Advertise here

Je ni lazima kubadilisha jina baada ya kuokoka?

Je ni lazima kubadilisha jina baada ya kuokoka?

Katika biblia Mungu hakuwabadilisha watu majina kutokana na tafsiri za majina yao.
Ni muhimu sana kufahamu hili, vinginevyo shetani anaweza kukutesa na tafsiri ya jina lako.

Hii ni kwa sababu usipomwelewa Mungu jinsi anavyotenda kazi, utachukuliwa na kila aina ya upepo wa elimu, na mafundisho ya mashetani, ambayo kazi ya hizo elimu ni kuwafunga watu wala siyo kuwafungua, kuwatwisha watu mizigo mizito na wala si kuwatua.

Kitabu cha Yohana 8:36, kinasema: “Basi Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli”.

Tuangalie watu wachache waliobadilishwa majina katika biblia, na tafsiri za majina yao kabla na baada ya kubadilishwa, ndipo tutajua tabia ya Mungu.

IBRAHIMU

Huyu mara ya kwanza alikuwa anaitwa “Abramu”. Tafsiri ya jina Abramu ni “Baba aliyeinuliwa”, na Ibrahimu tafsiri yake ni “Baba wa mataifa mengi”.

Kulingana na tafsiri hizo, siyo kwamba Mungu aliona tafsiri ya jina lake la kwanza ilikuwa ni mbaya, na hivyo akataka kumpa jina jipya lenye tafsiri nzuri, hapana. Ilikuwa ni nzuri tu kuitwa “Baba aliyeinuliwa” siyo jina baya. Lakini ilipofika wakati wa Mungu kumpa agano kwamba atakuwa Baba wa mataifa mengi, ndipo jina lake likabadilishwa na kuwa Ibrahimu.
Jina lilibadilishwa kwa sababu ya huduma iliyokuwa mbele yake.

SARA

Huyu alikuwa ni mke wa Ibrahimu, ambaye hapo kwanza alikuwa anaitwa “Sarai”, maana yake ni “binti wa mfalme”. Lakini jina lake lilibadilishwa na kuwa “Sara”, ambalo maana yake ni “mama wa wana wa wafalme”. Hivyo, halikubadilishwa kwa sababu lilikuwa na maana mbaya, hapana, bali ni kwa sababu ya ahadi ya Mungu, kwa mumewe Ibrahimu, kuwa Baba wa mataifa mengi, hivyo hana budi na yeye kuwa mama wa mataifa na wafalme wengi.

Ni sawa kama wewe ubadilike kutoka kuitwa mtoto, na kuitwa Baba wa watoto wengi, au kutoka kuitwa binti na kuitwa mama wa mabinti wengi. Hiyo inakuwa ni kutokana na kubadilika majukumu, umetoka kwenye utoto sasa umeingia kuwa baba/mama.

YAKOBO
Yakobo alikuwa ni mwana wa Isaka. Jina lake lilibadilishwa kutoka kuitwa Yakobo hadi kuitwa Israeli. Tafsiri ya jina “Yakobo” ni “mshika kisigino”. Jina hilo aliitwa kutokana na jinsi alivyozaliwa, kwani alipozaliwa, alizaliwa huku ameshika kisigino cha ndugu yake (Esau), wakiwa tumboni mwa mama yao (Mwanzo 25:26). Na tafsiri ya jina Israeli ni “Kushindana na Mungu”.

Jina la Yakobo halikubadilishwa kutokana na tafsiri yake ni mbaya. Hapana, bali ni kutokana na ahadi mpya Mungu aliyokwenda kumpa baada ya kushindana na yule malaika na kumshinda (Mwanzo 32:25-28).

Hii ni kwa sababu kama tafisiri ya jina Yakobo lingekuwa ndiyo sababu ya Mungu kumbadilisha jina, basi Mtume wa Yesu aliyeitwa Yakobo, angepaswa naye pia abadilishwe jina.
Na aliyeandika kitabu cha Yakobo, naye pia angepaswa abadilishwe jina. Lakini tunaona hawakubadilishwa majina, bali waliendelea kuwa Mitume wa Yesu, waaminifu hadi mwisho.

