Advertise here

MY STORY; Ukisikia kufunzwa na ulimwengu basi mimi ndiyo ulimwengu mwenyewe! Mchumba wangu kaniacha kaenda kuoa wakati nimeenda kujifungua

Simulizi

Member
MY STORY; Ukisikia kufunzwa na ulimwengu basi mimi ndiyo ulimwengu mwenyewe! Mchumba wangu kaniacha kaenda kuoa wakati nimeenda kujifungua!

Baada ya kumaliza chuo sikuenda nyumbani, kuna kazi nilipata hivyo moja kwa moja nilianza kufanyakazi na tukaanza kuishi na mwanaume wangu ambaye tulimalizia chuo pamoja. Tulikuwa na mipango mingi, hivyo kila mshahara niliokuwa naupata nilikuwa nampa ili yeye afungue biashara kwani nilijua kuwa akifanikiwa yeye basi tumefanikiwa wote. Mshahara wangu kipindi hicho ulikuwa ni laki saba na vimatupurupu na dili nilizokuwa nikizipiga nilikuwa nafikisha mpaka laki tisa wakati mwingine milioni.

Hivyo tulikubaliana mshahara wote nimpe yeye na matupurupu ndiyo tutumie kwa ajili ya chakula kwani nyumba tulikuwa tunalipiwa na kampuni. Kwa miaka 3 nilijibana mpaka akafanikiwa kufungua duka kubwa tu la vitu vya nyumbani, alianza kama rejareja mwisho likawa ni la jumla na hata baada ya kufungua duka bado nilikuwa nampa mshahara ili tusitumie kabisa pesa ya dukani zaidi tuizungushie!

Tulinunua kiwanja ambacho kama mwanaume aliandika majina yake, na kwa kuwa nilishamuona kama mume niliamua kubeba mimba yake, hatukuongea hivyo alijua kama imetokea tu. Nilipobeba mimba ndiyo niliona kama amebadilika, akaanza kuniambia nitoe mimba kwani bado hajaja nyumbani, kwao itakuwa ngumu kunitambulisha nikiwa na mimba. Nilimuambia mimba bado haijaonekana kwani asimpeleke hivyo hivyo, akanambia yeye hawezi kumdanganya mama yake hivyo nitoe.

Tuligombana sana lakini niligoma kutoa mimba kwani nilijiona umri unaenda miaka 28 sina mtoto na tuna kipato kizuri. Kuona nimemshikilia msimamo wangu alikaa kimya na kuikubali tu mimba. Isu ikaja kwa yeye kunitambulisha kwao na kuja kwetu, tulikuwa tunabishana sana akaniambia biashara bado haijasimama na kulalamika bado ana majukumu sijui kwao, yeye hajaamua kuoa bado wakati nikiangalia mauzo kwa siku yanaweza kufika hata milioni 3.

Ujauzito ulipoifikisha miezi 6 ulikuwa unanisumbua sana na kazini ruhusa ilikuwa ni kila siku. Mwisho nilichoka nikamuambia mwanaume mimi nataka kuacha kazi! Akanambia hapana usiache kazi itakuja kukusaidia mbeleni! Nilimuambia hapana naacha, tubaki wote dukani, aligojma kabisa ila nilishachoka kazi, mimi nikaacha kwenda kazini tu. Mwisho nikaishia kusimamishwa kwani hata sikuomba ruhusa. Sikumuambia kama nimeacha kazi, nilimuambia nina ruhusa kwani sikuataka tugombane, nilishajipanga kuwa hata nikijifungua siwezi kurudi kazini.

Mazungira ya kazi ni magumu, changamoto ni nyingi, ukiingia saa mbili asubuhi kutoka ni saa mbili usiku sasa na mtoto, nilikuwa naona jinsi wanawake wenzangu wanateseka nikasema hapana sitaki hii kazi. Ilipofika miezi 8 aliniambia niombe ruhusa ili niende kwetu kujifungua. Mimi sikupanga kujifungulia nyumbani kwani nilijua kuwa kwa kuwa sijaolewa na yeye hajaja kwetu kujitambulisha basi ndugu zangu wataninyanyasa sana. Nilimuambia hapana mimi siwezi kwenda kwetu kujifungua ila alilazimisha mpaka nikaona sina namna nikaenda kujifungua.

