Matumizi ya maneno damu na jina la Yesu

Matumizi ya maneno damu na jina la Yesu

Kumekuwa na mjadala kuhusu matumizi ya maneno DAMU ya Yesu na JINA la Yesu.


Hebu tuangalie misingi ya tofauti ya matumizi ya maneno hayo.

Kwa waaminio au wafuasi wa Yesu Kristo, je, damu ya Yesu ina kazi ya kutulinda sisi au mali zetu pale tunapoomba kupitia damu? Je, ni sahihi kuomba hivyo? Damu ya Yesu inatumikaje kwa wakristo?

Ili kuelewa tofuati ya utendaji kazi wa DAMU ya Yesu na JINA la Yesu, ni vizuri kwanza tukajifunza katika maisha ya kawaida. Katika maisha ya kawaida mtu anayo DAMU na vile vile analo JINA

JINA la mtu linaelezea utambulisho wa mtu yule, cheo alicho nacho, heshima aliyo nayo, nguvu aliyo nayo na mamlaka aliyo nayo. Kwa mfano, katika nchi yo yote, mtu mwenye jina kubwa na lenye nguvu kuliko wote ni Rais wa nchi hiyo.

Vile vile, katika upande wa pili, DAMU ya mtu inaelezea uzima wa huyo mtu, asili ya mtu huyo, undugu alionao na wanafamilia wenzake, ukoo, na inaelezea pia urithi alionao, yaani watu atakaowarithisha mali zake.

Kila Rais au Mfalme wa nchi, anayo DAMU na vile vile analo JINA.

Turudi katika mamla ka ya kimbingu, ambayo hiyo ni kuu kuliko ya kidunia.

Tunaye Mfalme mmoja, naye ni Yesu Kristo. Huyo ni zaidi ya Rais ye yote wa nchi. Na huyu analo JINA, na vile vile anayo DAMU.

Kama tulivyosema, damu inaelezea undugu wa mtu, yaani uana-familia.

Na Yesu pia anao ndugu zake wa damu, ambao ni wale wote waliozaliwa mara ya pili. Hao wanayo mamlaka ya kumsogelea katika meza yake na kula naye, na kumwomba lolote kwa jina lake na kupewa.

Mtoto wa mfalme akiomba apewe jimbo fulani kutoka kwa baba yake, haitachukua mlolongo mrefu kupewa haja ya moyo wake. Mara moja tu baba yake atamwandikia hati ya nakala kwa JINA lake, na kuipeleka mahali husika kupata anachokihitaji. Na huyo mtoto kwa JINA la baba yake, anaweza kupata lolote katika nchi.

Lakini hebu mtu wa kawaida tu amsogelee mfalme wa nchi na kumwomba apewe hicho kipande cha ardhi, uone mlolongo wake. Anaweza kufukuzwa, au hata asipofukuzwa, basi ombi lake linaweza kuchukua muda mrefu kujibiwa.

Yote hayo ni kutokana na nini?
Ni kutokana na kwamba mtoto wa Mfalme anatumia DAMU kupata lolote kwa JINA la baba yake, wakati ambapo kwa wengine, wanatumia bahati tu. Kwamba kwa wengine, maombi yao yakikubaliwa ni kama wamepata bahati tu. Wangeweza kukataliwa.
Lakini mtoto wa Mfalme ana uhakika wa kukubaliwa ombi lake kwa sababu anatumia DAMU.

Je ni sahihi kuomba kutumia damu ya Yesu kutulinda na mali zetu?
Kulingana na maelezo ya hapo juu, mtu aliyeokoka tayari damu ya Yesu inanena mema juu yake, kwani tayari ni mwanafamilia. Haihitaji kumweleza sana Baba wa mbinguni kwamba anahitaji ulinzi. Kitendo tu cha kuwa mwanawe wa DAMU, tayari ni jukumu lake kukulinda wewe na mali zako, na pia kwa JINA lake kupewa cho chote katika huu.

Ni tofauti na mtu ambaye hajaokoka? Ndiyo, ni tofauti.

