Fahamu kuhusu Utakatishaji Fedha (Money Laundering)

Kasomi

JT Founder
1764281364076.jpg

1.0 UTANGULIZI

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (Tume) ilianzishwa mwaka 1980 kwa Sheria ya Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, Sura ya 171. Kwa mujibu wa Sheria hii pamoja na majukumu mengine, Tume ina majukumu ya kupitia na kutathmini utekelezaji wa sheria zote za Jamhuri ya Muungano kwa lengo la kuziwezesha sheria hizo kuendana na mabadiliko yanayotokea katika nyanja za kijamii, kisiasa, kiuchumi, kisayansi na teknolojia. Aidha, Tume ina jukumu la kutoa elimu ya sheria kwa umma.

2.0 UTAKATISHAJI FEDHA

Fedha inayopatikana kutokana na vitendo vya jinai inatambulika kama fedha chafu. Watendaji wa makosa ya jinai hulazimika kuziingiza fedha hizo katika mfumo wa fedha wa kawaidaili ziwe halali. Hivyo basi kwa kifupi utakatishaji fedha ni kitendo cha kuweka fedha iliyotokana na uhalifu katika shughuli halali ili iingie katika mzunguko wa kawaida wa fedha kwa lengo la kuhakikisha wahalifu hao wanafaidika kutokana na vitendo vya kihalifu. Vilevile, wahalifu wanatakatisha fedha hizo ili kuhakikisha Serikali inashindwa kujua chanzo, kufuatilia na kutaifisha fedha hizo.

3.0 UMUHIMU WA KUZUA UTAKATISHAJI WA FEDHA

Moja ya malengo ya mfumo wa jinai ni kuhakikisha mhalifu hafaidiki na vitendo vya kihalifu. Njia hii pia inasaidia kuonyesha jamii kuwa vitendo vya kihalifu havina manufaa. Kukosekana kwa mfumo imara wa kudhibiti utakatishaji wa fedha kunaweza kusababisha wahalifu kuwa na nguvu kubwa ya kifedha na hivyo kuvuruga amani na usalama na pia inaweza kuchangia kuongezeka na kushamiri kwa vitendo vya rushwa

4.0 MADHARA YA UTAKATISHAJI FEDHA

Hufanya uhalifu kushamiri sababu fedha inayotakatishwa na wahalifu hutumika tena kutenda uhalifu na hivyo vitendo vya kihalifu kuwa endelevu.

Utakatishaji fedha huwezesha wahalifu kutengeneza magenge makubwa ya uhalifu yanayowapa nguvu ya kifedha hivyo inaweza kusababisha ukosefu wa amani na usalama katika jamii kwa ujumla.

Hurudisha nyuma maendeleo ya taifa kwasababu utakatishaji fedha huweza kudhoofisha biashara na kuathiri shughuli za kibenki katika kukuza uchumi. Uchumi ukishuka hushusha sifa ya nchi na kukimbiza wawekezaji.

Utakatishaji fedha ni tishio kwa ustawi wa uchumi, siasa na jamii kwa ujumla. Wahalifu huweza kutumia fedha hizo kutoa rushwa kwa ajili ya kupata nguvu kimamlaka kwenye jamii ili kuendelea kufanya uhalifu.

Huchochea ugaidi; kwa kupitia fedha zilizotakatishwa magaidi huweza kuwapa mtaji vikundi vingine vya ugaidi kwa ajili ya kuwawezesha kufanya vitendo vya ugaidi katika nchi na kuharibu amani ya nchi.

5.0 SHERIA YA KUZUIA UTAKATISHAJI FEDHA

Sheria hii inaeleza kuwa mtu yeyote atahesabika ametenda kosa la utakatishaji wa fedha ikiwa atafanya yafuatayo:-

atajihusisha moja kwa moja au kwa kificho katika muamala unaohusiana na mali ambayo ni zao la kosa tangulizi wakati akijuwa mali hiyo ni zao la kosa hilo;

⚫ atabadilisha, atahamisha au atasafirisha mali wakati akijuwa kuwa mali hiyo ni zao la kosa tangulizi kwa nia ya kuficha au kudanganya chanzo cha mali au kumsaidia mtu yeyote anayehusika katika kutenda kosa tangulizi ili aweze kukwepa hatua za kisheria kutokana vitendo vyake;

ataficha, atadanganya au kuzuia kupatikana ukweli kuhusu chanzo, mahali, uuzwaji, uhamishaji au umiliki wa haki ya mali husika wakati akijuwa mali hiyo ni zao la kosa tangulizi.

⚫ atapata, atamiliki au kutumia mali huku wakati anapokea mali hiyo alifahamu kuwa ni zao la kosa tangulizi.

Sheria ya Kuzuia Utakatishaji wa Fedha imeeleza kuwa "kosa tangulizi" ni kosa kubwa kama inavyotafsiriwa katika Sheria ya Mazalia ya Uhalifu. Kosa kubwa katika Sheria ya Mazalia ya Uhalifu imetafsiri ni kosa kubwa kuwa ni kosa lolote ambalo ni kinyume na sheria ambalo adhabu yake ni kifo au kifungo kisichopungua miezi 12, na kosa lolote ambalo mali imetumika au mazalia yalipatikana au faida imepatikana.
 
Back
Top