Kasomi
JT Founder
Jenista Joakim Mhagama alizaliwa 23 Juni 1967 na kufariki Leo 11 Desemba 2025. Alikuwa mmoja wa wanasiasa wanawake wenye mchango mkubwa Tanzania kupitia CCM. Alitumikia Jimbo la Peramiho kwa miaka mingi na kushika nyadhifa mbalimbali za uwaziri katika serikali tatu mfululizo.
Kwa asili alikuwa Mngoni. Alisoma Shule ya Wasichana Peramiho na baadaye kupata Diploma ya Ualimu Korogwe mwaka 1989. Alifanya kazi ya ualimu kwa miaka sita, jambo lililomjengea msingi wa uongozi na kujituma.
Safari yake ya siasa ilianza 1987 ndani ya CCM. Alipata nafasi ya kwanza Bungeni mwaka 2000 kupitia kiti maalum cha wanawake. Mwaka 2005 alishinda mchujo dhidi ya Simon Mbilinyi na kuwa mgombea wa Peramiho.
Kipindi cha 2005–2010 kilimtambulisha zaidi kama mbunge mchapa kazi. Alikuwa miongoni mwa wabunge waliotoa michango mingi bungeni. Januari 2014 aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Elimu hadi Januari 2015.
Mwaka 2015 alishinda ubunge wa Peramiho kwa kura nyingi. Rais Magufuli alimkabidhi wadhifa wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu. Baadaye mwaka 2022 alipewa majukumu mapya katika Ofisi ya Rais Utawala Bora.
Oktoba 29, 2025 alishinda tena ubunge wa Peramiho kupitia CCM. Ushindi huo ulimrejesha bungeni na kuendelea kuthibitisha uongozi wake katika jimbo hilo.
Jenista atakumbukwa kwa uadilifu na uchapakazi. Alikuwa kiongozi jasiri, mfano wa kuigwa na aliiacha Tanzania ikiwa imefaidika na mchango wake kwenye Bunge na serikali.