Madaktari wa Marekani waandike Historia KCMC

Kasomi

JT Founder
Screenshot_20250627-013229~2.png

Madaktari bingwa wa upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu kutoka taasisi ya Barrow Neurological Institute nchini Marekani, kwa kushirikiana na wataalamu wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC), wamefanikisha upasuaji kwa wagonjwa sita waliokuwa wakisumbuliwa na matatizo sugu ya uvimbe kwenye ubongo.

Huduma hiyo imetolewa katika kambi maalum ya upasuaji iliyofanyika kati ya Juni 23 hadi 27, 2025, ikiwa ni sehemu ya mpango wa kubadilishana ujuzi na kutoa matibabu ya kibingwa kwa wagonjwa waliokuwa wakihitaji msaada maalum wa kiafya.

Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu kutoka KCMC, Dkt. Happyness Rabiel, amesema kambi hiyo imelenga kuwafikia wagonjwa waliokuwa wakisubiri huduma kwa muda mrefu kutokana na changamoto za upatikanaji wa wataalamu wa eneo hilo.

“Tayari tumeweza kuwafanyia upasuaji wagonjwa sita na tunatarajia kufikia wagonjwa kumi katika kipindi hiki kifupi. Ushirikiano huu ni wa manufaa makubwa kwa wagonjwa wetu na kwa madaktari wetu wanaopata fursa ya kujifunza mbinu mpya,” amesema Dkt. Rabiel.

Dkt. Michael Lawton, mmoja wa madaktari bingwa waliotoka Barrow na ambaye pia ni mbobezi wa upasuaji wa mishipa midogo ya damu katika ubongo, ndiye aliyeongoza upasuaji kwa wagonjwa hao.

Amesema wagonjwa waliopasuliwa walikuwa na changamoto ngumu za kiafya, lakini mafanikio ya upasuaji huo yametokana na ushirikiano mzuri kati ya timu zote mbili.

“Tumeshughulikia kesi ngumu, lakini kwa kushirikiana na wenzetu wa KCMC, tumeweza kufanikisha matibabu na kuleta matumaini kwa wagonjwa na familia zao,” amesema Dkt. Lawton.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka KCMC, wagonjwa waliopasuliwa wanaendelea vizuri, huku wakihudumiwa na jopo la madaktari bingwa wa ndani na wenzao kutoka Marekani chini ya uangalizi wa karibu.

Kambi hii ni sehemu ya jitihada za KCMC katika kuboresha huduma za kibingwa na kuongeza uwezo wa ndani wa kutoa matibabu magumu bila wagonjwa kulazimika kwenda nje ya nchi.

Chanzo: Manara TV
 

Similar threads

Back
Top