Advertise here

Simulizi: GENERAL’S DAUGHTER

Simulizi

Member
Simulizi: GENERAL’S DAUGHTER (01)
Mtunzi: Kalmas Konzo
Simu: 0625 646265
Camp 26 ilikuwa ni kambi maalum ambayo ilikuwa imeandaliwa kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa kikosi maalum ambacho kilikuwa kimekusudiwa kuanzishwa na jeshi la ulinzi la Bantu. Kazi ya kikosi hiki itakuwa ni kutekeleza misheni mbalimbali za usalama wa Taifa pindi zitakapokuwa zimeandaliwa. Kikosi hiki kilipewa ina la THE 5 EAGLES’ SQUAD.
Askari mbalimbali wa jeshi walikusanywa kutoka katika vikosi mbalimbali vya jeshi nchi Bantu na kuletwa katika kambi hii. Lengo lilikuwa ni kupatiwa mafunzo yenye mitihani mizito sana. Kutoka katika askari jeshi hao walitakiwa askari watano tu ambao wangekuwa wamefuzu na kuunda kikosi cha THE 5 EAGLE’S SQUAD
Miongoni mwa askari jeshi waliokuwa wakitarajiwa kupata mafunzo katika kambi hii maalum, mimi nilikuwa ni mmoja wao.
Jina langu ni Wilson Julius. Mimi ni askari jeshi kutoka katika Jeshi la ulinzi kikosi namba mbili kilichopo jijini Kano. Mimi ni askari mahiri sana katika utendaji wangu wa kazi. Sifa hii ndiyo ilifanya niwe miongoni mwa wachaguliwa wa kupata mafunzo katika kambi ile maalum ya kijeshi ambayo ilikuwa imeanzsihwa.
Camp 26 ilikuwa ni kambi ambayo ilikuwa ikipatikana katikati ya nchi ya Bantu kilometa sabini kutoka mini. Eneo ambako ilikuwepo kambi hii lilikuwa ni eneo la misitu pasi na makazi ya watu. Hakukuwa na usafiri maalum wa kuweza kukufikisha huko.
Yalikuwa ni majira ya saa tisa za alasiri ndipo nilipowasili katika kambi hii. Nilikuwa nimechoka sana kwani nilikuwa nimetumia usafiri wa punda kwa sababu magari hayakuruhusiwa kuja katika eneo la kambi.
Kambi hii ilikuwa ni ya kuvutia sana. Ilikuwa na majengo mbalimbali ya ghorofa ambayo yalikuwa ya kisasa sana. Nadhani majengo haya baadhi ni ofisi, madarasa pamoja na mabweni. Kambi hii ilikuwa imeandaliwa kwa muda mrefu kwani ilikuwa na miundo mbinu yote muhimu. Inaonekana serikali ilikuwa imewekeza fedha za kutosha katika mradi huu.
Niliibeba mizigo yang una moja kwa moja niliekea mpaka getini mahali maalum kwa ajili ya mapokezi. Pale getini palikuwa na askari watatu ambao walikuwa na silaha nzito kabisa.
“Jambo afande! Naitwa Wilson Julius, mwanafunzi katika kambi hii!” niliongea nikitoa kitambulisho changu na kumkabidhi mmoja wa askari wale.
Askari yule hakujibu chochote zaidi ya kukipokea kitambulisho changu na kuanza kukikagua.
Alitumia kama dakika moja na nusu kukikagua kitambulisho kile. Baada ya hapo aliuinua uso wake na kunitazama akijaribu kulinganusha picha iliyokuwepo kwenye kitambulisho na sura yangu.
Nilishangaa ni kwa nini askari huyu alikuwa akichukua muda mrefu sana katika kukikagua kitambulisho. Lakini baadaye nilijipa jibu kwamba ile ilikuwa ni kazi yake na alikuwa akionyesha umakini katika kazi.
Baada ya kujiridhisha, aliinua simu na kisha akapiga. Sikuelewa alikuwa akipiga wapi na alikuwa akiongea nini kwani nilichosikia ni "Sawa" na kisha simu ikakatwa.
Baada ya kama dakika tano hivi nilipigwa na butwaa kubwa sana. Ndani ya uzio kutoka katika jengo mojawapo macho yangu yaliweza kumwona mwanamke mkoja akija pale getini.
Mwanamke huyu alikuwa mzuri sana. Alikuwa na kila sifa ya uzuri wa mwanamke ambayo wewe ulikuwa ukiifahamu. Alikuwa amejaaliwa kila kitu kuanzia uzuri wa sura, rangi mpaka umbile.
