Naingiwa na uvivu kila nikitaka kusali

Naingiwa na uvivu kila nikitaka kusali

Kwa nini kila nikitaka kusali naingiwa na uvivu. Au nikitaka kusoma Neno ninapatwa na usingizi. Je, hizi ni nguvu za giza zinazisonga au ni nini?

Kwa mtu yeyote aliyeokoka, mbele yake wapo maadui wawili wakubwa.

Adui wa kwanza ni SHETANI. Adui wa pili ni MWILI WAKE MWENYEWE.

Adui wa kwanza: SHETANI

Adui wa kwanza ni shetani (Luka 22:31-32)
Shetani anachofanya ni kuhakikisha kuwa unakaa mbali na Mungu. Atafanya hivyo kwa kuhakikisha analeta kila namna ya presha za nje ili tu kukufanya uchukie maombi au ukose muda wa kusoma Neno la Mungu kwa ujumla. Anaweza kutumia ndugu, au mke au mume, kukukataza kusali, anaweza kunyanyua mazingira yo yote, ili kukufanya ukose muda kwenda kwenye maombi, au kusikiliza Neno la Mungu.
Kwa mfano, muda ambao ungepaswa uwe unasali, shetani anakuletea vipindi vya tamthilia nzuri kwenye televisheni, anakuletea magrupu ya kuchati, anakuletea sherehe za kuhudhuria, kazi fulani ya kufanya, nk.

Na kama mtu usipokuwa na msimamo katika imani yako, kuhakikisha kuwa Mungu anapewa nafasi ya kwanza, basi utachukuliwa na ulimwengu na kujikuta umerudi nyuma. Baadaye, ndiyo unakuja kushtuka ukiangalia mara ya mwisho kuomba ilikuwa ni miezi miwili iliyopita, mara ya mwisho kusoma biblia ni miezi mitatu iliyopita. Na ukijaribu kufanya tena hivyo, huwezi. Hali kama hiyo ikikukuta, basi ujue shetani amekuweza.

Adui wa pili: MWILI WAKO MWENYEWE
Adui wa pili ni mwili wako mwenyewe (Wagalatia 5:17, 19)
Adui wa pili ni mwili. Tofauti na watu wengi wanavyofikiri, kwamba ukiwa kwenye ibada, halafu ukasinzia, basi huyo ni shetani aliyekufanya usinzie. Au ukiwa unasoma Neno nyumbani ukasinzia, basi huyo ni shetani aliyekufanya ulale.

Nataka nikuambie kuwa huyo siyo shetani, bali ni mwili wako mwenyewe. Ukishaokoka, shetani hana mamlaka na mwili wako.

Kwa wale ambao hawajaokoka, labda shetani ndiye anaweza kuwaletea nguvu nyingine za mapepo kwenye miili yao ili wasimkaribie Mungu, lakini kwa mtu aliyeokoka, shetani hawezi kufanya hivyo.

Yesu alipowachukua wanafunzi wake watatu na kwenda kusali nao saa chache kabla ya kwenda kuteswa, alirudi na kuwakuta wamelala. Akawaamsha wasali. Akaenda kusali, akarudi tena, akakuta wamelala. Lakini Yesu hakukimbilia kuwaambia mna mapepo ndani yenu, kemeeni hizo roho, hapana.

Alijua tatizo ni nini, ndipo akawaambia maneno haya, katika kitabu cha Marko 14:
37 “Akaja akawakuta wamelala usingizi, akamwambia Petro, Je! Simoni, umelala? Hukuweza kukesha saa moja?
38 Kesheni mwombe, msije mkaingia majaribuni, ROHO I RADHI ILA MWILI NI DHAIFU.
39 Akaenda zake tena, akaomba, akisema neno lilo hilo”.

Unaona? Aliwaambia Roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu. Mwili siku zote unashindana na roho (Warumi 8:6; Wagalatia 5:17). Mwili haupendi mambo ya rohoni. Wakati roho inasema nataka kusali, mwili unasema lala. Wakati unasema nataka nisome Neno la Mungu, mwili unakuambia umechoka sana pumzika, kesho utafanya hivyo. Matendo ya MWILI dhahiri ni uasherati, ufisadi, uchawi, uadui, mziki, ugomvi, wivu, hasira, fitina, nk (Wagalatia 5:19).

Hivyo, njia pekee ya kuushinda mwili wako ni kuulazimisha uitii nia ya Kristo. Usiubembeleze. Hakikisha ukitaka kusali unakaa mahali ambapo hapana vichocheo vya usingizi, hudhuria ibada za maombi, jumuika na watakatifu wengine katika kusali. Hiyo inasaidia sana. Biblia inasema "kamba ya nyuzi tatu haikatiki haraka" (Mhu 4:12).
Ukisali na mwenzako utapata motisha na nguvu ya kuzidi kusali kuliko unavyoweza kusali mwenyewe. Ukitaka kila siku kwenda mwenyewe kwa mwenyewe kuna mahali utakwama tu.

Vile vile, hakikisha unajijengea utaratibu wa kuongeza kiwango chako cha kusali kila siku. Kama uwezo wako ulikuwa ni dakika 15, kesho ongeza nyingine 5, kesho kutwa 5. Hivyo hivyo, hadi mwezi unapoisha unakuta uwezo wako wa kwenda masafa marefu umeongezeka, unaenda hata masaa kadhaa katika maombi bila kusimama. Na ukawa bado hujachoka, siku umesali nusu saa, unajiona hujasali kitu.

Aidha, ongeza bidii binafsi katika kujifunza Neno la Mungu kupitia biblia, kila siku. Hakikisha siku haipiti bila kusoma Neno. Isiwe kusoma mstari fulani na kwenda kulala, hapana. Bali ni kusoma na kulitafakari Neno, na kujifunza, kwa muda mrefu kwa jinsi uwezavyo. Kila jambo linahitaji bidii.
2Petro 1:10 “Kwa hiyo ndugu, jitahidini zaidi kufanya imara kuitwa kwenu na uteule wenu; maana mkitenda hayo hamtajikwaa kamwe”.

Kwa ujumla, mtu yeyote aliyeokoka, mbele yake wapo maadui wawili wakubwa. Adui wa kwanza ni shetani, na adui wa pili ni mwili wake.

Ili kumshinda shetani, fanya yafuatayo:
1. Kuwa na MSIMAMO KATIKA IMANI YAKO.
2. Hakikisha kuwa MUNGU ANAPEWA NAFASI YA KWANZA katika maisha yako.
Mungu hapendi kuwekwa mwisho.

Ili kuushinda mwili wako, fanya yafuatayo:
1. UULAZIMISHE mwili uitii nia ya Kristo.
2. USIUBEMBELEZE, hakikisha ukitaka kusali unakaa mahali ambapo hapana vichocheo vya usingizi, hudhuria ibada za maombi, jumuika na watakatifu wengine katika kusali.
3. Hakikisha unajijengea utaratibu wa KUONGEZA KIWANGO CHAKO CHA KUSALI KILA SIKU, kwa mfano kutoka mara moja hadi mara tatu kwa siku.
4. Ongeza bidii binafsi katika KUJIFUNZA NENO LA MUNGU kupitia biblia, kila siku.

Ukizingatia hayo, hutaona ugumu wowote katika kutimiza nguzo zote za imani, ikiwa ni pamoja na kusali. Ukitaka kusali hutaingiwa na uvivu katika kusali.
 
Back
Top