Advertise here

Mke kupenda fedha kama Delila hubomoa ndoa yake

Mke kupenda fedha kama Delila hubomoa ndoa yake

Samsoni na Delila

Hebu kwanza tusome habari fupi kuhusu Samsoni na Delila, kama ilivyoandikwa kwenye kitabu cha Waamuzi 16:1-22

Samsoni ni nani
Siku moja, Samsoni alikwenda mjini Gaza, akakutana na malaya mmoja akalala naye. Watu wa Gaza walipoambiwa kuwa Samsoni yuko huko, walilizingira eneo hilo na kumvizia Samsoni kwenye lango la mji usiku kucha. Wakakaa kimya huko langoni usiku wote, wakifikiri kwamba wanaweza kungojea mpaka mapambazuko wapate kumuua. Lakini, Samsoni akabaki mjini mpaka usiku wa manane. Wakati wa usiku wa manane, akaamka, akashika miimo miwili ya malango (geti), akaing'oa pamoja na makomeo yake, akaibeba na kwenda nayo mpaka karibu na Hebroni. Miimo ni fremu za mlango au geti za upande wa kulia na kushoto.

Delila ni nani

Baada ya hayo, Samsoni alimpenda mwanamke mmoja aitwaye Delila, ambaye aliishi katika bonde la Soreki. Wakuu wa Wafilisti wakamjia Delila, wakamwambia, “Mbembeleze Samsoni, ili ujue asili ya nguvu zake nyingi ili tuweze kumkamata na kumfunga. Ukifanya hivyo, kila mmoja wetu atakupa vipande thelathini vya fedha".
Delila akamwambia Samsoni, “Tafadhali, niambie asili ya nguvu zako, na jinsi gani mtu anaweza kukushinda na kukufunga". Samsoni akamjibu, “Wakinifunga kwa kamba saba mbichi za upinde, nitakuwa dhaifu kama mtu yeyote". Wakuu wa Wafilisti wakamletea Delila kamba hizo saba mbichi za upinde, naye akamfunga Samsoni kwa kamba hizo. Delila alikuwa ameweka watu wamvizie katika chumba cha ndani. Kisha, akamwambia Samsoni kwa sauti kubwa, “Samsoni, Wafilisti wamekujia kukushambulia". Samsoni akazikata kamba hizo, kama nyuzi za kitani zinapogusa moto. Hivyo hakuna aliyegundua siri ya nguvu zake.

Delila akamwambia Samsoni, “Wewe umenidhihaki. Umenidanganya. Tafadhali niambie jinsi unavyoweza kufungwa". Samsoni akamjibu, “Wakinifunga kwa kamba mpya ambazo hazijatumiwa, nitakuwa dhaifu kama mtu yeyote". Basi, Delila akachukua kamba mpya, akamfunga nazo. Kisha akamwambia Samsoni kwa sauti kubwa, “Samsoni! Wafilisti wamekuja kukushambulia"! Wakati huo kulikuwa na watu chumbani wakimvizia. Samsoni akazikata kamba hizo, kama uzi.

Delila akamwambia Samsoni, “Mpaka sasa bado unanidhihaki. Umenidanganya. Niambie unavyoweza kufungwa". Samsoni akamwambia, “Ukivisuka vishungi vyangu saba vya nywele zangu katika mtandio wa nguo na kuvikaza kabisa kwa kigingi, nitakuwa dhaifu kama mtu yeyote". Wakati Samsoni alipokuwa analala Delila akavisuka pamoja vishungi saba vya nywele za Samsoni, akavifunga kwa mtandio wa nguo na kuvikaza kabisa kwa kigingi. Kisha akamwambia Samsoni, “Samsoni! Wafilisti wanakuja kukushambulia". Samsoni akaamka kutoka usingizini akaking'oa kile kigingi na kuutatua ule mtandio wa nguo.

Delila akamwambia Samsoni, “Unawezaje kusema kuwa unanipenda na moyo wako hauko pamoja nami? Umenidhihaki sasa mara tatu. Hujaniambia asili ya nguvu zako iko wapi".

Delila alipoendelea kumbana sana Samsoni kwa maneno, siku baada ya siku, na kumkera hata akachoka rohoni karibu kufa, hakuweza kuvumilia, akamfunulia siri yake, akisema, “Nywele zangu kamwe hazijapata kunyolewa. Mimi nimewekwa wakfu kwa Mungu tangu tumboni mwa mama yangu. Kama nikinyolewa nguvu zangu zitanitoka, nami nitakuwa dhaifu kama mtu yeyote". Basi, Delila alipoona kwamba Samsoni amemwambia siri yake yote, akawaita wakuu wa Wafilisti, akawaambia, “Njoni safari hii moja tu maana Samsoni ameniambia siri yake yote". Wakuu wa Wafilisti wakamwendea Delila huku wamemletea fedha walizomwahidi. Naye Delila akamfanya Samsoni alale usingizi magotini mwake, akamwita mtu amnyoe vile vishungi vyake saba.

