Kasomi
JT Founder
Serikali ya Urusi imekiri ripoti kwamba mwanamume mmoja raia wa Urusi anadaiwa kurekodi matukio ya mapenzi ya wanawake aliokuwa amewarubuni katika nchi nyingi za Afrika na kuweka video zao mtandaoni bila ridhaa yao.
Ghana inasema inataka mshukiwa arejeshwe nchini humo ili haki ipatikane - lakini Moscow bado haijasema kama itatoa ushirikiano katika hilo.
Katika taarifa fupi, Ubalozi wa Urusi mjini Accra ulithibitisha tu kwamba "unazingatia" madai hayo.
Haikutoa dalili yoyote kama Urusi ingeunga mkono ombi la Ghana la kurejeshwa nchini humo - hatua inayochukuliwa kuwa isiyowezekana, kwani ni nadra Moscow kuwakabidhi raia wake.
Kenya imeanzisha uchunguzi wa mashirika mbalimbali na inashirikiana na washirika wa kimataifa, ikielezea kisa hicho kama uhalifu wa kuvuka mpaka unahitaji kuchukuliwa kwa hatua za haraka.
Mamlaka zote za Ghana na Kenya zimeshutumu rekodi hizo, na kuzitaja kuwa za kutatanisha, za ukatili na ukiukaji mkubwa wa haki za wanawake.
Serikali imeagiza vyombo vya usalama na uchunguzi kuchunguza haraka tukio ambalo raia wa Urusi anadaiwa kurekodi kwa siri na kusambaza picha za wanawake wa Kenya bila idhini yao.
Katika taarifa, Waziri wa jinsia Hanna Cheptumo alikashifu kisa hicho akielezea kama aina ya unyanyasaji wa kijinsia unaowezeshwa na teknolojia ambao unatishia usalama wa wanawake na wasichana.
Kama Serikali, tunaona ukiukaji kama huo sio tu kitendo cha uhalifu lakini pia vitisho kwa mfumo wa jamii yetu, ambayo msingi wake ni heshima, utu na ulinzi wa watu walio hatarini," Cheptumo alisema.
Waziri huyo alisema Serikali itachukua hatua kali huku mashirika husika yakiagizwa kufuatilia suala hilo mara moja, ikiwa ni pamoja na ushirikiano na mamlaka za kimataifa kutokana na hali yake ya kuvuka mpaka.
"Mtu yeyote atakayepatikana na hatia atakabiliwa na nguvu kamili ya sheria za Kenya chini ya Kanuni ya Adhabu, Sheria ya Matumizi Mabaya ya Kompyuta na Uhalifu wa Mtandaoni, na sheria zote muhimu zinazolinda wanawake na watoto," alisema.
Aidha amewataka wananchi kujiepusha na kushiriki au kusambaza maudhui, akionya kuwa kufanya hivyo kunaendeleza unyanyasaji na kunaweza kuvutia dhima ya uhalifu.
Wakati huohuo Msemaji wa serikali Isaac Mwaura amelilaani vitendo vya mwanamume huyo, akimshutumu kwa kuwadhulumu wanawake na kukiuka faragha yao kwa kurekodi majibizano yao na kushiriki picha mtandaoni bila ridhaa.
"Ninamlaani mwanamume wa Urusi kwa kuwadhulumu wanawake wetu," Mwaura alisema. "Hata hivyo, kama Waafrika, lazima pia tujifunze kujipenda wenyewe. Wanawake wetu hawapaswi kutambua kwamba kila mtu ambaye ni mzungu ni tajiri moja kwa moja."
Katika muda wa saa 24 zilizopita, mwanamume mwenye asili ya Kirusi, aliyejulikana tu kama Yaytseslav, amekuwa akivuma kwenye majukwaa mbalimbali ya mitandao ya kijamii.
Hii inafuatia ufichuzi kuwa amekuwa akirekodi kwa siri matukio ya faragha na wanawake wengi barani Afrika na kushiriki video hizo kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.
Vitendo vyake vilidhihirika hivi majuzi baada ya kutoa msururu wa video zilizowashirikisha wanawake wa Ghana, jambo ambalo lilipelekea uchunguzi zaidi.
Uchunguzi wa kina ulibaini kuwa Yaytseslav ameripotiwa kushiriki video za wanawake kutoka Kenya, Afrika Kusini, Ghana, na nchi nyingine nyingi za Afrika.