Katika maisha yangu sikuwa nimewahi kumwona mwanamke mzuri kama yule yule.
"Hivi hapa nipo kambi ya jeshi kweli?" nilijiuliza moyoni pasi kuwa na jibu.
"Kijana vipi?" askari mmoja aliniulshtua kwa kuniuliza mara baada ya kuona nimezama katika lindi la duwao huku macho yangu nikiwa nimeyatoa kuelekea kwa mrembo yule.
"Ah! Hapana afande!" nilijibu huku nikizuga kuonyesha kwamba nilikuwa katika hali ya kawaida.
Jambo jingine lililonishangaza kuliko yote ilikuwa ni pindi alipofika pale getini. Mwanamke yule mrembo katika sare yake ya jeshi iliyomkaa vema alikuwa amechafukwa na nyota za kutosha. Nilipochunguza zaidi niligundua kwamba alikuwa na cheo cha Major General.
Askari wote pale getini walipiga saluti za heshima kwa mkubwa wao. Nami niliungana nao kwa kuiangusha saluti moja matata ya kikakamavu.
"Pole kwa safari afande!" askari yule aliniambia kwa sauti nyororo na ya upole yenye kuweza kumtoa nyoka pangoni.
"Ahsante sana!" nilijibu huku nikiwa nimeduwaa.
Alinitazama kwa muda wa sekunde kadhaa mithili ya mtu aliyekuwa akinifananisha. Kitendo kile kilinifanya nijishtukie na kujihisi huenda labda nilikuwa na kasoro fulani.
"Nifuate!" askari yule mrembo aliongea na kuanza kuondoka.
Niliibeba mizigo yangu na kuanza kumfuata. Jambo ambalo lilinishangaza ni kwamba iweje askari mwenye cheo kikubwa kama yule ndo aje kunipokea! Nilibaki kuogelea katika bahari ya swali like pasi kuwa na jibu.
Safari ya kumfuata ikiendelea.
Jambo la kushangaza ni kwamba mwanamke yule alinichukua mpaka katika uwanja wa mazoezi. Sikujua alikuwa na lengo gani kwani kwa fikra zangu mimi nilidhani labda ningechukuliwa mpaka katika hosteli ambako ningeoga na baadaye ningepewa chakula.
Hakika ilibaki kuwa ajabu kwangu.
"Weka mizigo chini!" mwanamke yule aliongea kwa sauti yake ile ile ya upole yenye mvuto.
Niliweka mizigo chini na kusimama kwa ukakamavu mbele yake kwani askari yule alikuwa amenizidi cheo mbali sana.
"Unaitwa nani?" niliulizwa.
"Naitwa Wilson Julius afande!" nilijibu kwa ujasiri.
"Sasa hivi ni saa ngapi?" aliniuliza.
"Ni saa tisa alasiri afande!" nilijibu kwa ukakamavu macho yakiwa mbele.
"Muda wa mwisho kuripoti uliambiwa ni saa ngapi?" aliuliza tena.
Kwa swali lile hapo ndipo akili yangu ikaanza kunikaa sawa. Nikajua tayari mambo yalikuwa yamekwishaharibika.
"Saa sita mchana afande!" nilijibu.
"Sasa ni kwa nini umefika saa hizi? Mbaya zaidi leo ndiyo siku ya mwisho kuripoti. Au unafikiri hili ni jeshi la baba yako!" niliulizwa.
ENDELEA
 
Simulizi: GENERAL’S DAUGHTER (02)
Mtunzi: Kalmas Konzo
Simu: 0625 646265
Safari hii nilishindwa kuamini kama huyu alikuwa ni askari yule yule ambaye mara ya kwanza nilimwona ni kama malkia. Alikuwa amebadilika ghafla.
“Naomba radhi afande!”
Ilinibidi niwe mpole na kuomba radhi. Niliamini kama nisingefanya hivyo basi kulikuwa na uwezekano mkubwa sana wa mimi kuipoteza nafasi ile.
Kuipoteza nafasi ile pekee halikuwa jambo ambalo lingenitisha, ila kama ingetokea hivyo ningekwenda kujibu nini kwa wakubwa wangu ambao waliniamini na kulipendekeza jina langu kuwa miongoni mwa wanafunzi wa kambi hii ya kijeshi.
