Advertise here

Simulizi; Oscar Kambona alivyokutana na Mwalimu Nyerere

Kasomi

JT Founder
Na Peter Mwaihola
1762686630804.jpg

Ilizaliwa Tanganyika, ikajengwa jamhuri ikazaa Tanzania.

Tanzania kama Taifa lililoasisiwa na Vijana makini wenye, busara, utukutu wa kimawazo na uchu wa mabadiliko.

Tanzania ya akina Julius Nyerere, Mfalme Kawawa, Bibi Titi Mohamed, Eli Anangisye Mwalulesa na wengine wengii walioonyesha mchango wa hali na mali katika kulijenga taifa lao.

Oscar Kambona hakuachwa mbali kwenye mbio hizo za ujenzi wa taifa mama Tanzania.
Kambona ni mmoja kati ya vijana walio andika historia ya taifa hili kabla na baada ya uhuru.
Wakati wake aligeuza ubingo wake akifikiri ili kuleta ladha tofauti ya mawazo yenye tija kwa taifa lake pendwa.

Kambona Alizaliwa mnamo Agosti 13, 1928 katika kijiji kidogo cha kwambe kilichopo katika fukwe za ziwa nyasa karibu na Mbamba bay wilaya ya Nyasa.
Alikuwa ni mtoto wa kiume wa bwana David Kambona na Bi Miriam Kambona, baba yake alikuwa ni miongoni mwa waafrika wa mwanzo kupewa cheo cha uchungaji katika kanisa la kianglikana Tanganyika.
Oscar Kambona alipata elimu yake ya msingi chini ya mti wa muembe ambao hadi sasa ungali umesimama huko kijijini kwao alisomeshwa na wazazi wake pamoja na mjomba ambae nae alikuwa mwalimu.
Baadae alijiunga na shule ya kati ya mtakatifu Barnabas liuli (St. Barnabas Middle school) ambayo haikua mbali sana kutoka kijijini kwao.

Baada ya kumaliza masomo yake ya katika shule hizo kambona alibahatika kulipiwa ada na askofu wa kanisa la kianglikana Tanganyika kwani baba yake hakuwa na uwezo wa kumudu kuendelea kulipa ada ambayo ilikuwa ni takribani paundi 30 za kiingereza kwa mwaka. Inasemekana Kambona alimshawishi askofu huyo kutokana na uwezo wake mkubwa wa kusoma sara ya baba mtakatifu kwa lugha ya kiingereza.

Hii ikawa nyota nyingine njema kwa kambona kwani baada ya hapo alichaguliwa kujiunga na shule ya wavulana ya Tabora ambapo kwa mara ya kwanza alikutana na na Julius Nyerere ambae alikua tayari amefundisha shule ya mtakatifu maria ya mjini Dodoma.
Kambona alikuwa ni kijana mwenye ushawishi na umaarufu mkubwa baada ya mwalimu Nyerere yeye alifuata. Mawazo yake juu ya ukombozi yaliamfanya akubalike na kuteuliwa kuwa katibu mkuu wa TANU huku mwalimu Nyerere akiwa mwenyekiti.
Alishirikiana kwa ukaribu sana na watanganyika wengine kupigania uhuru mnamo mwaka 1961 Tanganyika ilipata uhuru kutoka kwa mwingereza.

Baada ya uhuru Kambona alibaki kuwa na ushawishi mkubwa hata baada ya muungano ambao ulizaa Tanzania na ikaaminika kuwa angekua Rais baada ya mwalimu Nyerere kustaafu au kung’atuka madarakani kwa sababu yoyote ile.

Uwezo wake katika kuongoza ulithibitika pale alipokuwa waziri wa ulinzi alipo watuliza wanajeshi ambao walifura wakitaka kuipindua serikali mwaka 1964 ambapo Rais Nyerere na makamu wake Rashidi kawawa walipelekwa mafichoni sehemu salama kutokana wanajeshi kutaka kuwadhuru.

"Asante Sana, asante ndugu yangu" hii ndiyo ilikuwa kauli pekee ya Rais Nyerere baada ya upepo huo wa jaribio la mapinduzi kupita alijitokeza hadharani kumshukuru kambona kwa kazi kubwa aliyoifanya kuwatuliza wanajeshi.

Viongozi wawili hawa walianza kutofautiana miaka michache baadae mgawanyiko wa kwanza ulianza baada ya jaribio la mapinduzi ya 1964 na mgawanyiko wa pili ulikuwa mwaka 1965 Tanzania ilipo ingia rasmi kwenye mfumo wa chama kimoja.

