Kasomi
JT Founder
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Dkt. Bill Kiwia, amesema kuwa namba ya utambulisho wa taifa itakuwa ni ya lazima katika kuomba mkopo kwa mwaka ujao wa masomo. “Tunatarajia kufungua dirisha la maombi ya mkopo mwezi Juni, 2025… kwa mwaka wa masomo wa 2025/2026 namba ya utambulisho wa taifa itakuwa hitaji la lazima katika maombi ya mkopo”, amesema Dkt. Kiwia.
Ameyasema hayo leo mei 16, 2025 katika kikao cha Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na waandishi wa habari katika ofisi za HESLB Kanda ya Mashariki zilizopo Dar es Salaam kwa lengo la kuutarifu umma kuhusu kuanza kushirikiana kuwapatia namba ya utambulisho (NIN) wanafunzi wanaotarajia kujiunga na vyuo vikuu kwa mwaka wa masomo wa 2025/2026.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, Bw. James Kaji, amesema kuwa NIDA wapo tayari kuwahudumia wanafunzi wote wanaotarajia kujiunga na vyuo vikuu na kuomba mikopo kutoka HESLB kwa kuwapatia namba za utambulisho kwa wakati na hivyo wanafunzi wanapaswa kufika kwenye ofisi za NIDA mapema ili kupatiwa namba za utambulisho.
Kuhusu kurahisisha huduma kwa waombaji wa namba za utambulisho wa taifa, Bw. Kaji amesema NIDA imeboresha huduma kwa njia ya mtandao na kusisitiza waombaji wa namba za utambulisho wa taifa kuingia kwenye mtandao wa NIDA kwa kutumia kiunganishi https://eonline.nida.go.tz ili kuwasilisha maombi yao.