Hii ingenifanya nionekane mzembe ambapo ningepewa adhabu nzito sana ambayo ingepelekea kushushwa cheo hata kupelekea kufukuzwa kabisa jeshini. Sheria za kijeshi ni ngumu sana.
“Haya push up mara elfu moja!” askari yule aliongea.
“Khaaaa afande!” niliuliza kwa mshangao maana siakuamini kile ambacho nilikisikia.
“Vipi, hazikutoshi nikuongezee nyingine!” mwanamke yule aliuliza kama ni mtu ambaye hakuwa akijali.
Kwa binadamu wa kawaida adhabu ile ambayo alikuwa amenipa ilikuwa ni nzito sana.nikaamini kwamba askari huyu alikuwa na lengo la kunikomoa. Lakini sikufahamu nilikuwa nimemkosea nini kwani sikuwa nikifahamiana hapo awali. Nilihisi huenda alikuwa amekasirishwa huko alikokuwa ametoka na hasira zake akaamua kuzimalizia kwangu.
Baadaye nikakumbuka sheria mojawapo ya jeshi ni kwamba unapopewa amri na mkubwa wako unatakiwa kuitekeleza pasi kuhoji. Tofauti nah apo lingekuwa ni kosa kubwa sana. Utii ni kiapo kikubwa sana jeshini.
Basi nikalianza zoezi lile huku nikiwa na wasiwasi kama nitafanikiwa kuimaliza adhabu ile.
“Kunja ngumi!” afande yule aliongea.
“”Jamani afande, naomba unisamehe!” niliongea huku nikipiga magoti mikono nikiwa nimeikunja machozi pia yakiwa yakinilengalenga.
“Nadhani unazifahamu sheria za jeshi!” afande yule alinipa jibu ambalo lilinitosha.
Nikaamua kuitekeleza adhabu ile ila moyoni niliumia sana. Sikudhani kama afande yule anaweza kuwa mnyama kiasi kile. Hata kama atakuwa ameghadhabishwa huko, hakutakiwa kuja kumalizia hasira zake kwa watu wengine wasio na hatia. Nilihisi kama nimeanza kumchukua.
Nilikunja ngumi na kuanza kuitekeleza adhabu ile. ilikuwa ni adhabu nzito sana ambayo mwanaume mzima ilinitoa machozi.
Ndani ya dakika hamsini nikawa nimefanikiwa kuitekeleza adhabu ile. lakini hali yangu ilikuwa mbaya sana kwani mikono yangu ilikuwa imechubuka ikitoa damu. Pia nilikuwa hoi nimechoka hasa.
“Hongera, umefanikiwa kutekeleza adhabu yako ya kwanza. Sasa tunakuja katika adhabu ya pili!” afande yule aliongea.
Alinipa tairi la gari ndogo na kunitaka nivae shingoni. Baada yah apo alinitaka nianze kuruka kichura chura huku yeye akinifuta nyuma. Aliniambia kwamba nilitakiwa kuuzunguka uwanja ule mara mbili. Sikuamini kwa kweli.
Nilianza adhabu ile huku hali yangu ikizidi kuwa mbaya. Miguu iliniuma. Nilihisi kulemewa na adhabu ile. sikudhani kama nitaweza kutoboa. Nyuma yangu afande yule aliendelea kunihimiza kuendelea na zoezi lile.
Nilifanikiwa kumaliza mzunguko wa kwanza tu. Ile naanza mzunguko wa pili nilijikuta naanguka chini na kupoteza fahamu.
********
Nilizinduka majira ya usiku wa kama saa moja hivi. Ilichukua muda kidogo kwa macho kuzoea nuru ambayo ilisababishwa na taa za umeme. Mwili ulikuwa na maumivu na nilikuwa mchovu sana. Nilipojitazama mikono yangu ilikuwa imezungushiwa bandeji. Na wakati huo nilikuwa juu ya kitanda huku nikiwa nimefunikwa shuka jeupe.
Nilijiuliza nilikuwa wapi pale lakini jibu lilishindwa kwa haraka kwani netiweki ilikuwa inasachi taratibu sana. Baadaye pua zangu zikabaini harufu ya dawa mbalimbali. Hapo ndipo nikahisi kwamba huenda mahali pale palikuwa ni hospitali.
“Hapa niko wapi?” nilimwuliza mwanamke mmoja ambaye alikuwa pembeni yangu akirekebisha dripu.
Niliamini kwamba mwanamke yule alikuwa ni nesi kutokana na mavazi ambayo alikuwa amevaa.
