwezi kupita kati. 17 Yamefungamana pamoja; Yameshikamana, hata hayawezekani kutengwa”.

Vile vile, samaki aliyekuwa na mapezi alikuwa ni mwepesi kukatiza katika maji. Ni sawa na mabawa kwa ndege, au miguu kwa binadamu.

Hivyo, na sisi katika ulimwengu huu wa dhambi, ili tusionekane kuwa najisi, tuvae mapezi yetu ambayo maandiko yanasema. Ndio ule utayari wa kuihubiri injili:
Waefeso 6:15 "na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa injili ya amani".

Tusienende kama watu wasio na kusudi maalum la kufanya duniani. Tuvae utayari, ndiyo mapezi yetu. Tutembee ulimwenguni kote kiuhubiri/kushuhudia habari njema.

Kwa sababu tukikosa haya, siku ile ya mwisho, tutatengwa, samaki wema na waovu. Kisha wale waovu watatupwa nje. Zingatia Mathayo 13:
47 "Tena ufalme wa mbinguni umefanana na juya, lililotupwa baharini, likakusanya samaki wa kila namna;
48 hata lilipojaa, walilivuta pwani; wakaketi, wakakusanya walio wema vyomboni, bali walio wabaya wakawatupa.
49 Ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia; malaika watatokea, watawatenga waovu mbali na wenye haki".

Tunaweza kulinganisha na nadharia ya baadhi ya vyakula, ambavyo vinasemwa sana na madaktari hata kwenye vyombo vya habari, kwamba watu wasipendelee sana kula chipsi, au unga wa nafaka ambazo zimekobolewa. Siyo kwamba binadamu akivila hataishi, la hasha. Ila ni kwamba uimara na ufanisi wa vyakula hivyo mwilini ni mdogo, hivyo mwili unakuwa dhaifu katika baadhi ya nyanja.

Kadhalika katika samaki wasiokuwa na mapezi, au wasiokuwa na magamba. Uimara na uthabiti wa ulinzi wa samaki hao unaakisi na ni kivuli cha moja kwa moja, katika uimara wa kiroho katika kupambana na adui shetani, maadui wa kiroho.

Ndiyo maana samaki wa aina hiyo hawaruhusiwi kuliwa, kulingana na imani ya kikristo.

Hivyo, tusiwe samaki najisi, wale wasiokuwa na mapezi, au wasiokuwa na magamba.

Hiyo itatuwezesha kupambana na adui shetani, NA KUSHINDA.
 
Back
Top