Kasomi
JT Founder
Aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Ester Bulaya, ametangaza rasmi nia yake ya kugombea Ubunge wa Jimbo la Bunda Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM). Hatua hiyo imekuja ikiwa ni sehemu ya mchakato wa ndani ya chama hicho tawala ambao umeanza leo Juni 28, 2025, kwa wanachama kujitokeza kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Ester Bulaya ambaye pia aliwahi kuwa Mbunge wa Bunda Mjini kwa tiketi ya CHADEMA katika Bunge la 11 (2015–2020), amesema ameridhia kurudi nyumbani kwa ajili ya kuendelea kuwatumikia wananchi wa jimbo hilo kwa moyo na ari mpya kupitia CCM. Ameeleza kuwa dhamira yake ni kuendeleza maendeleo na kushirikiana na Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Nimerudi Bunda nikiwa na moyo uleule wa kutumikia watu. Nimeamua kuomba ridhaa ya chama ili niweze kupeperusha bendera ya CCM katika Jimbo la Bunda Mjini. Nawaomba wana CCM waniamini,” alisema Bulaya mbele ya wanahabari.
Tangazo hilo limepokelewa kwa hisia mseto kutoka kwa wakazi wa Bunda na wanasiasa wenzake, ambapo wengi wameeleza kuwa ushindani utakuwa mkali katika kura za maoni ndani ya CCM kwa jimbo hilo ambalo lina historia ya kisiasa ya ushindani mkubwa.