MOHAMED SAID SALUM
Member
KUMBUKUMBU
BABA YANGU ABDULWAHID SYKES KAMA NINAVYOMKUMBUKA
Aisha ‘’Daisy’’ Sykes Buruku
Utangulizi
BABA YANGU ABDULWAHID SYKES KAMA NINAVYOMKUMBUKA
Aisha ‘’Daisy’’ Sykes Buruku
Utangulizi
Aisha ‘’Daisy’’ Sykes Buruku ni binti ya Abdulwahid Sykes mmoja kati ya wazalendo 17 waliounda chama cha TANU kilichopigania uhuru wa Tanganyika. Daisy kama anavyofahamika zaidi kwa jina hili, ni msichana wa kwanza Mwafrika kusoma Shule ya Wasichana ya Aga Khan mwanzoni mwa miaka ya 1950 na msichana wa pili kuingia Chuo Kikuu Cha Afrika ya Mashariki, Dar es Salaam mwishoni mwa miaka ya 1960. Daisy amefahamiana na wazalendo wengi mmoja wapo akiwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na machifu mashuhuri kama Mangi Mkuu Thomas Marealle waliokuwa wakifika nyumbani kwa baba yake wakati wa harakati za kupigania uhuru wa Tanganyika. Katika kuadhimisha miaka 50 ya kifo cha baba yake, Daisy ameandika makala haya kukumbuka siku zile zilizojenga haiba ya baba yake na ya wazalendo walioshiriki katika kupigania uhuru wa Tanganyika. Kwa miaka mingi Daisy amekuwa akiishi na kufanya kazi nje ya Tanzania.
Marehemu baba yangu Abdulwahid Sykes (31 January, 1924 - 12 October, 1968), ambae hapa nitakuwa namtaja kama, ‘’baba,’’ alikuwa mtu maarufu na mzalendo ambae fikra zake zilipea na kwenda mbali kupita wakati wake. Leo tunaadhimisha miaka 50 toka kifo chake kilichotokea tukiwa na mategemeo kuwa wakati wake wa kuaga dunia ulikuwa bado haujafika. Licha ya sasa ni nusu karne toka kufariki kwake, baba yangu bado amebaki kama kielelezo na rejea muhimu ndani ya ukoo wetu wa Sykes, hasa katika wanae wanane ambao wengine wametangulia mbele ya haki na watatu walio hai – Aisha ‘’Daisy’’ Buruku, Ilyasa na Misky. Baba katika uhai wake alikuwa akifahamika kama mtu wa watu – nikitumia msemo wa siku hizi, kwani ukarimu wake ulipitiliza, na zaidi hasa kwa jinsi alivyokuwa mwepesi wa kukirimu wageni wake. Haya yalijionyesha sana Dar-es- Salaam mji aliozaliwa na kukulia na akafahamika kwa wengi Tanganyika na nje ya mipaka yake. Sifa hizi zilijulikana kwa kiwango cha juu na wote ambao walikuja kumjua, watu kutoka sehemu na tabaka tofauti, licha ya sera za kikoloni zilizotamalaki za, ‘’wagawe uwatawale,’’ ambazo wakoloni walizieneza kote. Baba hakumbagua mtu kwa hadhi yake, dini, kabila na wapi katokea.
Kumbukumbu yangu ya awali udogoni ni baba yangu alipokuwa Mkuu wa Soko la Kariakoo (Market Master), mimi wakati ule nilikuwa na umri kama wa miaka mitano au sita hivi. Namkumbuka akiwa amevaa sare yake ya shati la khaki jeupe, kaptula na soksi ndefu hadi magotini. Alikuwa na matege kwa hiyo akisimama urefu wake ulikuwa unapungua kutoka futi 5 inchi 6 hadi futi 5 inchi 5.
