Kasomi
JT Founder
Baada ya kumalizika kwa ligi mbalimbali barani Ulaya, wadau wa soka kote ulimwenguni hujiuliza ni kwa namna gani mshindi wa tuzo ya kifahari ya Ballon d’Or hupatikana.
Ballon d’Or ni tuzo ya heshima ya mtu binafsi inayotolewa kila mwaka na jarida la France Football, kwa mchezaji anayeonekana kuwa bora zaidi duniani kwa msimu husika.
Mchakato wa kumpata mshindi hufanyika kwa awamu mbili. Kwanza, waandishi wa habari kutoka France Football na L'Équipe, kwa kushirikiana na baadhi ya wachezaji wa zamani, huandaa orodha ya wateule 30 kutokana na kiwango cha uchezaji katika msimu uliopita.
Baadaye, mwandishi mmoja wa habari za michezo kutoka kila moja ya mataifa 100 bora kwenye viwango vya FIFA hupiga kura kwa kuwachagua wachezaji 10 bora kutoka kwenye orodha hiyo. Kila mchezaji hupewa alama kulingana na nafasi aliyowekwa, ambapo mgawanyo wa pointi ni: 15, 12, 10, 8, 7, 5, 4, 3, 2, na 1.
Baada ya kura zote kukusanywa, pointi hujumlishwa na mchezaji mwenye alama nyingi zaidi hutangazwa mshindi wa Ballon d’Or. Wengine huorodheshwa hadi nafasi ya 30 kulingana na pointi walizopata.
Swali kubwa sasa ni: Ni nani anastahili tuzo hiyo msimu huu?
Chanzo: TBC