Kasomi
JT Founder
THAILAND : MWAKILISHI wa Tanzania katika mashindano ya Miss Grand International 2025, yaliyofanyika nchini Thailand, Beatrice Alex, amefanikiwa kushika nafasi ya tano bora duniani kwa mwaka huu, hatua iliyopokelewa kwa furaha na Watanzania wengi.
Akizungumza na HabariLeo kwa simu kutoka Thailand, Beatrice alisema: “Nashukuru Mungu kwa hatua hii niliyofikia. Ni fursa ya pekee kwa Tanzania kuonekana kimataifa. Nawashukuru Watanzania kwa sapoti yao ya kunipigia kura."
Mbali na urembo, Beatrice anatambulika kwa kipaji chake cha kuchora, kupiga picha, na jitihada zake za kijamii katika kuhamasisha elimu jumuishi kwa watoto wenye ulemavu.
Shindano hilo, lililofikia kilele chake Jumamosi Oktoba 18, 2025, pia limemuweka Beatrice katika nafasi ya tatu katika kipengele cha Grand Talk, na nafasi ya 15 katika kipengele cha Talent, akitumbuiza wimbo maarufu “Chambua kama Karanga” wa msanii Saida Karoli.
Kwa mafanikio haya, Beatrice Alex ameipa Tanzania heshima kubwa kimataifa, akibeba matumaini na ndoto za watanzania wengi, na kuthibitisha kwamba urembo wa Kitanzania si wa uso tu bali ni wa moyo, akili na utu.
Imeandaliwa: Brighter Masaki