Kasomi
JT Founder
Kutoka kuwa chini ya lebo kubwa ya muziki hadi kumiliki ya kwake binafsi, msanii nyota wa Bongo Fleva, @mbosso_, ameandika ukurasa mpya katika safari yake ya muziki kwa kuzindua rasmi Record Label yake inayojulikana kama "Khan Music".
Mbosso, amedhihirisha ukuaji na ukomavu wa hali ya juu katika tasnia ya muziki, hatua inayoweka alama mpya katika mafanikio yake ya muziki ambayo yalianza miaka kadhaa iliyopita kupitia kundi la Yamoto Band. Baada ya kuvunjika kwa kundi hilo, Mbosso alichukua muda mfupi kimya kabla ya kurejea kwa kishindo kupitia lebo ya WCB Wasafi, inayomilikiwa na supastaa @diamondplatnumz
Alijiunga rasmi na WCB mnamo 29 Januari 2018, ambapo alitambulishwa hadharani na Diamond katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam. Siku moja kabla ya utambulisho huo, Mbosso alitoa wimbo wake wa kwanza chini ya lebo hiyo uitwao “Watakubali”, ambao ulipokelewa kwa hamasa kubwa na mashabiki wake.
Katika kipindi cha takriban miaka saba akiwa chini ya WCB, Mbosso aliweza kujijengea jina kama miongoni mwa wasanii bora wa muziki wa kizazi kipya nchini Tanzania. Ameshatoa vibao vingi vilivyotikisa anga la muziki kama vile “Hodari”, “Nadekezwa”, “Tamu”, na “Picha Yake”. Mwaka 2021, alizindua albamu yake ya kwanza Definition of Love, iliyopata mafanikio makubwa ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.
Hata hivyo, mwezi Februari 2025, Mbosso alitangaza kuondoka rasmi kutoka WCB Wasafi. Diamond Platnumz alithibitisha taarifa hiyo kupitia mitandao ya kijamii, akieleza kuwa kuondoka kwa Mbosso kulifanyika kwa makubaliano ya amani na kwamba lebo hiyo inamtakia mafanikio katika safari yake mpya.
Safari hiyo mpya imechukua sura tofauti kabisa – kuwa mmiliki wa lebo yake mwenyewe. Kupitia Khan Music, Mbosso anatarajiwa sio tu kuendeleza kazi yake ya muziki kama msanii, bali pia kuwainua vipaji vipya na kuandika historia kama mmoja wa wasanii wachache waliowahi kutoka kwenye lebo kubwa hadi kuwa wakurugenzi wa lebo zao binafsi.
Anaingia kwenye kundi la wasanii wachache waliofanikiwa kusimama peke yao huku wakiendelea kutoa mchango mkubwa kwa tasnia ya muziki. Kwa sasa, mashabiki wake wanasubiri kwa hamu kusikia "RN3' ambayo itakuwa ndio project ya kwanza
Chanzo: Manara TV