Advertise here

Je, 'Wachokonozi' Mlimchokonoa Nani?

Kasomi

JT Founder
JE, 'WACHOKONOZI' MLIMCHOKONOA NANI?
1750453997222.jpg

Joseph Mrindoko na Jackson Kabalo! Huenda pia jina lenu la kikazi la 'Wachokonozi' linaweza lisiwatambulishe ninyi ni akina nani! Kwa hiyo, hata kutekwa au kupotezwa kwenu kusiwaguse watu wengi wakiwemo vijana wenzenu kwani nimewasikia baadhi vijana wakiwasema ninyi lakini kwa kujikinai kana kwamba wao au hata ndugu zao hawawezi kutekwa!

Siwezi kuamini kama vijana hao hawajui kabisa kuwa kuna utekaji na pia siwezi kuamini kuwa wote wanaobeza yale mliyokuwa mkiyafanya kuwa wote wanalipwa na mawakala wa utekaji!
Vijana hao hawahitaji hasira ya askofu kwani ni huenda wamekata tamaa ya kupambania haki na hawaamini kama wanaweza kupambana na mfumo unaotumia pesa nyingi sana kwa ajili ya kunyamazisha wakosoaji!

Lakini mliwezaje kufikia hatua ya kuunda kundi la 'wachokonozi'? Hii ndiyo agenda ya askofu! Wazazi wenu waliwasomesha ninyi hadi kufikia ngazi adimu ya chuo. Mlipohitimu hamkupata ajira kwani wakubwa walifilisi viwanda vyote na vingine wakauza. Wafuatilizi au warithi wao ni wale walisitisha ajira kiduchu zilizobakia, sasa miaka 10 imepita tangu zisitishwe ajira, hivyo hakuna ajira kwa vijana walio wengi nchini.

Elimu yenu ilitosha kuwajuza kuwa ukosefu wa ajira ni matokeo ya sera mbovu, kutokujali na hata uongozi mbovu kwa kiasi kikubwa. Lakini pamoja na kujua hayo, ninyi hamkukata tamaa kama vijana wengine. Hamkutaka kuwa vibaka, 'mario' na wala hamkutaka kuwa machawa!

Mkabangaiza, mkakopa, mkadunduliza kwa ajili ya kununua kamera, laptop, kompyuta na vifaa kadhaa vya kazi. Mliamua kutumia kalamu na ujuzi wenu kuwa wabunifu na kuanzisha kundi la 'wachokonozi' wa fikra. Mlitaka kutoa elimu kwa vijana wenzenu ili hatimaye watoke katika giza nene la umaskini, wajue shida ya nchi yao!

Lakini kuna watu hawakupenda kundi lenu na fikra zenu. Huenda kwa fikra zao, 'uchokonozi' wenu unahatarisha 'uhafidhina' au 'status quo' kwani wanafaidika na yale mnayoyachokonoa, hivyo hawataki muendelee kuyachokonoa!

Mwili wangu unatetemeka pia niandikapo haya kwani sijajua kama mko hai au mmeshakuwa baridi kama jiwe la Kisongo! Haijulikani kama tayari mmeshatupwa kama alivyotupwa Sativa au mnafanywa kama walivyofanywa vijana wa ng'ambo ile. Sijui hata kama mtaelezwa kuwa nimeandika makala ndefu kuwahusu kwani kuna vijana wawili enzi zilizotimu waliokolewa na makala zangu ndefu! Ndio! Waliowateka pia wanasoma maandiko yangu na huenda muda wote wanachungulia kujua nimeandika nini!

Lakini kuna upande mwingine usiojulikana juu yenu! Inawezekana pia ni waumini wazuri sana na huenda kesho mngekuwa Kanisani kama ni Wasabato au mngekuwa katika Jumuiya kama ni Walutheri, Wanglikana, Waroma, Wamoravian au Wa-AICT. Lakini huenda usiku huu mmoja wenu au wote mngekuwa kwenye mkesha wa maombi kama na Wapentekoste, Waasemblizi au Makanisa huru.

Bila shaka mlikuwa watoa sadaka wazuri sana na hata watoaji wa mafungu ya kumi! Ni nani ajuaye huenda pia mlikuwa mmewaajiri vijana wengine kutokana na kazi zenu? Lakini sasa ni kama ninaelea katika bahari ya 'mapoyoyo' kwa kuwa sasa ni sielewi kitu. Sijui kama waumini wenzenu, wachungaji, mapadri, wainjilisti au maaskofu wenu wanaguswa na kilichowapata!

Sijui kama na wao wako kama hao watumishi ambao sasa wamejivika utetezi wa watawala na kutaka kila mtu anayeikosoa serikali basi cha moto na akione! Kama wapo waliothubutu kumshambulia Askofu Gwajima aliyehoji pia vitendo vya utekaji na wakafurahia pia kufutwa kwa Kanisa la Ufufuo na Uzima hao wataweza kuthubutu kuwatetea ninyi, achilia mbali hata kuwatafuta?

Lakini mmpelekwa wapi? Katika taifa ambalo hakuna watu waliowahi kuwajibika kwa utekaji, ni vigumu sana kuamini kama mko salama na hasa ikizingatiwa ya kuwa hakuna mamlaka ye yote iliyokiri kuwashikilia hadi sasa. Katika hii nchi ambayo tangu mwaka jana watekaji sasa wamebuni mtindo wa kupoteza wahanga wao, hofu yetu inazidi kuwa kubwa.

Mwezi uliopita walimteka kijana mwenzenu Kuna Kaswahili na hadi leo hajulikani alipo na habari ya Mdude ndio mliijua ipasavyo. Lakini ni nini hasa mlichokichokonoa kilichowafanya hao kikosi nyeti wawashukie kama mwewe?

Kama Askofu, ninawajibu wa kuwatafuta na pia kuwaombea! Ninamuomba Mungu Mwenyezi akawashurutishe waliowateka na hao waliotoa amri ya kutekwa kwenu kusudi wawaache huru mrudi katika familia zenu! Ole wake mtu yule atakayegusa uhai wenu na kuutowesha kwani Biblia inatoa ole kwa watu wamwagao damu za watu wasiokuwa na hatia bila ya kuthibitishwa na mamlaka ya haki!

Kuwavamia na silaha kali za kivita vijana walio wajasiliamali ambao hawana hata visu lakini hujipatia kipato kwa kuuza akili ni uwoga wa hali ya juu! Ninyi hamjawa tishio kwa mamlaka ye yote iliyo halali kwani mngekuwa hivyo, basi mngekamatwa kihalali kwa taratibu za kisheria!
Bila shaka wengi watashangazwa na tukio hili lililowapata ninyi na hivyo watatoa maoni yao!

Mwana Kondoo Ameshinda! Tumfuate!
Ameandika
Askofu Emmaus Bandekile Mwamakula
 
Back
Top