“Hapa upo hospitali. Pole sana. Nakuona sasa umepata nafuu!” nesi yule alijibu.
“Ni nini kilinikuta?” nilimwuliza tena nesi yule.
Nesi yule hakutoa jibu la moja kwa moja. Nilimwona amesita kidogo na kisha akasema, “Ulizimia ulipokuwa mazoezini!”
“Mazoezini!” nilijikuta nimepayuka.
Mazoezi gani tena ambayo nilikuwa nafanya? Swali hili lilizunguka haraka haraka kichwani mwangu. Swali lile lilikuwa linahitaji majibu ya haraka sana ili kuzifanya fikra zangu ziweze kuondoa msongo ambao zilikuwa nao.
Baadaye ndiyo kumbukumbu ikaanza kuja taratibu. Nilikumbuka jinsi ambapo niliwasili Camp 26 na kupokelewa na walinzi ambao walinikabidhi kwa askari wa kike mwenye cheo cha Major General.
Nilikumbuka pia kwamba askari yule alinichukua mpaka katika kiwanja cha mazoezi ambako alianza kuniadhibu kwa kosa la kuchelewa kuwasili pale kambini. Baada ya adhabu ya muda mrefu hatimaye nilizirai.
Sasa ndiyo nikabaini kwamba kumbe pale nilikuwa nimelazwa katika hospitali ya jeshi ambayo ilikuwa ndani ya kambi ile.
Taratibu machozi yalianza kunitoka. Niliona kama hali yenyewe ilikuwa ndiyo vile, basi kambi ile ilikuwa si ya mchezo. Hii ilimaanisha kwamba ukileta uzembe unaweza kujikuta unapoteza maisha.
“Sasa naomba uamke ukae uweze kupata chakula!” nesi yule aliongea kwa sauti ya upendo.
Wakati ule alikuwa amekwishaandaa chakula na kukiweka katika kijikabati kilichokuwa pembeni ya kitanda changu. Alinisaidia kuniamsha na kukaa kitandani. Baada yah apo alinipa chakula nami nikaanza kula.
ENDELEA
 
Simulizi: GENERAL’S DAUGHTER (03)
Mtunzi: Kalmas Konzo
Simu: 0625 646265
Nilikula haraka na kwa pupa kwani njaa ambayo nilikuwa nayo ilikuwa ni ya kiwango cha juu sana. Nesi yule alinitazama na kutabasamu. Alielewa kwamba nilikuwa na njaa sana.
“Ahsante sana nesi!” niliongea nikimkabidhi nesi yule sahani.
“Vipi umeshiba? Au nikuongeze!” nesi yule aliongea akitabasamu.
“Inaonekana ulikuwa na njaa sana!” nesi yule aliongea akinikabidhi glasi ya maji ya kunywa.
“Ni kweli nesi. Njaa niliyokuwa nayo ilikuwa si ya nchi hii. Yaani hapa toka nile jana ndiyo sasa Napata chakula!” nilijibu huku nikiipokea glasi ile na kuyanywa maji yaliyokuwamo ndanimwe.
Nesi yule alibaki akicheka tu maana kauli niliyokuwa nimeitoa ilimvunja mbavu.
“Basi sasa ulale upumzike. Hali ikiendelea hivihivi, basi asubuhi tutakuruhusu!” nesi yule aliongea.
“Nashukuru sana nesi kwa huduma yako. Mungu akubariki!” nilijibu na kujilaza kitandani.
*********
Asubuhi ya siku iliyofuata niliruhusiwa kutoka pale hospitali kwa sababu hali yangu ilikuwa imetengemaa. Nilipata fursa ya kuungana na wenzangu takribani ya mia mbili ambao kwa pamoja tulikuwa tukiwania nafasi tano za kuunda kikosi maalum cha 5 Eagles’ Squad.
Saa moja kamili sote tulikusanyika mesini ambapo tulipata kifungua kinywa. Kilikuwa ni kifungua kinywa kizuri na kitamu sana.
Lakini mimi kwa wakati huo hamu yangu ilikuwa ni kumwona askari yule wa kike ambaye alinisulubu siku iliyopita. Nilitaka nimwone na kumkagua kwa nafasi maana bado nilikuwa nashindwa kuamini kwa uzuri aliokuwa nao na ukatili ambao alinifanyia kwamba anaweza kuwa ni yeye.
