Advertise here

Yesu alimaanisha nini kwa kusema waache wafu wazike wafu wao

https://www.jamiiforums.com/
Yesu alimaanisha nini kwa kusema waache wafu wazike wafu wao

Tamko hilo lilitolewa na Yesu, kupitia kitabu cha Mathayo 8:21.


Ili kufahamu vizuri habari hii, twende kwenye historia ya Wayahudi/Waisraeli katika tamaduni zao kuhusu shughuli za mazishi.

Waisraeli walivyozika zamani siyo kama wanavyozika siku hizi. Siku hizi mtu akifa, wanamvisha sanda (katika baadhi ya tamaduni), kisha wanamfukia chini bila jeneza, na shughuli inakuwa imeisha. Lakini zamani, haikuwa hivyo katika tamaduni zao.

Makaburi yalikuwa siyo ya kuchimbwa chini futi 6 kama yanayotumika hivi sasa.
Yalikuwa yanachongwa kwenye mwamba, au pango lililotokea lenyewe asilia.
Na pango halikuwa la kuzikia mtu mmoja mmoja. Bali mapango yalikuwa ni ya familia.

Kulikuwa kuna kuzikwa kwa hatua ya kwanza, na kuzikwa kwa hatua ya pili.
Jambo hilo ni tofauti na tamaduni karibu zote tulizonazo leo.

Maziko hatua ya kwanza

Kwa mfano, imetokea mshirika wa familia amekufa, mwili wake ukishaoshwa na kuvishwa sanda, ulikuwa unapelekwa kwenye kaburi la familia. Wakifika huko, wanamweka sehemu yake maalum peke yake, ambayo itakuwa imechongwa ndani ya kaburi/pango hilo. Huko wanaoruhusiwa kuingia ni wanafamilia tu. Wakishamlaza, jambo linalofuata ni kulifunga kaburi kwa jiwe kubwa, kisha wanalisakafia kwa nje, kisha wanarudi nyumbani kuendelea na maombolezo.

Maombolezo hayo yalidumu kwa muda wa siku kadhaa ikiwa aliyefariki ni mtoto katika familia. Lakini kama aliyefariki ni mtu mzima (baba au mama), siku za kuomboleza ziliendelea kwa muda wa mwaka mzima.

Maziko hatua ya pili
Baada ya mwaka kupita, wanafamilia wote na ndugu wanakusanyika tena kwa ajili ya maziko hatua ya pili.

Hapa ndipo mifupa ya yule marehemu inatolewa pale alipolazwa mara ya kwanza, na kupelekwa sehemu nyingine, yenye mifupa ya wanafamilia wote waliokufa kabla yake. Kisha, mifupa yake inalazwa pamoja na ya kwao (familia). Kufikia hapo, ndipo habari ya mazishi inakuwa imeisha rasmi.

Kutokana na mchakato huo wenye hatua mbili za maziko, maziko yote yalichukuwa mwaka mzima kukamilika. Ni katika hatua ya pili ya maziko ya KUKUSANYA mifupa na kuipeleka sehemu ya familia, ndipo unasikia pale biblia inaposema "akafa, AKAKUSANYWA pamoja na watu wake”.

Sasa turudi kwenye swali, kwa nini Bwana alimwambia yule mtu vile (Mathayo 8:21).

Hebu tusome kitabu cha Mathayo 8:21 "Mwingine katika wanafunzi wake akamwambia, Bwana, nipe ruhusa kwanza, niende nikamzike baba yangu. 22 Lakini Yesu akamwambia, Nifuate; waache wafu wazike wafu wao".

Tumeona kuwa jambo la kumzika mtu mzima/baba, halikuwa jambo jepesi la kwenda na kurudi kuchukua siku mbili au tatu. Ni jambo linalochukua mwaka mzima. Ingekuwa ni jambo la kuchukua siku mbili au tatu na kurudi, pengine lisingekuwa jambo kubwa kwa Bwana kumwambia nenda urudi.