Huyo si mwana wa Mungu. Si damu yake. Hana uhusiano wo wote na damu ya Mungu. Kwa hiyo, hata akiomba lolote kwa jina la Yesu, kwake ni bahati nasibu kupata anachokiomba.

DAMU YA YESU INAFANYA KAZI ZIFUATAZO:

Hutengeneza agano jipya kati ya Mungu na mwanadamu aliyemwamini Yesu (Marko 14:24).

Hufuta dhambi zote za mtu anayetubu kwa Mungu katika Yesu (Mathayo 26:28).

Huleta upatanisho kati ya mwanadamu anayeokoka na Mungu (Warumi 3:25).

Husafisha dhamiri, nafsi na mioyo yetu (Waebrania 9:13-14).

Inaleta ulinzi katika mwili, afya, familia, biashara, ndoa, nk kulingana na maombi ya mkristo mhitaji anayeomba (Ufunuo 12:11).

Hututakasa na kutufanya tuwe huru (Waebrania 13:12).

Hutufanya tukae ndani ya Yesu (Yohana 6:54-56).

Imetununua tuliookoka ili tuwe wa Mungu kwa ajili ya uzima wa milele (Matendo 20:28).

Hutufanya tuhesabiwe haki mbele za Mungu (Warumi 5:9).

Huleta ukombozi kwetu tuliompokea Yesu kama mwokozi wetu (Waefeso 1:7).

KAZI ZA JINA LA YESU

Jina la Yesu limebeba uungu wote wa kufanya mambo ambayo hakuna awezaye kufanya isipokuwa Mungu peke yake.

Mstari wa kusimamia: "Kwa maana kila atakayeliitia jina la BWANA ataokolewa" (Warumi 10:13).

Kwa ujumla wake, jina la Yesu limebeba kazi mbili KUBWA (broad), kama ifuatavyo:

1. Ulinzi wa kiroho na kimwili
Kwa jina lake tunalindwa katika ulimwengu wa damu na nyama na ulimwengu wa roho (Yoh 17:12).

2. Fimbo ya kuchapia nguvu za giza
Hakuna fimbo inayouma kama fimbo ya jina la Yesu. Pale ambapo kuna nguvu za giza, ukitamka jina la Yesu tu bila hata kuweka maneno mengi, ujue nguvu za giza, mbali na kushindwa, lakini zinaumia sana kiasi kwamba zinapiga kelele.

Tufanyeje ili kunufaika kwa kutumia DAMU na JINA la Yesu

Ni muhimu kuhakikisha kuwa umefanyika kuwa mwana wa Mungu, ili uwe DAMU moja na Mungu. Kama hujaokoka, basi fahamu kuwa ni vigumu kupokea upendeleo wo wote kutoka kwa Mungu.

Hii ni kwa sababu Mungu anawaangalia kwanza wanawe kuwapatia mema (Warumi 8:28-29). Na hao ndio atakaowarithisha uzima wa milele.

Hawezi kuwarithisha watu wasio wanawe. Hata wewe mwenyewe ni vigumu kumrithisha mtoto asiye wako, mali zako na kuwaacha wanao bila urithi.

Nini cha kufanya?
Cha kufanya ni kubatizwa kwa mara ya pili na kupokea Roho Mtakatifu.
Utakuwa umezaliwa mara ya pili na kuhesabika mwanafamilia wa familia ya kimbingu, na hivyo kuwa mrithi na ile DAMU ya thamani isiyoisha muda wa matumizi.

DAMU ya Yesu Kristo itaanza kunena mema juu yako.

DAMU ya Yesu inaleta ulinzi katika mwili, afya, familia, biashara, ndoa, nk, kulingana na maombi ya mkristo mhitaji anayeomba (Ufunuo 12:11). Hapa unahitaji tu kufanya maombi ili damu ya Yesu ifanye kazi kama ulivyoomba katika maombi yako.

Tukumbuke kuwa maagizo ya Yesu Kristo ni kumwomba Mungu kwa JINA la Yesu (Yohana 14:13-14; Yohana 16:23-24).

Ukishakuwa mwanafamilia, ukiomba jambo lo lote kwa JINA la Yesu, utapata.
 
Back
Top