Kasomi
JT Founder
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Mohamed Salum, amesema meli ya MV Mwanza, ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 98, inatarajiwa kufanyiwa majaribio mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu.
Akizungumza mkoani Mwanza baada ya kukagua maendeleo ya mradi huo, Salum amesema ujenzi wa meli hiyo umezingatia viwango na taratibu zote za usalama wa majini kama inavyotakiwa kimataifa.
Ameeleza kuwa maeneo mengi ya meli hiyo, ikiwemo sehemu ya injini, yamekamilika kwa asilimia 100, huku kazi kubwa iliyobaki ikiwa ni ufungaji wa vitanda katika vyumba vya kulala kwa abiria.
Salum ameongeza kuwa mafanikio hayo ni sehemu ya jitihada za serikali kuboresha usafiri wa majini na kwamba kukamilika kwa meli hiyo kutaimarisha huduma za usafiri baina ya mikoa ya Mwanza na Kagera.
Meli hiyo imejengwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 128 na inatarajiwa kuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wakazi wa Ukanda wa Ziwa Victoria.
Chanzo: TBC online