MY STORY; Mfanyakazi Kutoka Nyumbani

Simulizi

Member
MY STORY; Mfanyakazi Kutoka Nyumbani!

Kuna wakati nililetea mfanyakazi kutoka nyumbani kwetu, aliyenitafutia alikuwa ni mama yangu mzazi. Hii ni baada ya kusumbuka sana kutafuta wasichana wa kazi. Mwanzo wakati anakuja kila kitu kilikuwa vizuri, alikuwa anahudumia watoto vizuri na mke wangu alimpenda sana. Lakini baada ya kama miezi miwili hivi nilimuona kama amebadilika.

Mimi si mtu wa kufuatilia mambo ya msichana wa kazi, lakini kuna kitu nilikiona kama hakiko sawa. Mwanzo akiwa nyumbani alianza kuwa anafanya kazi sana, anajitahidi sana kwa watoto, yaani unajua ile kama una akili unajua kabisa anaigiza, ndiyo hiyo. Basi mimi nikachukulia poa kwa sababu mke wangu alikuwa halalamiki kabisa, alikuwa anakaa kimya. Lakini sasa simu za nyumbani zikawa hazikomi, mama akawa ananipigia simu ananiulizia mambo ambayo yanatokea kwenye familia yangu.

“Mkeo hivi,” “mkeo kafanya vile,” ukiangalia kuna vitu vya kweli labda nilikwaruzana na mke wangu kitu cha kawaida. Kwa mfano, mimi siwezi kula chakula bila chai ya maziwa, sasa unakuta siku nyingine mke kasahau kuandaa maziwa, mimi nikakasirika kidogo, si ile ya kununa, hapana, ni ile ya kusema:

“Ina maana hukujua maziwa yameisha?”
Basi mke wangu akaomba msamaha, yanaisha utasahau, unashangaa kesho yake mama anakupigia simu anaongelea kitu kilekile!

Kwakweli nilikuwa nakerwa, siku hiyo nikamuuliza mke wangu kuhusu chai ya hapo, akanijibu kuwa hakukuwa na shida, mbona ni kawaida. Niliona mabadiliko, kuna siku sasa hajatoka kwenda kazini, niko zangu ndani nimelala, huko jikoni nasikia binti anamjibu mke wangu:

“Utaondoka huyu ni kaka yangu, yeye ndiye aliyenileta hapa! Kwa taarifa yako nikimpigia simu moja tu narudi kwetu.”
Akamtolea mke wangu maneno makali, mke wangu akakaa kimya.

Sikuongea chochote, mke wangu akarudi chumbani alikuwa kama analia lakini naye ni kama alishashtuka kuwa niko ndani kwani aliponiona akawa kama ameshtuka, basi mimi nikamuuliza:

“Mbona binti anakujibu kijinga hivyo, jina gani hiyo hufanyi chochote?”
Yaani hicho kisichana kinakujibu hivyo, unaangalia si ungemkemea awe na adabu!
Mke wangu akajibu akisema,
“Acha hayo, huyo binti ni utoto tu!”

Mimi nikasema:

“Hapana.”
Nikatoka nikamfuata yule binti na kumwambia:
“Beba mizigo yako uondoke!”
Lakini kabla sijatoka, mara simu ya mke wangu ikaita, ni mama yangu anap*iga.
Mke wangu akakataa kupokea, mama akap*iga tena, nikahisi kuna kitu.
Nikachukua nikapokea, hata kabla sijasema “hallo”, mama akaanza kumtukana mke wangu.
Nikamuuliza:
“Hivi unamtukana huyo binti, umemzidi nini? Unafikiri hapa kwa mtoto wangu nikitaka si anaondoka?”
Akamtolea maneno mengi mke wangu, mke wangu akaanza kulia, anaomba msamaha.

Mimi wakati huo hasira zimeshapanda, ukiangalia ni asubuhi, jana yake sijapata usingizi halafu wanataka kuniharibia usingizi wangu. Yaani wameniwekea vurugu, mke wangu alikuwa hausiki kabisa, nilisema hawa hawanijui.
Mama akaongea wee mara anasema:

“Nikitaka uachike, utaachika, huyo binti nimemleta mimi, sitaki umpelekeshe.”
Mke wangu akaomba msamaha, mama akakata simu!

Hata sijamuuliza mke wangu shida ni nini, haya mambo yameanza lini. Simu ya mama inaingia, ananipigia mimi! Nikapokea hata bila salamu, analia, anaanza kuniambia kuwa mke wangu sijui anamnyanyasa binti, sijui anamnyima chakula, anaongelea mabaya kuhusu mimi na mambo kibao.
Wakati naona mimi hasira zinapanda, nusu nitukane, lakini mke wangu ndiye alikuwa ananisihi, ananiambia:

“Tulia! Tulia!”
Basi mama akaona nimekaa kimya, nikamuambia:
“Usijali, leo ndiyo mwisho wa haya mambo nitayashughulikia mwenyewe!”

Akakata simu, nikasema:

“Hapana, huyu mama hajanijua. Hivi anajua nimetoka wapi na huyu mwanamke, halafu ananichukuliaje mimi, Yeye ndiyo wa kuniambia jinsi ya kuishi na mke wangu?”
Nikatoka kwa hasira, nikafika nje binti anongea na mama.
Sikutaka kumshtua, hakuniona nikarudi chumbani. Nililala ndani mpaka jioni ndipo nikajifanya nimerejea kutoka kazini.
Kesho yake Asubuhi na mapema, nilimwambia binti:
“Ingiza mizigo yako kwenye gari.”
Nikamuambia mke wangu:
“Samahani, atachukua mizigo yake yote hata mswaki alioleta alikusanya!”

