Kasomi
JT Founder
Waziri Mkuu wa Albania, Edi Rama, ametangaza kuwa Diella, waziri wa kwanza wa akili bandia (AI) duniani, sasa ni “mjamzito” na watoto 83 wa kidijitali, kila mmoja akipewa mbunge mmoja kama msaidizi binafsi.
Watoto hao wa kidijitali, ambao ni wasaidizi wa Akili Bandia, watakuwa wakifuatilia mijadala bungeni, kurekodi hoja, na kuwasaidia wabunge kupata taarifa walizozikosa au hata kupendekeza majibu katika mijadala.
Diella aliteuliwa rasmi mwezi Septemba 2025 kusimamia mfumo wa ununuzi wa umma, kwa lengo la kuufanya uwe wazi na usio na rushwa. Waziri Mkuu Rama amesema mfumo huu wa kisasa utakuwa tayari kufanyiwa kazi kikamilifu mwishoni mwa mwaka 2026.
Ingawa hatua hii imepongezwa na wafuasi wa mageuzi kama hatua ya kihistoria kuelekea uwazi wa serikali, baadhi ya wanasheria na wapinzani wameitaja kama hatari kwa katiba na uhuru wa kidemokrasia, wakisema haiwezekani “mwanadamu wa kidijitali” kuwa waziri halali.
Rama, hata hivyo, amesisitiza kuwa Diella na “watoto wake” 83 ni mfano wa mapinduzi ya utawala wa kisasa unaotegemea teknolojia, akisema:
“Ikiwa mbunge ataenda kunywa kahawa na kusahau kurudi kazini, mtoto wake wa AI atamwambia kilichosemwa, na ni nani wa kumjibu.”
Albania imefungua ukurasa mpya katika historia ya uongozi wa kidigitali duniani. Wakati wengine wakiona ni majaribio hatari, dunia inatazama kama teknolojia inaweza kweli kuondoa rushwa na kuboresha uwajibikaji wa serikali.