Kasomi
JT Founder
Mwanaume mmoja aitwaye Gal Gony Gatluak, mhitimu wa Shahada ya Uhasibu na Fedha, huko Sudan Kusini, amejikuta akiingia kwenye biashara ya uuzaji wa mkaa jijini Juba baada ya kutuma maombi ya kazi 47 bila mafanikio.
Gony, mwenye umri wa miaka 38, anasema licha ya kuwa na uzoefu wa kazi katika sekta ya misaada ya kimataifa, ofisi za serikali na nafasi za uongozi, bado hakufanikiwa kupata ajira nyingine baada ya mkataba wake wa mwisho kumalizika.
“Nilipoona maisha yanakuwa magumu na familia inahitaji huduma, nikaamua kuanza kuuza mkaa. Nimetuma maombi ya kazi zaidi ya 47 lakini sijapata wala kuitwa kwenye usaili. Ndio maana nikaamua nisikae bila kazi,” amesema Gony katika mahojiano maalum na "The Radio Community".
Kwa sasa, Gony anaendesha biashara yake iitwayo "Nyaruach Charcoal Business" kando ya Barabara ya Suk Harnab, akihudumia wateja wake kila siku bila kujali jua wala mvua.
Hatua yake ya kujiajiri imeibua mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii, huku wengi wakimtaja kuwa ni mfano wa kuigwa kwa vijana waliomaliza vyuo lakini wanakaa wakisubiri ajira za ofisini zisizo na uhakika.