Advertise here

Filamu ya royal tour kuifungua tanzania

Kasomi

JT Founder
20220419030829_1179940156_1834043192060351845_640_320_85_webp.jpg


SERIKALI imesema kuwa filamu ya Royal Tour iliyozinduliwa jana na Rais Samia Suluhu Hassan, jijini New York, Marekani, itaitangaza Tanzania duniani, huku ikileta maelfu ya watalii kutoka nchini humo.

Katika uzinduzi huo uliofanyika katika jumba la Makumbusbo la Guggenheim 89th Avenue jijini New York, ulihudhuriwa na wadau wa utalii na watu mashuhuri wapatao 300, huku ikipambwa na burudani mbalimbali.

Filamu hiyo iliyochukua takribani saa moja imesheheni vivutio mbalimbali vya utalii, sanaa na burudani vinavyopatikana nchini Tanzania, vilivyotambulishwa kwa kuelezewa kwa kina na Rais Samia.

MUKTADHA WA FILAMU

Akizungumzia filamu hiyo wakati wa mjadala wa viongozi wa serikali na taasisi zake uliofanyika kwa njia ya mtandao wa Zoom, Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Hassan Abbas, kipindi cha filamu ya saa moja inayotangaza utalii wa Tanzania kiliratibiwa na mtangazaji mashuhuri nchini Marekani, Peter Greenberg.

Alisema mwandishi huyo hushawishi viongozi wa nchi kuwa mbele kutangaza vivutio vya nchi yao na Tanzania ni nchi ya tisa duniani kushiriki mradi huo unaolenga kuitangaza nchi kwenye utalii ili ijulikane duniani.

“Kwa ujumla ni kui ‘repackage’ (kuviweka pamoja) nchi yetu ili ijulikane kote duniani, iwe ni sehemu ambayo watu wawe wanakuja siyo tu kutembea, kuona wanyamapori lakini pia kurekodi matukio makubwa ya kuburudisha,” alifafanua.

Dk. Abbas ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya Royal Tanzania Tour, alisema ni mradi wa kwanza wenye kuhakikisha mazuri ya Tanzania yanafahamika ulimwenguni ikiwamo utalii, viwanda, sanaa na utamaduni.

Aliongeza kuwa filamu hiyo imezinduliwa Marekani kwa sababu lengo ni kuitangaza nchi kimataifa na kwa kuanzia wamealikwa watu washuhuri ikiwamo wafanyabiashara, wadau wa utalii na burudani.

UMUHIMU WA ROYAL TOUR

Naye, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Pindi Chana, alisema uzinduzi wa filamu hiyo unakwenda kufungua milango ya uwekezaji katika utalii pamoja na sekta nyingine, jambo litakaloongeza kipato cha mtu mmoja na taifa.

“Sisi Wizara ya Maliasili na Utalii, tunamshukuru sana Rais kwa maana hili ni jukumu letu sote la msingi. Tukisema Royal Tour inakwenda ‘ku-ibrand’(kuitangaza) Tanzania watu hawatuelewi. Tanzania tuna vivutio vingi sana vya utalii ingawa siyo wote wanavijua na utalii unachangia katika pato la taifa kwa asilimia 17,” alisema.

Alisema filamu hiyo inakwenda kutangaza utajiri wa utaliii uliopo Tanzania ikiwamo Hifadhi za Taifa 22, mapori ya akiba 27, mapori tengefu 42, kilomita 1,428 za fukwe ya Bahari ya Hindi, Mlima Kilimanjaro na Hifadhi za Wanyamapori za Jamii (Wildlife Management Area) 33.

Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Simai Said, alisema Royal Tour inakwenda kufungua milango ya watalii Zanzibar kwa kuwa wageni wanaokuja bara watavutiwa kwenda Zanzibar pia.

“Wamarekani wao wanapenda kutumia pesa, ‘they tip well’ (bakshishi safi) wanapenda huduma nzuri na wanafurahia wanachokiona, sisi lazima tuitumie fursa hiyo. Lakini huduma zetu lazima tuziweke katika mfumo ambao utawaridhisha,”alibainisha.

Aidha, alisema kuwa biashara ya utalii siyo ya serikali pekee, hivyo aliziomba sekta binafsi kushirikiana na serikali katika kukuza utalii.

Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC), Dk. Maduhu Kazi, alisema anajivunia kuwa sehemu ya mpango huo kwa kuwa wanategemea kujitokeza fursa nyingi za uwekezaji kupitia filamu hiyo.

“Kwa upande wa uwekezaji tumejiandaa vizuri sana na tunaona kuwa kutakuwa na fursa nyingi, ndani ya siku mbili kutakuwa na (Makubaliano Maalum (MOU’s) kadhaa ambazo zitasainiwa baina ya kampuni za nyumbani na za huku Marekani. Bado tunaendelea kuziaccount…kwa zile ambazo zimekashakamilika tunaona kuwa kuna uwekezaji mkubwa ambao unakuja nchini mwetu,” alisema Dk. Maduhu.

Aliongeza kuwa aina ya wawekezaji ambao Rais Samia atakwenda kukutana nao ni wale wa hali ya juu hali inayoleta matumaini ya uhakika wa kupata wawekezaji.

Alisema licha ya kuvutia wawekezaji wa Utalii wamejipanga pia kuwavutia wawekezaji katika kilimo ‘agroprecessing’ (usindikaji mazao) kwenye maeneo ambayo nchi inahitaji zaidi wawekezaji ikiwamo mafuta ya kula ambalo linaigharimu nchi Sh. bilioni moja kwa mwaka.

TTB KAZI NDO IMEANZA

Mkurugenzi wa Masoko katika Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Felix Michael, alisema ikiwa kama wahusika wakuu wa kutangaza vivutio vya utalii filamu ya Royal Tour wanaichukulia kama ni kifaa cha kimkakati cha kuitangaza biashara ya utalii kimataifa.

“Na hii filamu kwetu tunaichukulia kama ‘promotion tool’ ya kimkakati, ambayo inakwenda kujibu maswali magumu, kama upotoshaji ambao umekuwapo. Kuna baadhi ya watu duniani bado wanaamini kuwa Mlima Kilimanjaro upo nchi jirani. Kuna watu wanaamini kuwa Hifadhi ya Taifa Serengeti (SENAPA) ipo nchi tofauti na nchi yetu,” alifafanua.

Alisema wanatarajia kupitia filamu hiyo kutumia mabalozi wao wa hiyari, kutangaza na kuhamasisha utalii katika nchi za kimakakati Marekani ikiwamo, lakini pia kupanga mikakati mingine ya kuitangaza nchi.

Rais Samia aliondoka nchini Aprili 14, mwaka huu kuelekea nchini humo kwa ziara ya kikazi, ambayo pamoja na mambo mengine, anatarajia kuzindua kipindi maalum cha kutangaza utalii wa nchi yake katika majiji ya New York na Los Angeles nchini humo.

Pia, atazungumza na watanzania wanaoishi nchini humo kueleza mipango mbalimbali ya serikali, na kuwahimiza kuunga mkono juhudi za kuendeleza nchi.
 
Back
Top