Kisha Delila akaanza kumtesa Samsoni kwa kuwa sasa nguvu zilikuwa zimemtoka. Delila akamwambia Samsoni, “Samsoni! Wafilisti wanakuja kukushambulia”!

Samsoni akaamka usingizini huku akifikiri kwamba atatoka na kujiokoa kama hapo awali. Kumbe hakujua kwamba Mwenyezi-Mungu alikuwa amemwacha. Wafilisti walimkamata, wakamng'oa macho, wakampeleka Gaza, wakamfunga kwa pingu za shaba, na kumlazimisha kufanya kazi ya kusaga unga, huko gerezani.

FUNDISHO KUTOKANA NA HABARI YA SAMSONI NA DELILA

Habari ya Samsoni na Delila ina fundisho kubwa nyuma yake kwa wanandoa. Baadhi ya watu wanafikiri Delila alikuwa mwanamke kahaba ambaye Samsoni alikukutana naye tu na kumuokota. Uhalisia ni kwamba Delila alikuwa ni mke wa Samsoni.

Mwanamke huyu, aliweza kubadilishwa akili kwa tamaa tu ya fedha. Ni mwanamke ambaye alipendwa sana na Samsoni, cho chote ambacho angetaka kwa Samsoni, angepatiwa.


Wafilisti waliona mwenendo wa Samsoni jinsi alivyompenda sana mwanamke huyu. Wakatumia fursa ile, kumshawishi Delila, kwa kumuahidi donge nono la fedha, ili tu atoe siri ya asili ya nguvu za Samsoni.

Delila, akakubali, akaanza kumshawishi Samsoni mume wake, kwa kipindi kirefu. Akaenda akauza siri ya Samsoni kwa Wafilisti, kwa vipande vya fedha. Hatimaye akafunuliwa siri ya nguvu zake.

Kama mke, upendo unapohamia kwenye fedha, ni dalili madhubuti kuwa nguvu ya ndoa, inayotokana na upande wa mume, itakufa. Usitangulize mali mbele ya ndoa yako, wala usishawishiwe na fedha kwa chochote ukadharau thamani ya mumeo.


Samsoni hakuwa mfanya biashara au mwajiriwa wa kampuni fulani. Hakuwa hata na akaunti benki. Yeye alikuwa ni Muamuzi wa taifa teule la Mungu.

Samsoni alikuwa ni mtetezi wa wanyonge, na mkombozi wa walioonewa. Hakujitajirisha yeye, alilitajirisha taifa, jambo ambalo Delila hakulithamini.

DELILA AKAWA TAYARI KUOLEWA NA FEDHA KUTOKA KWA WAFILISTI, ILI ATOE SIRI KUHUSU NGUVU ZA SAMSONI, MUME WAKE.

Siku hizi, wapo wanawake, ambao wanachotafuta kwa waume zao ni fedha tu, na kitambulisho kuwa wameolewa. Wakikosa hiyo, wapo tayari kufanya lo lote. Wengine hata huanzisha mahusiano na wanaume wengine wenye uwezo wa juu wa kifedha, ili wapate fedha. Bahati mbaya sana, hao wanaume wa nje ya ndoa, nao huendekeza tabia hiyo.

BAADHI YA WATU HAWAJUI KUWA MWANAMUME ANAWEZA ASIWE TAJIRI KIFEDHA, LAKINI ANA KARAMA ZA KUIENDESHA NA KUILINDA FAMILIA, JAMII NA NDUGU. Kipawa alicho nacho mume kinaweza kumuwezesha mke akae vizuri au kuistaajabisha jamii au taifa, endapo tu mke atakiona kipawa hicho na kukithamini. Hivyo, mke, anatakiwa atoe moyo wake wote kwa mume wake, badala ya kuthamini fedha kuliko mume wake.

Ni muhimu kupenda utu zaidi kuliko fedha au mali. Fedha au mali huweza kuja na kuondoka, lakini utu utakuwepo hadi mwisho.

FEDHA ni nyenzo ya kiuchumi inayosaidia katika kuishi. Tupende fedha kwa kiasi tu. MKE KUPENDA FEDHA KAMA DELILA, NI KUBOMOA NDOA YAKE KWA HULKA NA HIARI YAKE MWENYEWE.

Aidha, kupenda fedha kwa kiwango hicho (too much) kunaweza kusababisha mwenza wa ndoa kufanya jambo lo lote hasi, kama vile kuiba, kujidhuru, kudhuru, au kutoroka na kutelekeza ndoa, kwa kuogopa mbinyo wa kifedha kutoka kwa mke, au usalama binafsi katika ndoa dhidi ya wanaume wengine waharibifu.
 
Back
Top