PETRO
Petro hapo awali alikuwa anaitwa Simoni. Yohana 1:42: “Akampeleka kwa Yesu. Naye Yesu akamtazama, akasema, Wewe u Simoni, mwana wa Yohana; nawe utaitwa Kefa (tafsiri yake Petro, au Jiwe)”.
Tafsiri ya jina Simoni ni “Amesikia”, na tafisiri ya Kefa/Pertro ni “jiwe dogo la kurusha” na siyo “mwamba”. Hivyo kwa hali ya kawaida, Simoni ndilo lenye tafsiri bora kuliko Petro.
Lakini utaona Bwana Yesu hakumbadilisha jina Simoni kwa sababu lina maana mbaya, hapana, bali ni kwa sababu ya huduma yake inayokwenda kuanza, kwamba Bwana angemtumia kama jiwe lake, kwa kazi yake.

Jina “Simoni” lingekuwa na tafsiri mbaya inayomchukiza Mungu au yenye madhara kiroho kwa Petro, basi angembadilisha pia mtume wake mwingine miongoni mwa wale 12, ambaye naye pia alikuwa anaitwa Simoni Mkananayo (Mathayo 10:4); kwa sababu Bwana asingeweza kumbadilisha mtume mmoja na kumwacha mwingine mwenye jina hilo hilo.
Kwa hiyo Petro naye alibadilishwa kutokana na huduma iliyokuwa mbele yake.

SAULI
Mwingine tunayeweza kumwona ni Mtume Paulo, ambaye hapo awali alikuwa anaitwa “Sauli” ambapo tafsiri ya jina hilo ni “Ombea” (mfano, kuombea kitu fulani kwa Mungu). Hiyo ndiyo tafisiri ya jina Sauli. Lakini jina hilo lilikuja kubadilishwa na kuwa “Paulo” ambalo maana yake ni “Mdogo”.

Hivyo unaona hapo, jina lake halikubadilishwa kwa sababu lilikuwa na tafsiri mbaya. Hata katika hali ya kawaida ungeambiwa uchague uitwe jina lenye tafsiri ya “mdogo” au uitwe jina lenye tafsiri ya “ombea”, bila shaka ungechagua lenye tafsiri ya “ombea”. Lakini Mungu alimbadilisha Sauli na kumpa hilo jina lenye tafsiri ya mdogo.

Na kwa nini Mungu alimpa jina hilo Paulo? Ni kwa sababu ya huduma yake, ambayo angekwenda kuifanya hapo mbeleni, ambapo, ingempasa awe mdogo sana na mnyenyekevu.
Kuhusu uhudumu, Waefeso 3 inasema:
7 “Injili hiyo ambayo nalifanywa mhudumu wake, kwa kadiri ya kipawa cha neema ya Mungu niliyopewa kwa kadiri ya utendaji wa uweza wake.
8 MIMI, NILIYE MDOGO KULIKO YEYE ALIYE MDOGO WA WATAKATİFU WOTE, nalipewa neema hii ya kuwahubiri Mataifa utajiri wake Kristo usiopimika;
9 na kuwaangaza watu wote wajue habari za madaraka ya siri hiyo, ambayo tangu zamani zote ilisitirika katika Mungu aliyeviumba vitu vyote”.

Jambo la kujifunza
Jambo kubwa la kujifunza ni kwamba, tafsiri za majina yetu, hazina maana sana mbele za Mungu wetu. Ndiyo, ni vizuri kuwa na jina lenye tafsiri nzuri, lakini hilo halikusogezi karibu na Mungu. Hiyo ni kwa sababu majina yaliyoandikwa kwenye kitabu cha uzima, hayajaandikwa kulingana na maana za majina hayo, bali kulingana na matendo ya mtu.


Watakuwepo wengi mbinguni ambao majina yao hayana tafsiri nzuri. Vile vile, watakuwepo wengi kuzimu wenye majina mazuri. Watakuwepo wakina Ibrahimu wengi kuzimu, watakuwepo wakina Paulo wengi kuzimu, watakuwepo wakina Petro wengi kuzimu, na watakuwepo wakina Yohana wengi kuzimu.