Binti hakutegemea, nilichukua simu ambayo ni ya mke wangu niliyomnunulia, kisha nikamwambia twende. Nikajaza mafuta mpaka Morogoro. Hapa sikumuambia mtu yeyote kwa sababu sikuwa napatikana kwa simu na mimi nilimshtukiza. Alivyofika, mama alishangaa kuona nimekuja na binti. Ananiuliza, “Vipi?” Nikamwambia,

“Mama, siwezi kuachana na mke wangu kwa sababu yako. Hukumuoa wewe, siwezi kuachana na mke wangu kwa ajili ya huyu binti. Watoto wangu walelewe na mwanaume mwingine wakati mke wangu sijamuacha?”

Sasa huyu binti nimemleta, si mtaji kwangu. Na wewe mama, kama kuna kitu mke wangu amefanya, unanipigia simu unaongea na mimi. Huna mamlaka ya kumtukana mke wangu, huna mamlaka ya kumtishia. Unaniamrisha mimi kama mwanao, lakini huyo ni mke wangu. Ni mimi pekee nina haki ya kumwambia kitu, si wewe, si baba, si ndugu yeyote! Mama alinigeukia na kuanza kulia. Nikamwambia,

“Mama, lia. Toa machozi, yanasaidia kutoa hasira na kupunguza kisirani. Lakini leo iwe mwanzo na mwisho wa kumpigia simu mke wangu na kumtukana.”

Akajifanya kama hakumtukana. Nikamwambia,

“Wakati unamtukana, nilikuwa pembeni yake. Nilikuwa nasikia akiniambia nisikujibu.”
Sikutaka hata kukaa, nilitaka kuondoka zangu. Mama akaniambia:
“Kama mimi ni mama yako basi utaachana na huyo mwanamke. Lakini ukiendelea kuwa naye, mimi si mama yako.”

Niligeuka nikacheka, nikamwambia,

“Mama, hakuna laana za hivyo. Isitoshe, mimi sijui kama wewe ni mama yangu kweli au la. Nimejikuta ukubwani watu wanasema huyu ni mama yako. Sasa kama kweli ni mama yangu utanitakia niwe na furaha, lakini kama ulipewa tu unilee, basi utakuwa unahangaika nisiwe na amani! Kama unataka kunipa laana ya kuwa mwanao, basi nipe hiyo laana niondoke nayo, lakini huwezi kunipangia maisha na mke wangu!”

Nilitoka mpaka kwenye gari. Nilijua nimeongea maneno magumu, lakini nilikuwa na hasira, na katika maisha yangu niliwahi kuapa kuwa hakuna mtu wa kuvunja ndoa yangu, labda mke wangu mwenyewe aamue kuivunja, si ndugu. Nilipofika kwenye gari, nilikaa kama dakika tano hivi kisha nikaweka nia ya kuondoka. Mama yangu akatoka na kusimama mbele yangu, akiniomba nishuke.

Sikuwa na namna, nilishuka. Niliposhuka tu alianza kuniomba msamaha, akitaka kupiga magoti, nikamshika nikamwambia,

“Mama hapana.”

Alinirudisha ndani mpaka chumbani, kisha akaanza kuniambia:

“Mwanangu, nisamehe. Sijui kwa nini nimekuwa hivi, lakini ninaumia sana. Kila nikiona jinsi unavyoishi na mke wako, una mke mzuri anakujali na anakupenda sana, lakini mimi sina amani!”
Akaanza kuniambia jinsi alivyonyanyasika kipindi cha ndoa yake, jinsi baba alivyo kuwa anampiga, jinsi mashangazi walivyokuwa wanamtukana. Akaniambia jinsi alivyo kuwa anampikia baba chakula lakini haruhusiwi kula hata kwa siku mbili.

Amezaa watoto wanne lakini wote hawana ndoa za amani. Dada yako mmoja amezaa nyumbani watoto watatu na sasa anaishi na mume wa mtu, mwingine ameolewa lakini yeye ndiye anamhudumia mwanaume, mwingine, na huyu wa mwisho ndiyo hatujui kama ni mgonjwa au vipi, ana miaka 45 hana hata mume. Mtoto wangu ni wewe, una maisha mazuri, anaumia kwa nini mke wako apate mume mzuri kama wewe wakati mabinti zake wanateseka.

“Juzi ulinunua gari kwa ajili ya mke wako, sijui mmeenda mpaka wapi na mke wako wakati mimi wanangu hawana waume wa maana. Nimejikuta na hisia za wivu. Nisamehe!”

Aliongea vitu vingi ambavyo hata sikujua kama kapitia. Alionyesha jinsi baba alivyo mtesa, wakati mimi nilikuwa namuona baba kama malaika. Nilijikuta nalia, nikamwambia,

“Mama, yameisha.”

Alimpigia simu mke wangu akitaka kumuomba msamaha, nikamwambia:

“Hapana, yule ni mke wangu, nitamalizana naye mimi.”
Sikutaka mama aendelee kujishusha, nilijua mke wangu tutaongea naye na yataisha. Kweli nilirudi, nikaongea na mke wangu, akampigia simu mama na kumuambia:
“Nimekusamehe mama, nina amani.”

Nilitafuta mfanyakazi mwingine kutoka sehemu nyingine, lakini tangu siku hiyo sijasikia tena ishu ya simu, sitaki huyo mwanamke. Mpaka leo, mama na mke wangu wanaishi kwa amani!

Hivyo mwanaume mwenzangu, najua unapenda ndugu zako, lakini je, wanaposema wanamchukia mke wako, ni kwa sababu mke wako ni mtu mbaya, au ni wivu tu?
Usihitimishe ujumbe huu haraka — labda kuna mtu atajifunza.
 

Similar threads

Back
Top