Marekani: Meta Kulazimika Kuuza Instagram na WhatsApp

Kasomi

JT Founder
Kampuni ya teknolojia ya Meta, inayomilikiwa na bilionea Mark Zuckerberg, huenda ikalazimika kuuza Instagram na WhatsApp kufuatia kesi ya ukiritimba (antitrust) inayosikilizwa nchini Marekani. Meta, ambayo pia inamiliki Facebook, ilinunua Instagram mwaka 2012 na WhatsApp mwaka 2014.

Serikali ya Marekani sasa inadai kuwa ununuzi huo ulikuwa na nia ya kuondoa ushindani na kujenga ukiritimba katika sekta ya mitandao ya kijamii. Ingawa Tume ya Biashara ya Marekani (FTC) iliidhinisha manunuzi hayo wakati huo, imeendelea kufuatilia athari zake kwa ushindani wa soko. Ikiwa FTC itashinda kesi hiyo, Meta inaweza kulazimika kuuza Instagram na WhatsApp.

Wataalamu wanasema kuwa hatua hiyo itakuwa na athari kubwa katika taswira ya sekta ya mitandao ya kijamii. Mike Proulx, Mkurugenzi wa Utafiti katika kampuni ya uchambuzi wa teknolojia Forrester, amesema kesi hii, pamoja na hali ya sintofahamu inayoikabili TikTok, inaweza kuanzisha “mpangilio mpya wa dunia ya mitandao ya kijamii.”

“Matokeo ya kesi hii, yakichanganywa na hatma isiyoeleweka ya TikTok, yanatishia mwelekeo mzima wa soko la mitandao ya kijamii. Meta huenda isiwe tena kitovu cha nguvu katika sekta hiyo.”

Ameongeza kuwa hatujaona hali ya mabadiliko ya aina hii tangu enzi za awali za mitandao ya kijamii kati ya mwaka 2006 hadi 2011, na kwamba huenda tukashuhudia kuibuka kwa kizazi kipya cha mitandao mipya ya kijamii.

“Ingawa Facebook ndiyo msingi wa utawala wa Meta, inaweza kukumbwa na changamoto kubwa ya ushindani ikiwa itaachwa pekee. Instagram imekuwa ‘bima ya kijamii’ ya kampuni hiyo kwa muda mrefu. Bila Instagram na WhatsApp, Meta itakuwa nini hasa?”

Proulx ameonya kuwa Threads haiwezi kutegemewa kwa mapato makubwa, huku akiongeza kuwa ndoto ya metaverse ya Meta pia haipaswi kuwa tegemeo. Hata hivyo, amesifu maendeleo ya kampuni hiyo katika teknolojia ya miwani ya AI na kazi zake pana kwenye akili bandia (AI).

“Iwapo Meta itagawanywa, juhudi zake za AI zinaweza kuchukua nafasi ya mizizi yake ya kijamii.”

Kesi hiyo imeanza kusikilizwa jijini Washington DC na inatarajiwa kuchukua wiki kadhaa. Mwanzilishi wa Meta, Mark Zuckerberg, pamoja na aliyekuwa afisa mkuu wa uendeshaji Sheryl Sandberg wanatarajiwa kutoa ushahidi.
Meta si kampuni pekee ya teknolojia inayochunguzwa kwa tuhuma za ukiritimba. Kampuni ya Google pia inakabiliwa na uwezekano wa kulazimishwa kuuza kivinjari cha Chrome na kuvunja utawala wake katika soko la utafutaji mtandaoni. Mwaka jana, jaji aliamua kuwa Google inashikilia ukiritimba katika utafutaji mtandaoni, na Wizara ya Sheria ya Marekani ikaitaka mahakama kuamuru Google kuuza Chrome kama sehemu ya hatua za kumaliza utawala wake wa soko hilo.
 

Similar threads

Back
Top