Vile vile, watakuwepo wakina Sauli wengi mbinguni, watakuwepo wakina Yakobo wengi mbinguni, watakuwepo wakina Matatizo wengi mbinguni, watakuwepo wakina Majuto wengi mbinguni, na pia watakuwepo wakina Masumbuko wengi mbinguni.
Kwa hiyo baada ya kuokoka, tafsiri ya jina lako isikusumbue sana. Kama umependa kulibadilisha kwa mapenzi yako mwenyewe (kwamba hupendi kuitwa hilo jina katikati ya jamii yako), ni sawa, hutendi dhambi. Na Kama Bwana amekuongoza kubadilisha jina lako, pia ni sawa, fanya hivyo.

Lakini kama Bwana hajakuongoza wala usiwe na hofu, wala usitishwe na elimu zilizozagaa kwamba utapata mikosi kwa jina hilo, au jina hilo ni kikwazo kwako na mafanikio yako.
Kuwa tu kama Simoni Mkananayo mwanafunzi wa Yesu, ambaye jina lake lilibakia kuwa lile lile, lakini bado aliendelea kuwa mwanafunzi wa Yesu. Japokuwa mwenzake alibadilishwa na kuwa Petro, yeye aliendelea kuwa vile vile Simoni. Kwa sababu Mungu hatembei na wewe kwa sababu ya tafsiri bora ya jina lako, bali kwa sababu ya uaminifu wako kwake katika kuyafanya mapenzi yake.

Kama vile asivyobagua rangi, vivyo hivyo Mungu habagui watu kutokana na tafsiri za majina yao.

Katika Biblia kuna mtu anaitwa Tabitha au Dorkasi, tafisiri ya jina hilo ni “paa” (Matendo 9:36). “Paa” kwa lugha inayoeleweka ni “mnyama swala”. Lakini pamoja na jina lake hilo lenye tafsiri isiyo na maana, tunasoma Tabitha alimpendeza Mungu sana:
Matendo 9:36: “Na mwanafunzi mmoja alikuwako Yafa, jina lake Tabitha, tafsiri yake ni Dorkasi (yaani paa); mwanamke huyu alikuwa amejaa matendo mema na sadaka alizozitoa”.

Kadhalika, katika biblia kuna mtu aliyeitwa Yabesi (1Nyakati 4:9-10). Huyu alipewa jina lenye tafsiri mbaya ya HUZUNI, kwa sababu mama yake alimzaa akiwa na huzuni. Lakini yeye alimpendeza Mungu sana.

Ipo mifano mingine mingi kwenye biblia. Lakini kwa hiyo michache itoshe tu kusema kwamba, kama ulikuwa na hofu na tafsiri ya jina lako, badilisha mtazamo. Anza kuwa na hofu na mwenendo wa maisha yako katika hatima ya maisha yako, kuliko ya tafsiri ya jina lako.

Ufunuo 20:12: “Nikawaona wafu, wakubwa kwa wadogo, wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi; na vitabu vikafunguliwa; na kitabu kingine kikafunguliwa, ambacho ni cha uzima; na hao wafu wakahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawa sawa na matendo yao”.

Ya kuzingatia katika vile vitabu, siyo uzuri wa majina, wala tafsiri zake, ni majina. Kinachozingatiwa zaidi ni matendo ya kila mtu/jina, yaliyofanyika duniani.

Hivyo utazame mwenendo wako, je umesimama katika imani sawa sawa?

Je matendo yako yanampendeza Mungu? Kama bado, rekebisha mapema kabla hujafikia mwisho wa siku za kuishi duniani.

Anza kuwa na hofu na mwenendo wa maisha yako katika hatima ya maisha yako, kuliko ya tafsiri ya jina lako.
Kama ulikuwa na hofu na tafsiri ya jina lako, badilisha mtazamo. Hakuna ulazima wa kubadilisha jina. Kubadilisha jina ni hiari ya mtu mwenyewe, siyo takwa la kiimani baada ya kuokoka.
 

Similar threads

Back
Top