Advertise here

Polisi Mbeya yathibitisha kifo cha Shairose Mabula, Mwanafunzi wa Mzumbe-Mbeya

Kasomi

JT Founder
1758297052700.jpg

Baada ya kusambaa taarifa za kifo cha mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Ndaki ya Mbeya, Kitivo cha Sheria, Shairose Mabula (21), ambaye aliripotiwa kutoweka na baadaye mwili wake kupatikana jijini Mbeya, Jeshi la Polisi mkoani humo limesema linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo la mauaji.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, SACP Benjamin Kuzaga, Septemba 14, mwaka huu, baba mzazi wa marehemu, Dk. Michael Mabula, alifika katika kituo cha Polisi Mbeya na kutoa taarifa ya kupotea kwa binti yake. Kufuatia taarifa hiyo, jalada la uchunguzi lilifunguliwa na kuanza jitihada za ufuatiliaji.

Ameeleza kuwa mnamo Septemba 16, 2025, majira ya saa 5:00 usiku, polisi walipokea taarifa ya ajali ya moto katika Mtaa wa Morovian, Kata ya Isyesye, Jijini Mbeya. Askari walipofika eneo la tukio walikuta kibanda kinateketea kwa moto, na baada ya uchunguzi wa awali, mwili wa mtu wa jinsia ya kike uligundulika ndani, ingawa haukuweza kutambulika mara moja.

“Mwili wa marehemu ulichukuliwa na kuhifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya na baada ya uchunguzi wa kitabibu pamoja na uthibitisho wa ndugu, ilibainika kuwa ni wa Shairose Mabula, mwanafunzi aliyekuwa anatafutwa,” amesema Kuzaga.

Ameongeza kuwa uchunguzi wa kina, ikiwemo wa kisayansi, unaendelea ili kubaini wahusika na kuwakamata wote waliopanga au kushiriki katika mauaji hayo.

Chanzo: Nipashe
 
Back
Top