Kipindi hicho tulishahama kwenye ile nyumba ya kampuni na mimi ndiyo nililazimisha nikimuambia nataka nyumba kubwa ili nikijifungua kumbe nilishaacha na kazi. Nilienda kujifungua, niliwaambia wazazi kuwa mwanaume atakuja kujitambulisha wakati anakuja kumuona mtoto. Nikajifungua lakini nilipomuambia kuhusu mtoto sikumuona akifurahia kama nilivyodhani, hata kuomba picha za mtoto hakuomba, yaani mimi ndiyo nilikuwa nalazimisha.

Nikaanza kazi ya kumuulizia unakuja lini kwetu, akanizungusha, mara sijui subirini kwanza mimi sijajipanga na vitu vingine, mpaka mtoto anafikisha miezi 3 alikuwa hajaja na kila nikimuambia nataka kurudi ananiambia nisubiri kidogo. Siku hiyo nilimuambia nataka kuja nikamuambia niko siriasi, akanambia ongea na kazini wakupe nyumba ile ambayo tulihama kama haijachukuliwa na mtu mwingine.

Nikamuuliza kwanini, akanambia hapana tu mimi sitaki kuishi na wewe kwa sasa kwa kuwa una mtoto, atanisumbua sana sitaki kuishi na mtoto. Nilimuambia kuwa mimi si kazi mbona nilishaacha tangu zamani. Hicho ndiyo akatumia kama sababu, akaanza kuniambia kuwa unanidharau sana kwanini uache kazi bila kuniambia, akaongea maneno mengi sana nikamuambia mimi nilikuwa naumwa nateseka kazini hivyo nilijua kuwa nikija na mtoto itakuwa ngumu kufanya kazi!

Alianza kuwa mkali, hapokei simu zangu, sijakaa sawa nashangaa akanitumia meseji, mimi naona tuachane, siwezi kuoa mwanamke ambaye hanisikilizi. Kaa huko huko kwenu mpaka upate kazi sehemu nyingine, mtoto wangu nitamhudumia lakini si kukuoa. Haunisikilizi! Nilijua kama anatania, nikamuuliza mbona unafanyahiyo, acha bwana! Kwa jinsi tulivyokuwa tunapendana kwa namna ambavyo nilihangaika naye nilijua kuwa hakuna namna anaweza kuniacha, nilimuona mume na sikuwahi kufikiria katika maisha yangu kuwa kuna wakati ataniambia maneno kama hayo!

Niliikaa kimya kama wiki nikiamini kuwa ni hasira tu zitakuja kuisha lakini haikuwa hivyo. Wiki hiyo hiyo ananiambia hivyo, nashangaa kapost status anamvalisha pete mwanamke mwingine. Nilimtafuta kumuuliza, akanijibu kwa dharau, "wewe si hunisikilizii, nimetafuta mwanamke anayenisikiliza na anayeniheshimu." Aisee nilichanganyikiwa, nilipanda gari kama kichaa kuja kumuona, nilifika tulipokuwa tukiishi nikakuta kashahama, nikaenda mpaka dukani, nilimkuta, akaanza kunifokea, tukagombana, nikavunja vitu, akaniitia polisi. Huwezi amini na mtoto wangu mchanga wa miezi 3 aliniweka ndani, usiku mzima mpaka rafiki yake ndiyo alikuja kunitoa.

Hakutaka hata kujua chochote kuhusu mtoto, hakutaka hata kumshika mtoto, nilitoka pale nikiwa sina mbele wala nyuma, rafiki yake akanipa nauli nirudi nyumbani kwanza ili nikae sawa. Niko nyumbani sasa na juzi nimeingia Instagram nimekuta mwanaume kaoa mwanamke mwingine, wanafuraha anavyomuongelea mke wake jinsi wlaivyohanagika ana maisha animejikuta nalia, sina hata nguvu ya kutoka ndani nipo tu nimechanganyikiwa, katika maisha ayangu jinsi tulibyokua tyukiishia ungeniambia hata ningeambiwa angetamani mwanamke mwingine nisingekuamini, lakini ndiyo hivyo, kaniacha ana amani, mimi nahangaika na mwanangu, sina kazi, sina chochote, sina hata mia. Nimeishia kulia tu. Andika kisa changu, angalau kuna mtu atajifunza kuwa mapenzi siyo mabaya, lakini usiingie kichwa kichwa. Kana mimi, ulimwengu hajanifundisha!
 
Back
Top