Advertise here

Biblia isemavyo kuhusu umri wa kuishi

Biblia Isemavyo Kuhusu Umri wa Kuishi

Katika biblia mtu aliyeishi miaka mingi kuliko wote, ni Methusela, mwana wa Henoko aliyetwaliwa na Mungu.
Biblia inasema Methusela aliishi miaka 969, na hakuna mwingine aliyerekodiwa kuishi miaka mingi kuliko yeye.

Mwanzo 5:25 “Methusela akaishi miaka mia na themanini na saba, akamzaa Lameki.
26 Methusela akaishi baada ya kumzaa Lameki miaka mia saba na themanini na miwili, akazaa wana, waume na wake. 27 Siku zote za Methusela ni miaka mia kenda na sitini na kenda, akafa”.

Watu walioishi miaka mingi katika biblia ni pamoja na wafuatao:

Methusela, aliishi miaka 969 (Mwanzo 5:27)

Yaredi, aliishi miaka 962 (Mwanzo 5:20)

Nuhu, aliishi miaka 950 (Mwanzo 9:29)

Adamu, aliishi miaka 930 (Mwanzo 5:5)

Sethi, aliishi miaka 912 (Mwanzo 5:8)

Kenani, aliishi miaka 910 (Mwanzo 5:14)

Enoshi, aliishi miaka 905 (Mwanzo 5:11)

Mahalaleli, aliishi miaka 895 (Mwanzo 5:17)

Lameki, aliishi miaka 777 (Mwanzo 5:31)

Henoko, miaka 365 (Mwanzo 5:23)

Baada ya gharika ya Nuhu, miaka ya wanadamu ilishushwa mpaka kufikia miaka 120. Hata hivyo, ni wachache tu walivuka miaka hiyo, wengi waliishi chini ya hapo.

Mwanzo 6:3 “Bwana akasema, Roho yangu haitashindana na mwanadamu milele, kwa kuwa yeye naye ni nyama; basi siku zake zitakuwa miaka mia na ishirini”.

Hata hivyo, kadri siku zinavyozidi Kwenda, miaka ya mwanadamu kuishi duniani ilizidi kushuka, kutoka 120 hadi 80.
Zaburi 90:9 “Maana siku zetu zote zimepita katika hasira yako, Tumetowesha miaka yetu kama kite. 10 Siku za miaka yetu ni miaka sabini, na ikiwa tuna nguvu miaka themanini; Na kiburi chake ni taabu na ubatili, Maana chapita upesi tukatokomea mara”.

Lakini, swali ni hili: kwa nini miaka halisi ya wanadamu inazidi kupungua siku baada ya siku?
Je ni kutokana na mabadiliko ya tabia nchi au mabadiliko ya vyakula?

Jibu rahisi, ni kwa sababu ya kuongezeka kwa maasi kwa Mungu.
Wala si mabadiliko ya tabia nchi, bali ni DHAMBI.

Kitu cha kwanza kilichopunguza miaka ya Adamu na Hawa kutoka kuishi MILELE mpaka kufikia kuishi miaka 930 si kingine zaidi ya DHAMBI. Wala si kwa sababu walikuwa hawazingatii mazoezi au milo kamili, bali ni DHAMBI. Na kanuni hiyo hiyo inayopunguza maisha ya mwanadamu, ndiyo inaendelea hadi sasa.

Wakati huo huo, kwa upande wa pili, shetani anajaribu kuwaaminisha watu kuwa ni milo wanayokula ndiyo inayopunguza miaka. Kwamba wapunguze ulaji wa nyama, na mafuta, na wazingatie mazoezi wataishi miaka mingi.

Mambo hayo ni mazuri, na yanafaa kuwezesha mwili kuwa na afya nzuri, lakini hayafai katika kuongeza urefu wa maisha ya mtu. Hii ni kwa sababu kuna wengi ambao wamezingatia hayo yote, lakini wamewahi kuondoka duniani. Na kuna ambao hawajazingatia hayo yote lakini wanayo miaka mingi duniani.

Kanuni ya kuishi miaka mingi na ya heri ni KUMCHA MUNGU NA KUEPUKANA NA UOVU. Hiyo tu. Zishike amri za Mungu, fanya mapenzi ya Mungu, maisha yako yatakuwa marefu. Pia, zingatia Neno katika Kutoka 20:12 “Waheshimu baba yako na mama yako; siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi upewayo na Bwana, Mungu wako”.
Hiyo nayo ni moja ya anri za Mungu.

Hivyo, kuhusu umri wa kuishi, tatizo kubwa ni utendaji wa DHAMBI. Zamani watu walikuwa wanaishi miaka mingi, hadi miaka 969. Lakini kadri dhambi ilivyoshamiri, ndivyo ikawa chukizo kwa Mungu. AKAPUNGUZA umri hadi miaka 120. Kisha, akazidi kuipunguza hadi 70-80.

Ili tuishi miaka mingi, biblia inasema ni muhimu kufanya yafuatayo:

1. Tusimuwekee Mungu mipaka, kwamba hiki na hiki Mungu hawezi
(Mwanzo 22:17; Zaburi 78:41; Luka 1:37)
2. Kumcha Mungu na kuepukana na uovu (Methali 10:27; Mhubiri 7:17)
3. Kutopenda ya dunia (1Yoh 2:15-17)
4. Kushika na kufuata amri za Mungu (Kutoka 20:1-17; Kumb 5:1-21)
5. Kuepukana na kutenda dhambi (Kutoka 23:24-26; Warumi 6:23)
6. Kuishi maisha ya utakatifu (Walawi 19:2; Mathayo 5-48; Mathayo 12:33)
 
Back
Top