Huu ulikuwa wakati wa neema ambapo vikapu vya vyakula vikiletwa nyumbani kwetu kila siku asubuhi mida ya kama saa nne. Hatukupata kuwa na shida ya chochote iwe nyama, samaki, mboga mboga au matunda. Kama ilivyo tabia yake ya ukarimu, chochote kilicholetwa nyumbani kiligawanywa kwa wote katika familia. Ukarimu wote wa baba haukuweza kushinda kile ambacho baba alifanya katika mwezi wa Ramadhani ambapo watu tusiowajua kabisa na wapita njia walipokaribishwa kuja kufuturu na sisi. Ilipofika Eid, baba alihakikisha ndugu zetu walinunuliwa wao kwanza nguo mpya za sikukuku kabla yetu sisi wanae. Ukarimu wake kwa wadogo zake wawili, Ally na Abbas Sykes ulikuwa hauelezeki katika shughulikia maisha yao. Kwake yeye siku zote familia ilikuja kwanza ikifuatiwa na haki na uadilifu.
Nikiwa mtoto wa kwanza, nikikua katika miaka ya 1950 na 1960, nilipata bahati ya kushuhudia kwa mshangao mkubwa ingia toka isiyokwisha ya msururu wa wageni waliokuwa wanakuja kwetu wakati mwingine wakifika katika nyakati za usiku. Wageni wengine baba alikuwa hata hawajui wamekuja nyumbani kwetu kutoka bara lakini wameelekezwa kwa baba na watu wanaomfahamu baba. Mara nyingi ilikuwa shida kidogo linapokuja suala la malazi lakini nyumbani kwetu hakuna mtu ambae hakupokelewa akarudishwa alikotoka na hili wakati mwingine lilimkera mama yangu na baba yangu mdogo Abbas. Mambo yalipozidi kiwango mama na baba yangu mdogo walikuwa wanakula njama na kumweleza mgeni kuwa baba amesafiri ili muradi ipatikane sababu ya huyu mgeni kwenda zake.
Mbali na matukio ya bahati mbaya kama haya, nyumbani kwetu milango ilikuwa wazi siku zote kwa wageni. Hivi ndivyo tulivyokuwa na wageni kutoka kila kabila, uwezo na hali tofauti. Lakini kile ambacho kimeathiri fikra zangu na kubakia na mimi katika kumbukumbu zangu ni kufika pale nyumbani kwa uongozi wa juu wa Waafrika kabla ya uhuru, machifu kutoka makabila mbalimbali ya Tanganyika na viongozi wa vyama vya wazalendo vilivyokuwa ndiyo vinainukia, viongozi wa vyama vya wafanyakazi na wafanyakazi Waafrika katika wa serikali ya kikoloni. Kutokana na hadhi hii ya baba yangu na umaarufu wake na kule kupenda kukirimu watu, nikawa si mgeni kwa machifu mashuhuri na nikawa nawahudumia walipokuwa mara nyingi wakija nyumbani. Wageni hawa mashuhuri waliokuwa wakija nyumbani ni pamoja na Mangi Mkuu Thomas Marealle, Machifu Abdiel Shangali, John Maruma kutoka Moshi, Adam Sapi Mkwawa kutoka Iringa, Kidaha Makwaia kutoka Usukuma, Abdallah Fundikira, Harun Lugusha kutoka Tabora, Humbi Ziota kutoka Nzega, Michael Lukumbuzya kutoka Ukerewe na Patrick Kunambi kutoka Morogoro na wengine wengi. Hawa machifu kwa kawaida walikuwa wakija na wake zao, wanawake warembo ambao hawakuacha kunifanya mimi kuwashangalia. Nakumbuka katika machifu wale, alikuwapo chifu mmoja na wa pekee mwanamke - Mwami Theresa Ntare kutoka Kasulu Kibondo. Katika hali kama hii iliyokuwa tabu kufahamika, tukiwa watoto tulipata kujua maisha ya jamii nyingine, lugha zao, utamaduni wa makabila mengi ya Tanganyika kabla ya watu wengi kutoka sehemu nyingine za pwani hawajajua chochote kuhusu watu hawa.
