Advertise here

Kona ya Mwalimu: Kwanini Unaweka Hali ya Ndoa kwenye CV Bila Kuombwa? Mwaajiri Anatafuta Mfanyakazi, si Mchumba

Kasomi

JT Founder
KWANINI UNAWEKA HALI YA NDOA KWENYE CV BILA KUOMBWA? MWAAJIRI ANATAFUTA MFANYAKAZI, SI MCHUMBA.
1777097544012.jpg

Huu ukweli watu wengi bado hawajaupokea.

CV si fomu ya maisha yako yote. CV ni waraka wa kazi. Inapaswa kumwonesha mwajiri jambo moja tu, una uwezo gani na unafaa kwa nafasi hiyo kwa sababu gani.

Lakini bado watu wanaweka kwenye CV:
Hali ya ndoa.
Dini.
Idadi ya watoto.
Kabila.
Picha zisizo za kitaaluma.
Na wakati mwingine hadi uzito na urefu kama wanaomba kazi ya ulinzi wa lango la airport au klabu ya kula maisha.

Tusipende kujipa moyo kwenye mambo yasiyo sawa. Mambo mengine kwenye CV yako hayakusaidii kupata kazi. Yanajaza nafasi tu na wakati mwingine yanakufanya uonekane hujui soko la ajira la sasa linataka nini.

Hali ya ndoa na mambo mengi niliyotaja hapo si lazima kwenye CV.
KAMA MWAJIRI HAJAOMBA, usiweke.
KAMA FOMU ya MAOMBI HAIJATAKA, usiweke.
KAMA HAIHUSIANI moja kwa moja na UWEZO WAKO wa KAZI, usiweke.

Mwajiri anataka kujua:
Umesoma nini.
Una uzoefu gani.
Unaweza kufanya nini.
Umeleta matokeo gani.
Una ujuzi gani unaoweza kusaidia taasisi yake.

Hayo ndiyo mambo yanayobeba CV. Siyo kuandika "single" au "separated", halafu, ukategemea hiyo ikupeleke interview.

CV ya kisasa inaondoa mambo yasiyo na tija na inaweka nguvu kwenye thamani yako.

Kwa hiyo, kabla hujatuma maombi tena, pitia CV yako ujiulize,
Hapa nimeandika vitu vya kazi, au nimeandika wasifu wa familia?

Watu wengi hawakataliwi kwa sababu hawana uwezo.
Wanakataliwa kwa sababu CV zao zinaonesha hawajajifunza namna ya kujitangaza kitaaluma.

Na kwenye soko la ajira la leo, kosa dogo kwenye CV linaweza kukutoa nje kabla hujapata nafasi ya kujieleza.

Credit: James Dea Elias
Kona ya Mwalimu!
 
Back
Top