Advertise here

Ofisi ya Rais-TAMISEMI inatoa fursa ya mwezi mmoja kwa wanafunzi waliohitimu Kidato cha Nne mwaka 2024 kubadili tahasusi au kozi

Kasomi

JT Founder
Serikali kupitia Ofisi ya Rais-TAMISEMI inatoa fursa ya mwezi mmoja kwa wanafunzi waliohitimu Kidato cha Nne mwaka 2024 kubadili tahasusi au kozi itakayomwandaa kuwa na utaalamu stahiki katika maisha yao ya baadaye, Utaratibu huo umeanza Machi 31 hadi Aprili 30 mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa Habari leo tarehe 02.04.2025 jijini Dodoma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa alisema hatua hiyo inatoa fursa kwa wanafunzi kubadilisha machaguo ya Tahasusi za Kidato cha Tano na Vyuo vya Kati na Elimu ya Ufundi kwenye mfumo wa kielektroniki wa uchaguzi wa wanafunzi watakaojiunga na Kidato cha Tano na Vyuo.

“Hatua hii ni maandalizi ya awali ya uchaguzi wa wanafunzi watakaojiunga Kidato cha Tano na Vyuo vya Serikali kwa mwaka 2025.”

Serikali imekuwa ikitoa fursa kwa wahitimu wa Kidato cha Nne kufanya mabadiliko ya machaguo ya Tahasusi (combination) na Kozi mbalimbali walizozichagua kupitia Fomu ya Uchaguzi (Selform.).

Fursa hii huwawezesha wanafunzi kurekebisha machaguo yao kulingana na ufaulu waliopata kwenye matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne yaliyotangazwa na Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA).

Mchengerwa alisema Serikali kupitia Ofisi ya Rais-TAMISEMI imekamilisha utaratibu wa awali wa kuingiza kwenye kanzidata taarifa zilizo kwenye fomu za uchaguzi za wanafunzi kama zilivyojazwa na wanafunzi wakiwa shuleni.

“Baada ya wanafunzi kufanya marekebisho yao, kazidata hiyo ndiyo itakayotumika kuwachagua na kuwapangia nafasi za Kidato cha Tano na Kozi mbalimbali katika Vyuo vya Kati na vya Elimu ya Ufundi kwa kuzingatia sifa za ufaulu na machaguo yao.”

“Ofisi ya Rais – TAMISEMI inatoa fursa kwa wahitimu wa elimu ya sekondari Kidato cha Nne, mwaka 2024 kubadili machaguo yao ili kutoa nafasi zaidi kwa mwanafunzi kusoma tahasusi au kozi itakayomwandaa kuwa na utaalamu stahiki katika maisha yake ya baadaye.”
 
Back
Top