Advertise here

Tujiepushe na tamaa ya mali au kupenda fedha

Tujiepushe na tamaa ya mali au kupenda fedha

Kwa namna ya kawaida fedha haina ubaya wowote
, ni nyezo ambayo Mungu aliiruhusu iwepo na itumiwe ili kuendesha kushughuli zote za kijamii:
Mhubiri 19:19 “…Na fedha huleta jawabu la mambo yote”.

Lakini kitendo cha kupenda fedha, hicho ndicho Mungu amekikataza, na katika biblia kimekemewa sana. Ikiwa wewe ni mtoto wa Mungu, na roho ya kupenda fedha ipo ndani yako, basi upo hatarini sana, kuzama katika maovu mengi, biblia inasema hivyo.

1Timotheo 6:10 “Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na imani, na kujichoma kwa maumivu mengi".

Ndiyo maana biblia inawaasa sana watoto wa Mungu na kuwaambia:
Waebrania 13:5 “Msiwe na tabia ya kupenda fedha; muwe radhi na vitu mlivyo navyo; kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa”.
Mungu ametoa ahadi ya kuwahudumia watoto wake, kiasi kwamba hawatapungukiwa kabisa, hawatakosa kabisa ikiwa tu watakuwa watulivu katika shughuli zao.

Mtu mwenye tabia ya kupenda fedha ni rahisi kuhonga, ili upate fursa fulani. Ni rahisi kufanya biashara haramu kisa tu ameona zinamwingizia fedha nyingi. Mwingine atakuwa radhi hata kujiuza mwili wake kisa fedha. Wengine wanakwenda kwa waganga, wengine wapo tayari kuikana imani, nk. Hapo ndipo unajua ni kwa nini biblia inasema kupenda fedha ni shina la mabaya yote ulimwenguni. Wengine wapo tayari hata kuua watu, ili walipwe au waibe.

Mithali 1:19 “Ndivyo zilivyo njia za kila mwenye tamaa ya mali; Huuondoa uhai wao walio nayo”.

Na dalili mojawapo ambayo biblia inasema itatutambulisha kuwa tunaishi katika siku za mwisho, ni kuibuka kwa wimbi kubwa la watu wanaopenda fedha.

2Timotheo 3:1 Lakini ufahamu neno hili, ya kuwa siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari.
2 Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi".

Imefikia hatua huduma za rohoni kwa baadhi ya makanisa, kutolewa kwa fedha:

1Timotheo 6:5 “na majadiliano ya watu walioharibika akili zao, walioikosa kweli, huku wakidhani ya kuwa utauwa ni njia ya kupata faida”.

Hiyo yote ni matokeo ya wanadamu kupenda fedha. Bwana Yesu alisema, katika Mathayo 6:24: “Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia huyu, na kumpenda huyu; ama atashikamana na huyu, na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali”.

Shetani alijua hapa ndipo wanadamu wengi wanapoweza kunaswa. Hivyo, akatumia njia hiyo hiyo kumjaribia pia Yesu.
Akamwambia, nitakupa milki zote za ulimwenguni, nitakupa fedha zote na majumba yote ikiwa utanisujudia tu.
Lakini Bwana Yesu alimkemea akamwambia utamsujudia Bwana Mungu wako tu. Kwa sababu alijua kupenda fedha ni kuupenda ulimwengu.
1Yohana 2:15 “Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake”.
Kama hiyo haitoshi, wenye mali, biblia inawapa nafasi ndogo sana ya kuurithi ufalme wa mbinguni:
Mathayo 19:23 “Yesu akawaambia wanafunzi wake, Amin, nawaambieni, ya kwamba itakuwa shida tajiri kuingia katika ufalme wa mbinguni.
24 Nawaambia tena, Ni rahisi zaidi ngamia kupenya tundu ya sindano, kuliko TAJIRI kuingia katika ufalme wa Mungu”.

Vifungu vipo vingi kwenye biblia vinavyozungumzia hatari za kupenda fedha.
Lakini kupitia hivyo vichache, kama na wewe ni mmojawapo, basi geuka haraka sana. Uridhike na vile Mungu anavyokupa, kwa sababu biblia inasema:

Mhubiri 5:10 “Apendaye fedha hatashiba fedha, Wala apendaye wingi hatashiba maongeo. Hayo pia ni ubatili”.
Na pia, maandiko yanasema:
Zaburi 37:16: “Kidogo alicho nacho mwenye haki ni bora kuliko wingi wa mali wa wasio haki wengi”.
Chuma kidogo kidogo utafanikiwa:
Mithali 13:11: “Mali iliyopatikana kwa haraka itapunguka; Bali yeye achumaye kidogo kidogo atazidishiwa”.

Lakini kama wewe hujaokoka, ukweli ni kwamba hii roho ya kupenda fedha haiwezi kuondoka ndani yako, hata iweje. Itaondoka, ikiwa tu utamruhusu Bwana Yesu aingie ndani yako aibadilishe nia yako. Akishakubadilisha, hapo ndipo Roho ya kuridhika na ya utulivu itaingia ndani yako, na hapo hapo Mungu ataanza kukufundisha njia sahihi na yenye baraka ya kukusanya. Mpaka mwisho wa siku, atakufikisha pale anapotaka uwepo. Na zaidi ya yote, utaurithi uzima wa milele.

Hivyo, tujiepushe na tamaa ya mali au kupenda fedha. Chuma kidogo kidogo utafanikiwa. Ridhika na vile Mungu anavyokupa, kwa sababu biblia inasema: apendaye fedha hatashiba fedha, wala apendaye wingi hatashiba maongeo (Mhubiri 5:10).

Ruhusu Yesu aingie ndani yako aibadilishe nia yako. Akishakubadilisha, hapo ndipo roho ya kuridhika na ya utulivu itaingia ndani yako, na hapo Mungu ataanza kukufundisha njia sahihi na yenye baraka ya kukusanya.
 
Back
Top