Kasomi
JT Founder
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imepanga kutoa mikopo kwa wanafunzi 252,773 mwaka 2025/2026, wakiwemo 88,320 wa mwaka wa kwanza, ili kuwafikia wengi zaidi.
Akizungumza leo Juni 14, 2025 jijini Dodoma wakati wa maadhimisho ya miaka 21 ya TAHLISO, Majaliwa amesema hatua hiyo inaendeleza dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuboresha elimu ya juu. Amebainisha kuwa mwaka 2024/2025 wanafunzi 248,331 walinufaika na mikopo ya Sh. bilioni 787.4, ikilinganishwa na wanafunzi 177,925 waliopata Sh. bilioni 570 mwaka 2021/2022—ongezeko la asilimia 40.
Kuhusu Samia Scholarship, amesema mwaka 2025/2026 wanafunzi 2,630 watanufaika, kutoka 1,976 waliopo sasa, hususan waliofaulu vizuri masomo ya Sayansi.
Majaliwa pia amesema Serikali imeondoa adhabu na tozo ya kulinda thamani ya fedha katika urejeshaji wa mikopo, jambo lililosaidia kuongeza marejesho. Aidha, amesema mfumo mpya wa marejesho na utambuzi umetumiwa na taasisi 3,565 na wanufaika 3,000 kwa mwezi.
Kwa wanafunzi wa Stashahada, amesema Sh. bilioni 19.95 zilitolewa mwaka 2024/2025, kutoka Sh. bilioni 7.29 mwaka 2023/2024 — ongezeko la asilimia 177.6, huku wanafunzi 13,214 wakinufaika.
Aidha, amewataka wanavyuo kutokubali kutumiwa kisiasa, na kuwa mfano bora kwa jamii. Ameonya dhidi ya ushoga, usagaji, na dawa za kulevya.
Rais wa TAHLISO, Geofrey Kiliba, alisema wanavyuo wako tayari kuilinda amani kuelekea uchaguzi, na kwamba taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali katika maendeleo ya elimu na sera.
Chanzo: TBC