Nilibahatika kukutana na katika utoto wangu na lile tabaka la Waafrika waliokuwa watumishi wa serikali, kundi dogo makhsusi lililokuwa linakua na liliopembuka kwa elimu zao kutoka Chuo Cha Makerere, Uganda na vyuo vingine. Hiki ndicho kilikuwa kizazi kipya cha Watanganyika wasomi waliohusika na kuasisi siasa fikra ya uhuru itakayopelekea Waafrika kujitawala - Hamza Mwapachu, Zuberi Mtemvu, Mzee John Rupia, Steven Mhando, Dunstan Omari, Dossa Aziz kwa kuwataja wachache. Kulikuwa pia na tabaka jingine la watu maarufu kutoka Zanzibar kama Ahmed Rashad Ali and Abdul Razak Abdul Wadud ambao walikuwa kama sehemu ya familia yetu. Siwezi kumsahau Maloo, Mburushi kutoka Congo ya Mashariki ambae alikuwa anakaa nyumbani na baba kwa muda mrefu sana kiasi tuliamini ni mmoja katika familia ya Sykes.
Lakini aliyeshika nafasi ya juu kabisa katika fikra zangu nikiwa mtoto alikuwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na ni kupitia kwake ndipo tukapata kujua kwa mara ya kwanza kuwa kuna kabila linaitwa, ‘’Wazanaki.’’ Kila alipokuwa anakuja nyumbani kwetu kuja kwake kulikuwa jambo maalum kulikosababisha minong’ono watu wakizungumza kwa sauti za chini wakipeana taarifa kuwa, ‘’Nyerere anakuja au keshafika.” Kwangu mimi hii ilikuwa ishara ya kutimiza kazi yangu kwani siku zote nilikuwa nikiambiwa kutengeneza kifungua kinywa cha chai na mayai kila alipokuja nyumbani akitokea Shule ya Mt. Francis, Pugu alipokuwa akisomesha.
Nakumbuka katika akili yangu ya kitoto kumuona Mwalimu Nyerere akiishi nyumbani kwetu kwa muda katika nyumba yetu ya Mtaa wa Stanley baada ya kuacha kazi wakati marafiki zake wa karibu baba na Dossa Aziz walikuwa wanamtafutia nyumba ya kuishi. Nyumba yetu ya Stanley kwa kuwa ilikuwa kwenye makutano ya barabara mbili ilikuwa na mjengo wa kipekee kwa nyakati zile. Nyumba kubwa na yenye vyumba kadhaa ilikuwa upande wa Mtaa wa Stanely na upande wa Mtaa wa Sikukuu ilikuwa nyumba nyingine inayojitegemea ikiwa na sebule na chumba cha kulala hapo hapo. Ingawa upande huu wa nyumba ilikuwa na nafasi ya kutosha ilikuwa vigumu kwa wanaume wawili wakubwa kuishi pamoja. Naamini baba yangu mdogo Abbas ambaye alikuwa akiishi kwenye nyumba ile ikabidi ahame aende kweye nyumba yetu nyingine Mtaa wa Kipata au ajibane nyumba kubwa ili Mwalimu Nyerere apate utulivu na faragha katika nyumba ile.
Mwalimu[MS1] Nyerere na Hamza Mwapachu ni watu walionivutia sana mimi kwa kiwango cha juu kwa namna walivyokuwa wakilitamka jina langu, ‘’Daisy,’’ kwa lafidhi yenyewe ya Kiingereza kama wanavyozungumza Wazungu na hii ikalifanya jina hili langu la utani linigande na liwe ndilo jina langu halisi. Nikiwa mtoto nakumbuka sana vipi baba akishughulishwa na kutaka kuona kuwa Mama Maria na watoto wake hawakosi chochote kuyafanya maisha yao kuwa mepesi, ya starehe na furaha akihakikisha chakula kinapelekwa dukani kwa Mama Maria kila siku katika duka lake dogo lilikuwapo Mtaa wa Livingstone kona na Mtaa wa Mchikichi, hiki kikiwa kielelezo chake kikubwa kabisa cha huruma na ukarimu wake.
Abdul Sykes na mkewe Mama Daisy (Bi. Mwamvua bint Masha)
[MS1]