Kasomi
JT Founder
Aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole ameeleza kwamba kama jeshi la polisi nchini linamtafuta waitumie Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kuwa ndiye aliyekuwa muajiri wake wa mwisho au wamtafute kupitia namba yake ya simu.
Akizungumza kupitia mtandao wa YouTube, Polepole ambaye amekuwa na mfululizo wa mazungumzo kuhusu masuala mbalimbali kupitia mtandao huo amedai kwamba wapo maofisa waandamizi ndani ya jeshi hilo ambao wana namba zake hivyo wamtafute kupitia namba hizo.
“Ikitokea jeshi la polisi halina namba yangu kitu ambacho si kweli mimi ninawafahamu maofisa wa jeshi la polisi waandamizi ambao wana namba zangu na tunawasiliana”
“Lakini kama hawana muajiri wangu wa mwisho ni Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, wanaweza wakawasiliana Katibu Mkuu na Katibu Mkuu wakapata namba zangu ni simu moja tu mimi ninajibu meseji na mara kadhaa nikiwa katika mazingira rafiki napokea simu” amesema Polepole.
Katika taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi Makao Makuu, David Misime ilibainisha kuwa jeshi hilo limefungua jalada la uchunguzi kuhusu tuhuma mbalimbali anazozitoa Polepole na hivyo kumtaka afike polisi na ushahidi wa tuhuma hizo.