Kama mmoja wapo wa baraza la mawaziri Oscar alipinga mabadiliko hayo akidai kuwa hakukua na mikakati wala mwongozo kwa serikali kikatiba kutawaliwa na chama kimoja huku hofu yake kubwa ikiwa katiba ilikuwa haina ulinzi kama nchi ama serikali itageuka kuwa ya kidikteta.

Mwaka 1967 baada ya azimio la arusha lililo adhimia ujamaa na kujitegemea, kambona alikuwa haamini katika ujamaa hivyo alipingana na mfumo huu akiitaka serikali kuanzisha sehemu chache za matazamio kama mfumo huu ungekidhi maendeleo kitaifa.

Utofauti mkubwa wa Rais Nyerere na Kambona ulikuwa kwenye masuala ya kisera ambapo kambona alikuwa sio muumini wa sera ya ujamaa na kujitegemea ambayo Nyerere alikuwa akiipigia chapuo.

Kuna msemo wa kiswahili usemao "Fahari wawili hawakai zizi moja" mnamo mwezi Julai 1967 Kambona aliondoka nchini akiambatana na mke wake pamoja na watoto wake kuelekea London nchini uingereza kuondoka kwake kuliripotiwa na vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo radio, magazeti na runinga.
“Mwacheni aende” hiyo ndio sauti kuu iliyotoka katika kinywa cha mwalimu nyerere aliposikia kuondoka kwake, pia alisisitiza kua Kambona aliondoka na kiasi kikubwa cha pesa ambacho hakikuendana na mshahara wake "je alipata wapi mapesa yote yale" Nyerere alihoji Kwani kulikua na tetesi kua alijitajirisha alipokua ofisini kupitia pesa za harakati za ukombozi wa bara la afrika chini ya umoja wa afrika (OAU) Ambapo yeye alikua mwenyekiti wa kamati hiyo ya ukombozi kusini mwa Afrika.

Nae kambona hakutaka kushindwa mara moja alijibu tuhuma hizo mbele ya umma wa wana habari huko ughaibuni akisema “sina hatia yoyote juu ya hili iwapo kuna mwenye ukweli basi anifanyie uchunguzi na anianike hadharani”.

Muda mfupi mwaka uliofuata wa 1969 kambona alitangaza kuwa atafanya mapinduzi mnamo mwezi wa oktoba lakini bado mpango wake ukakwama kwani wahisani wake wote walitiwa nguvuni na kambona alishitakiwa kwa uhaini licha ya kuwa ughaibuni na hukumu ikasomwa mahakamani.
Wakati wa hukumu mmoja wa washirika wake 'John Chifupa' aliulizwa je ulimaanisha nini uliposema unataka kummaliza Nyerere Chifupa akakana akisema “la hasha hakimu mimi sikumaanisha kummaliza Nyerere kimwili bali nilimaanisha nataka kummaliza kisiasa”
Baada ya kesi hiyo kuunguruma miaka kadhaa kambona aliendelea kuwa mwiba kwa serikali ya mwalimu Nyerere akiwa huko ughaibuni mpaka pale Nyerere alipo ng'atuka madarakni.

Ilikua mwaka 1992 baada ya Tanzania kurejesha mfumo wa vyama vingi nae Kambona akaamua kurejea nyumbani na kujiunga na chama cha siasa TADEA baada ya kukaa uhamishoni kwa muda mrefu zaidi ya miaka 25.
licha ya historia yake nzuri ya kuwa mstari wa mbele katika kupigania uhuru miaka ya 1960 kambona alinyimwa nafasi ya kugombea uongozi katika chaguzi zote za miaka ya 90 ikidaiwa kuwa si mtanzania bali Mmalawi,
wengine walisikika wakisema ni raia wa Msumbiji, Kambona alijibu mapigo kwa kumwambia Nyerere nae si mtanzania bali Mnyarwanda.

Mnamo mwezi julai 1997 huko London nchini Uingereza Oscar Kambona aliutoka umma wa watanzania baada ya kuugua kwa muda, Kambona amebaki katika historia ya vijana wa wakati ule akijumuishwa na Vijana wengine jasiri wa wakati huo kama Chifu Said Fundikira, na wengine wengi waliokuwa mstari wa mbele katika siasa na maendeleo ya Taifa.

© Peter Mwaihola
 
Back
Top