Advertise here

Kuna tofauti kati ya ndoto ya Mungu na ya shetani

Kuna tofauti kati ya ndoto ya Mungu na ya shetani

Maarifa yanayohusiana na ndoto ni mapana. Hata hivyo, kwa ufupi, zipo ndoto za aina tatu.

1. Ndoto zinazotokana na shughuli unazofanya
Ndoto hizi ndizo mara nyingi zinamjia mtu. Kwa mfano: mtu alikuwa anafanya shughuli fulani siku nzima, usiku anapolala bado anaota anaifanya ile shughuli
. Au, anaota mambo yanayoendana na jambo ambalo amekuwa akijishughulisha nalo mara kwa mara.

Kutokana na shughuli ile kuchukua sehemu kubwa ya siku yake au maisha yake, inapelekea pia kuchukua nafasi kubwa katika ulimwengu wa ndoto zake. Ndoto hizi ni mwili ndio unaozitengeneza, hazitokani na Mungu wala shetani.

Kuhusu ndoto hizo, Mhubiri 5:3, anasema: "Kwa maana ndoto huja kwa sababu ya shughuli nyingi; na sauti ya mpumbavu kwa njia ya wingi wa maneno".

2. Ndoto zinazotokana na yule mwovu
Hizi zinatengenezwa na yule mwovu (shetani) na kutumwa ndani ya mtu
.
Hizi ni ndoto zote zenye maudhui ya kumfanya mtu aikane au aiache IMANI, au zinampelekea mtu aende mbali na mpango wa Mungu, au kutenda dhambi. Huwa zinaambatana na ushawishi fulani mkubwa sana, mara baada ya kuamka.

Kwa mfano, mtu anaota ameachana na mume/mke wake na kupata mke/mume mwingine, ambaye ni mzuri kuliko yule aliyekuwa naye. Na anapoamka asubuhi, anajikuta anaanza kuona kero ya kuishi na mke wake au mume wake kama ilivyokuwa hapo mwanzo. Au, anashawishika kuamua kumwacha mumewe au mkewe.

Au, mtu anaota mzazi wake mmoja ni mchawi na hamtakii mema, na ile ndoto inamtaka ajitenge na huyo mzazi, au amchukie awe mbali naye.

Au, wakati mwingine mtu anaota ndoto ameenda kwa mganga, akafanikiwa na anapoamka anashawishika kufanya mambo yale.

Au, wakati mwingine mtu anaota, ametenda dhambi na amejaribu kumwomba Mungu, na Mungu hataki kumsamehe, na anapoamka asubuhi anashawishika kuamini kuwa Mungu hataki kumsamehe na anamchukia.

Ndoto zote kama hizi, zinatoka kwa yule mwovu, kwa sababu zina maudhui ya kumlazimisha mtu asilitii Neno la Mungu, au aende kinyume na maagizo ya Mungu. Zinampeleka mtu katika kutenda dhambi zaidi kuliko kumfanya kuwa mtakatifu. Nyingine zinamfanya mtu awe mwoga zaidi na kumchukia Mungu kuliko kumpenda.

Jinsi ya kudhibiti ndoto hizi
Namna ya kuzidhibiti hizi ndoto ni kuamua kuishi maisha safi yampendezayo Mungu, na kujifunza kwa kina Neno la Mungu, ili shetani anapoleta mawimbi yake kama bahari, uwe na uwezo wa kuyadhibiti. Kadhalika kudumu katika maombi.

Kwa mfano, mtu anayeota amefanya kosa na hasamehewi, hiyo ni mishale ya shetani kutaka kukuvunja moyo usitake kuendelea kumtafuta Mungu.
Kama Neno halipo ndani yako linalosema, “Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote" (1Yohana 1:9), hutaweza kumshinda shetani.

Au, ndoto inapokuja umegombana na mke wako na umeachana naye na kupata mwingine bora kuliko huyo. Utajua imetoka kwa yule mwovu kwa sababu Neno la Mungu limekaa ndani yako linalosema "Kila amwachaye mkewe na kumwoa mke mwingine azini; naye amwoaye yeye aliyeachwa na mumewe azini" (Luka 16:18).

Kadhalika na ndoto nyingine zote zinazofanana na hizo utazipima kwa Neno la Mungu tu, na utaweza kuzishinda na kuzifahamu, kama Neno la Mungu limekaa ndani yako.

Na pia kusali kabla ya kulala ni muhimu sana. Hiyo itasaidia kufunga mipenyo yote ya yule mwovu anayoweza kuitumia kukujaribu katika ndoto.

3. Ndoto zinazotoka kwa Mungu
Hizi ni zile zinazomjia mtu kutoka kwa Mungu kwa maudhui ya kumwonya mtu au kumuimarisha katika imani
. Hizi haziwi kwa wingi kama zile zinazotokana na shughuli nyingi.
Mfano wa ndoto hizi ni pale mtu anapoota kukutana na mtu/mhubiri, kamshuhudia na kumwonya juu ya maisha yake maovu, na anapoamka asubuhi anajikuta anahukumiwa na maisha ya dhambi anayoishi na kushawishika kutubu.

Nyingine, ni zile mtu anaota amefanyiwa jambo baya sana la kumuumiza, na anapoamka asubuhi anajikuta yeye ndiye amemtendea mtu hilo jambo, hivyo anashawishika kujirekebisha na kutubu.

Nyingine, unakuta mtu anaota amebeti, au kwenda kwa waganga, au kufanya uasherati, au ameiba, au amemtukana mtu, au amechukua mke au mume wa mtu, au amemsengenya mtu, au ameua.
Na baada ya kufanya hivyo, mambo yake yote yakaharibika, akajikuta amefilisika, au amefungwa, au amehukumiwa kufa. Na anapoamka asubuhi, anashawishika kutofanya moja wapo ya mambo hayo, ili yasimpate hayo mabaya.

Hizo ni ndoto kutoka kwa Mungu, zinalenga kumuonya mtu.

Kwa hiyo kwa ufupi ndoto zote zinazotokana na Mungu utazijua kama Neno la Mungu limekaa ndani yako.

Ndoto yo yote inayokupeleka kumtafuta Mungu zaidi, kutubu, au kukuonya tabia uliyo nayo ambayo siyo nzuri, unajua kabisa ndoto hiyo inatoka kwa Mungu.

Lakini, uichukie imani au ujitenge na kweli, basi hiyo utajua moja kwa moja ni ya shetani.

Katika kuhitimisha, hebu tuangalie Ayubu 33:
14 "Kwa kuwa Mungu hunena mara moja, Naam, hata mara ya pili, ajapokuwa mtu hajali.
15 Katika ndoto, katika maono ya usiku, Usingizi mzito uwajiliapo watu, Katika usingizi kitandani;

Kwa ujumla, kuna aina tatu za ndoto.

NDOTO ZINAZOTOKANA NA SHUGHULI UNAZOFANYA
Ndoto hizi ndizo mara nyingi zinamjia mtu, kutokana na mtu kufanya shughuli fulani mara kwa mara au kwa muda mrefu.

NDOTO ZINAZOTOKANA NA SHETANI
Hizi zinatengenezwa na shetani na kutumwa ndani ya roho ya mtu. Hizi ni ndoto zote zenye maudhui ya kumfanya mtu aikane au aiache IMANI, au zinampelekea mtu aende mbali na mpango wa Mungu, au kutenda dhambi.

NDOTO ZINAZOTOKA KWA MUNGU
Hizi ni zile zinazomjia mtu kutoka kwa Mungu kwa maudhui ya kumwonya mtu au kumuimarisha katika imani.
 

Similar threads

Back
Top