Advertise here

Kumuamini Yesu pekee inatosha au haitoshi?

Kumuamini Yesu pekee inatosha au haitoshi?

Swali: Je kuna haja ya kutafuta jambo lingine tena baada ya kumwamini YESU?


Katika kitabu cha Yohana 3:18 na 3:36, Neno la Mungu linasema: ".... amwaminiye mwana anao uzima wa milele, asiyemwamini hana uzima?

Jibu: Yapo maandiko katika biblia yanayokamilishwa na maandiko mengine. Yapo pia maandiko ambayo hayahitaji kukamilishwa na mengine kwani yanakuwa yamejitosheleza.

Lakini yapo ambayo yanaelezwa kwa ufupi, hivyo ni lazima yakamilishwe na maandiko yaliyo katika vifungu vingine.
Kwa mfano: andiko hilo la Yohana 3:18 na 36. Ni kweli maandiko yanatuonyesha kuwa “tukimwamini Bwana YESU hatutahukumiwa bali tutapata uzima wa milele”.
Yohana 3:18 “AMWAMINIYE YEYE HAHUKUMIWI; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu". 3:36 "Amwaminiye Mwana yuna uzima wa milele; asiyemwamini Mwana hataona uzima, bali ghadhabu ya Mungu inamkalia".

Lakini tukirejea Marko 16:16 tunaona kuna jambo lingine linaongezeka:
Marko 16:16 “Aaminiye na KUBATIZWA ATAOKOKA; asiyeamini, atahukumiwa”.
Hapa kinachoongezeka ni “UBATIZO”, kwamba mtu akiamini pasipo kubatizwa bado hataurithi uzima wa milele, (yaani ikiwa amesikia habari za ubatizo na hajataka kubatizwa).

Na ubatizo unaozungumziwa hapo siyo ule wa MAJI TU, bali ni pamoja na ule wa ROHO MTAKATIFU (Luka 3:16).

Ili tuzidi kuelewe vizuri lugha hii, hebu tafakari kauli hizi mbili. Ya kwanza: “Ukipanda maharage utavuna maharage”. Ya pili: “Ukipanda maharage na kuyamwagilia maji utavuna maharage”.
Je ni kauli ipi ni bora kuliko nyingine?

Ni wazi kuwa kauli zote zipo sahihi, isipokuwa ya pili imefafanua vizuri. Hivyo, inayofaa zaidi ni hiyo ya pili, kwa sababu ndiyo imekamilisha kauli ya kwanza.


Vivyo hivyo, Neno linasema katika Yohana 3:18, kuwa amwaminiye YESU hatahukumiwa, lakini Marko 16:16, inakamilisha vizuri zaidi kwamba, Amwaminiye YESU na kubatizwa, hatahukumiwa. Kwa hiyo ya pili ina uzito zaidi kwa sababu imeikamilisha ile ya kwanza.

Kwa nini imani peke yake haitoshi, bali ni lazima kubatizwa kwa maji na kwa Roho Mtakatifu?

Jibu ni kwa sababu hata mashetani yanaamini, lakini bado hayana wokovu.


Maandiko katika kitabu cha Yakobo 2, yanasema:
19 “Wewe waamini ya kuwa Mungu ni mmoja; watenda VEMA. MASHETANI NAO WAAMINI NA KUTETEMEKA. 20 Lakini wataka kujua, wewe mwanadamu usiye kitu, kwamba imani pasipo matendo haizai”.

KWA KIFUPI
IMANI YA KUMWAMINI BWANA YESU ni LAZIMA IENDE NA MATENDO.
Tendo la kwanza ni ubatizo wa maji, na la pili ni ubatizo wa Roho Mtakatifu.


Mtu anapomwamini YESU na kubatizwa kwa maji na kwa Roho anakuwa amekamilika, na kukidhi vigezo vya kuuona ufalme wa Mungu, kwani maana pia ya kuzaliwa mara ya pili ni kuzaliwa kwa maji na kwa ROHO.
Yohana 3:4-7 inasema:
4 “Nikodemo akamwambia, Awezaje mtu kuzaliwa, akiwa mzee? Aweza kuingia tumboni mwa mamaye mara ya pili akazaliwa? 5 Yesu akajibu, Amin, amin, nakuambia, MTU ASIPOZALIWA KWA MAJI NA KWA ROHO, HAWEZI KUUINGIA UFALME WA MUNGU.
6 KILICHOZALIWA KWA MWILI NI MWILI; NA KILICHOZALIWA KWA ROHO NI ROHO.

7 Usistaajabu kwa kuwa nilikuambia, Hamna budi kuzaliwa mara ya pili”.

Kwa hiyo, imani ya kumwamini Yesu peke yake haitoshi.
Ni lazima imani hiyo iende pamoja na matendo.
Matendo hayo ni pamoja na KUBATIZWA na kufanya matendo matakatifu yanayolingana na Neno la Mungu.
Kwa kufanya hivyo, imani kwa Yesu itakuwa imekamilika.
 

Similar threads

Back
Top