Kasomi
JT Founder
Baada ya miaka mingi ya kusubiri na miezi kadhaa ya maandalizi, mtandao wa WhatsApp umeanza rasmi kuruhusu watumiaji wake kote ulimwenguni kutumia majina yao ya kipekee ya watumiaji @username kama ilivyo kwa Instagram, X na mitandao mingine.
Kwa muda mrefu, namba ya simu ndiyo imekuwa njia pekee ya kumtambua mtumiaji ndani ya WhatsApp. Hata hivyo, kuanzia sasa mambo yanaenda kubadilika. Ukishatengeneza na kuhifadhi jina lako (username), utaweza kuwasiliana na watu wapya, wafanyabiashara, au kujiunga na magenge ya soga (groups) bila kulazimika kuwapa namba yako ya simu ya kibinafsi.
Hili ni ongezeko kubwa la faragha, kwani jina la mtumiaji litatumika kama utambulisho wako wa mwanzo badala ya tarakimu za namba yako.
Utekelezaji wa kipengele hiki umeanza kwa awamu tangu leo. Ili kuona kama akaunti yako imeshapata nafasi hii, fuata hatua hizi rahisi:
-> Hakikisha umesasisha (update) programu yako ya WhatsApp kwenda toleo jipya la sasa hivi.
-> Fungua programu kisha nenda kwenye Settings (Mipangilio).
-> Bonyeza Account (Akaunti).
-> Hapo utaona sehemu mpya ya Username. Bonyeza na uandike jina unalolipenda kisha ulisajili.
Kumbuka: Kwa kuwa WhatsApp ina zaidi ya watumiaji bilioni tatu duniani, majina mengi yanaweza kufanana au kuchukuliwa haraka. Hiyo ndiyo sababu kampuni ya Meta imeamua kufungua fursa ya kuhifadhi mapema ili kila mtu apate jina analolitaka kabla halijachukuliwa na mtu mwingine. Ikiwa bado hujaiona sehemu hiyo, usiwe na wasiwasi WhatsApp itakutumia taarifa (in-app notification) pindi itakapofika rasmi nchini kwako.