Lakini, tuone Yesu aliposikia habari za msiba wa Lazaro pamoja na umbali wote ule, na hatari zote zile za kutaka kuuawa, lakini alifunga safari kwenda kumponya (Yohana 11:3-11).

Ila, utaona huyu mtu alikuwa anajaribu kutafuta njia za kuikwepa kazi ya Kristo. Alikuwa anakimbia majukumu. Kwa kujua hivyo, Yeu akamwambia ukweli.

Ni muhimu kufahamu kuwa ili uwe mwanafunzi wa Yesu, ipo gharama ya kuingia. Yeye mwenyewe alisema, apendaye baba au mama kuliko mimi, hanistahili (Mathayo 10:37-39).

Ni muhimu pia, kutambua kuwa pale Mungu anapokuambia, sasa ni wakati wa wewe kunitumikia, usiwe ni wakati wa wewe kusema ngoja kwanza nikamalizie kufanya biashara zangu, msimu huu ukiisha, nitakutumikia. Mungu hataki udhuru. Na ndiyo maana akamwambia yule mtu "waache wafu wawazike wafu wao".

Hii inamaanisha kuwa mtu yeyote aliye mbali na Kristo, ni mfu tayari katika roho, japo atakuwa anatembea kimwili. Lakini mauti ipo ndani yake, na siku akifa, wafu wenzake ambao bado hawajafa ndio watakaokwenda kumzika. Mauti inaanzia tukiwa bado tunapumua.

Kadhalika, wokovu unaanza tukiwa bado tunapumua hapa hapa duniani. Ndiyo maana hatuokoki tukishafika kule. Kule ni hitimisho la wokovu wetu.

Hivyo basi, sisi tunaonywa kuwa tusitoe udhuru kwa vitu tuvipendavyo pale Yesu anapotuchagua tumfuate. Bwana akikuita umtumikie, na amekuambia acha kitu fulani, usianze kutazama ni jinsi gani utawaachia wengine hiyo fursa. Wewe waachie wanaokifanya hicho kitu waendelee kukifanya, wewe nenda kumtumikia Mungu.

Ikiwa leo hii amekuambia, acha biashara haramu nifuate, usianze kumwambia Mungu ngoja kwanza nimalizie kuuza hizi zilizopo, kisha nitakufuata. Kusema hivyo ni sawa na kusema kuwa wewe ni mfu kiroho. Mungu hapendi kuwekwa wa mwisho.

Na ndiyo maana Yesu akawaambia wanafunzi wake: ‘’Mtu aliyetia mkono wake kulima, kisha akaangalia nyuma, hafai kwa ufalme wa Mungu’’ (Luka 9:62).

Ukristo una gharama. Ni kujikana na kupiga gharama kweli kweli.

Hivyo, katika Mathayo Mathayo 8:21, Bwana aliposema “waache wafu wazike wafu wao", alimaanisha kuwa mtu yeyote aliye mbali na Kristo, ni mfu tayari katika roho, japo atakuwa anatembea. Lakini mauti ipo ndani yake, na siku akifa, wafu wenzake ambao bado hawajafa ndio watakaokwenda kumzika. Mauti inaanzia tukingali tunapumua.

Yesu alisema hivyo, baada ya kuona yule mtu aliyekuwa anamhitaji kufanya kazi ya Mungu, akitoa udhuru/visingizio, ili asifanye kazi hiyo. Yaani, alikataa hiyo kazi ya Mungu. Hii ilimaanisha kuwa TAYARI ALIKUWA MFU ROHONI MWAKE.

Pili, alisema hivyo KWA KUTAMBUA KUWA MAZIKO YA WAKATI ULE YALIKUWA YANACHUKUWA MWAKA MZIMA. KWA MUDA HUO, HAIWEZEKANI KUMSUBIRI MTU AMBAYE ULITAKA AFANYE KAZI YA MUNGU. Ni Dhahiri kuwa mtu aliyetoa udhuru wa kwenda kuzika kwanza, alikuwa hana nia ya kufanya kazi aliyoitiwa. Hivyo, jibu lake lilistahili kuwa “waache wafu wazike wafu wao".
 

Similar threads

Back
Top