Kasomi
JT Founder
Vyombo mbalimbali vya Habari Nchini Zambia vimeripoti kwamba Mahakama Kuu ya Nchi hiyo imewahukumu kifungo cha miaka miwili jela Wanaume wawili ( Leonard Phiri Raia wa Zambia na Jasten Mabulesse Candunde Raia wa Msumbiji) kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kosa la kujaribu kumloga Rais wa Zambia Haikande Hichilema kwa lengo la kumuua.
Wanaume hao wawili walitiwa hatiani chini ya sheria ya Uchawi ambapo wote walikamatwa tangu December 2024 wakiwa na vifaa vya kienyeji, kinyonga akiwa hai pamoja na vifaa vingine vya kichawi Hakimu Fine Mayambu, amesema Washtakiwa hawakuwa maadui wa Rais pekee bali pia Maadui wa Wananchi wote wa Zambia.
Kesi hiyo imekuwa ikifuatiliwa kwa karibu zaidi kutokana na kwamba ndio mara ya kwanza Nchini humo Mtu kushitakiwa kwa jaribio la kumloga Rais ambapo hati za mashtaka zimeonesha kuwa wawili hao walipewa kazi hiyo na Mbunge wa zamani wa Zambia.’
Ingawa wawili hao wamejitetea kwamba wao ni Waganga wa jadi, Mahakama iliwatia hatiani kwa makosa mawili chini ya sheria ya ulozi ambapo katika maelezo yake, Hakimu alifafanua kuwa Washitakiwa walikiri kumiliki dawa hizo na Phiri akaeleza kwamba mkia wa kinyonga ukidungwa na kutumika kwenye matambiko, unaweza kusababisha kifo ndani ya siku tano.