Historia ya Miriam Chirwa

Kasomi

JT Founder
Historia ya Miriam Thomas Chirwa ("Mhubiri Miriam")
1000705712.jpg

Miriam Thomas Chirwa, maarufu kama “Mhubiri Miriam,” ni mwimbaji wa Muziki wa Injili kutoka eneo la Makongo Juu, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam. Alizaliwa tarehe 15 Septemba 1998 akiwa na changamoto ya ulemavu wa macho pamoja na mwili mdogo sana kutokana na matatizo yaliyotokea wakati wa ujauzito wa mama, Hilda yake yaani alizaliwa akiwa Njiti. Licha ya changamoto hizo, Miriam ameendelea kuwa mfano wa ujasiri, matumaini na mafanikio kwa watu wengi wenye ulemavu nchini Tanzania.

Tangu kuzaliwa kwake, familia yake ilikumbana na changamoto nyingi pamoja na maneno ya kukatisha tamaa kutoka kwa baadhi ya watu katika jamii. Hata hivyo, wazazi wake hawakupoteza matumaini wala kumtelekeza. Walimlea kwa upendo mkubwa huku wakiamini kuwa ulemavu si mwisho wa maisha wala kikwazo cha mafanikio. Kupitia malezi hayo, Miriam alikua mtoto mwenye akili, kipaji kikubwa na moyo wa kumtumainia Mungu.

Elimu yake


Kutokana na hali yake ya ulemavu wa kuona pamoja na mwili wake kuwa mdogo sana, Miriam alichelewa kuanza shule kufuatia ushauri wa madaktari. Baadaye Mwaka 2006 alifanikiwa kujiunga na Shule ya Msingi ya Uhuru Jumuishi (Uhuru Mchanganyiko), shule maalum iliyopo karibu na Barabara ya Uhuru jirani na Shule ya Sekondari ya Benjamin Mkapa, Dar es Salaam. Akiwa shuleni, Miriam aliendelea kufanya vizuri katika masomo licha ya changamoto mbalimbali zilizokuwa zikimkabili.

Mwanzo wa Kipaji cha Muziki

Kipaji cha Miriam kilianza kuonekana akiwa bado mdogo sana, hata kabla hajafikisha miaka miwili. Alikuwa akiimba nyimbo za dini kwa sauti ya kipekee iliyowavutia wengi. Mama yake, Hilda, alianza kumfundisha nyimbo rahisi akiwa na umri wa miaka mitatu na baadaye baba yake akaanza kumuandikia nyimbo na kumuendeleza zaidi kisanii.

Akiwa na umri wa miaka sita, Miriam alipata nafasi ya kurekodi nyimbo tano za kwanza. Baadaye, akiwa na miaka saba, alirekodi nyimbo nyingine kumi zilizounda albamu yake iliyojulikana kwa jina la “Mseme Yesu Watu Wapone.” Kupitia albamu hiyo, Miriam alianza kujulikana kama mwimbaji mwenye ujumbe wa matumaini, imani na maadili mema kwa jamii.

Muziki na Huduma kwa Jamii

Mbali na kuimba nyimbo za Injili, Miriam pia ameimba nyimbo za kuelimisha jamii kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii. Baadhi ya nyimbo zake maarufu ni pamoja na:

“Rushwa” – wimbo unaopinga ufisadi na kuhamasisha uadilifu.

“Elimu ni Mwanga” – unaohamasisha umuhimu wa elimu.

“Nawasihi Wazazi” – unaowakumbusha wazazi wajibu wao kwa watoto.

“Imarisha Familia” – unaosisitiza umuhimu wa mshikamano wa kifamilia.

Kutokana na ujumbe mzuri wa nyimbo zake, Miriam alialikwa kushiriki katika matukio mbalimbali ya kitaifa na kijamii. Miongoni mwa matukio hayo ni:

Tarehe 15–16 Juni 2006, alishiriki kuimba katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika Mnazi Mmoja, Dar es Salaam.

Tarehe 15 Juni 2007, alitumbuiza katika Ukumbi wa St. Gaspars mjini Dodoma mbele ya Mama wa Rais wa wakati huo, Mheshimiwa Salma Kikwete, wakati wa uzinduzi wa Ripoti ya Elimu ya Dunia.

Tarehe 16 Juni 2007, alitumbuiza katika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma, ambapo Rais wa Tanzania wa wakati huo, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, alikuwa mgeni rasmi.

Kupitia kazi zake za muziki na ushiriki wake katika kampeni za kijamii, Miriam alipata tuzo ya “Balozi Bora wa Jamii” kwa mwaka 2011–2012 kutoka Tuzo za Muziki wa Injili Tanzania.

Ndoto na Maendeleo ya Baadaye

Miriam anaendelea kukuza kipaji chake cha muziki na ana ndoto ya kufikisha huduma yake ya muziki wa Injili katika nchi mbalimbali za Afrika kama Malawi, Zambia, Zimbabwe na Afrika Kusini kupitia nyimbo alizorekodi kwa lugha ya Chewa. Pia ana ndoto kubwa ya kuwa mtetezi wa haki za watoto wenye ulemavu ili kuwapa matumaini na kuwasaidia kufikia ndoto zao.

Pia Mwaka 2016 Miriam alikuwa maarufu sana kupitia kwenye wimbo wa Kala Jeremiah uitwao "Wanadonto" ambao ulikuwa maarufu sana

Changamoto Anazokutana Nazo

Licha ya mafanikio yake, Miriam bado alikabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo:

Kukosa mashine ya kuandikia ya Braille kwa ajili ya masomo kipindi anasoma.

Ukosefu wa msaada wa kifedha kwa ajili ya elimu na kukuza kipaji chake.

Kukosa vifaa vya muziki vya kisasa.

Changamoto za usimamizi na usambazaji wa kazi zake za muziki zilizochangia kutonufaika ipasavyo na albamu yake ya kwanza.
Japo kwa sasa anafanya vizuri sana

Aidha, awali familia yao ilikuwa inakabiliana na changamoto nyingine kutokana na kaka yake Miriam, aitwaye Obadiah, ambaye alikuwa na matatizo ya moyo yaliyosababisha ulemavu. Hata hivyo, naye alionyesha kipaji cha muziki, hasa katika upigaji wa vyombo vya muziki. Familia iliendelea kumpatia huduma za Physiotherapy na kuanza kuona maendeleo mazuri.

Ujumbe wa Familia

Wazazi wa Miriam wanaamini kuwa “ulemavu si kutokuwa na uwezo.” Kupitia juhudi zao, wamejitahidi kuhakikisha watoto wao hawapotezi matumaini bali wanapata nafasi ya kuonesha vipaji vyao na kutimiza ndoto zao.

Lakini pia mwanzoni mwa mwaka huu 2026 Miriam Chirwa alichumbiwa na Ruben
 
Back
Top