Pia kwa wakati ule nilikuwa nimepata umaarufu mkubwa sana pale kambini. Kimbembe ambacho kilinikuta siku ya jana na kupelekea kulazwa hospitali kilikuwa kimelipaisha jina langu.
Watu walikuwa wakinishangaa. Wengine waliniona goigoi hata kunitabiria kwamba ningeshindwa kutoboa mafunzo yale. Walishangaa kwamba inawezekanaje nikazimia kwa kupewa adhabu kidogo ya push up na kichura chura.
Wengine walinihurumia hata wakadiriki kunifuata na kunipa pole. Mimi nilishukuru na kuwahakikishia kwamba kwa wakati ule nilikuwa safi kabisa.
Saa tatu kamili tulikusanywa katika kiwanja cha kupigia kwata. Hapo tulipigishwa gwaride zito la takribani nusu saa. Gwaride lile lilikuwa na lengo la kuichangamsha miili yet una kuziweka sawa akili zetu.
Baada ya hapo waliingia maafisa mbalimbali ambao walikuwa nav yeo vya juu sana kijeshi. Maafisa wale walikuwa ndiyo waratibu na wakufunzi wa kambi ile.
Katika jopo lile, nilifanikiwa kumwona yule mwanamke mrembo ambaye alinishushia kimbembe siku ya jana. Nilishangaa kuona kwamba alikuwa ni mmoja wa wakufunzi.
Tukiwa bado tumesimama twisti, afisa mmoja mwenye cheo cha jenerali alisogea mpaka kwenye kipaza sauti na kuanza kuongea.
“Hamjambo vijana!” jenerali yule alitusabahi.
‘Hatujambo afande!” tulijibu kwa umoja na kwa ukakamavu.
“Naitwa jenerali Knowman Bisare. Mimi ndiye mkufunzi mkuu na mratibu wa mafunzo haya. Nawakaribisha sana vijana na mjisikie huru kabisa” alitulia kidogo na kumeza funda la mate.
“Mafunzo yenu yatafanyika kwa muda wa miezi sita. Katika miezi hiyo sita mtachijwa na hatimaye tutawapata vijana watano tunaowahitaji. Kwa muda huo wa miezi hiyo sita mtahudhuria mafunzi ambayo yamegawanywa katika ngazi sita. Kila ngazi itachukua mwezi mmoja. Ukihitimu ngazi moja basi utaenda katika ngazi nyingine”
“Watakaokuwa wanashindwa kwenye kila ngazi watabaki kuwa askari jeshi wa kawaida katika kambi hii. Hii ina maana kwamba hamtarudi katika kambi mlizotoka”
“Mbele yenu ni wakufunzi ambao mtakuwa nao katika mafunzo mbali mbali. Kila mmoja atajitambulisha pamoja na seksheni anayotoka!” jenerali Knowman Bisare aliongea.
Yule askari wa kike ambaye alinishushia varangati siku ya jana alisogelea kipaza sauti nna kuanza kujitambulisha.
“Naitwa Meja jenerali Cecy Knowman, mimi ndiye mkufunzi msaidizi wa kambi hii na pia nitakuwa nanyi katika seksheni ya mazoezi ya viungo pamoja na mapambano ya viungo vya mwili yaani Martial arts. Nahitaji ushirikiano!” mwanadada yule mrembo alimaliza.
Wakufunzi wale waliendelea kufanya utambulisho wa majina, vyeo pamoja na seksheni zao. Dakika kumi zilitosha kukamilisha utambulisho ule.
Mimi kwa wakati ule akili yangu ilikuwa imesimama kabisa. Kichwa nilianza kukiona kizito kutokana na mawazo ambayo yalikuwa yananiandama. Nikawa nahisi kama niko ndotoni vile.
“Inawezekanaje hii?” nilijiuliza moyoni.
Swali langu lilikuwa ni juu ya utambulisho wenye utata wa mwanamke yule mrembo meja jenerali. Nilijiuliza ni kwa nini jina lake la pili linafanana na la jenerali ambaye ndiye mkuu wa kambi ile? pili nilijiuliza ni kwa nini yeye amekuwa msaidizi wa mkuu wa kambi ukiachilia mbali sadifa ya majina yao. Nilibaki njia panda.
“Siku ya leo mtakuwa huru. Mtaitumia siku ya leo kufahamiana. Pia mtafanya maandalizi kwa ajili ya siku ya kesho ambayo ndiyo siku rasmi ya kuanza mafunzo. Nawatakia siku njema!” Brigedia Simon ambaye alikuwa ndiye inchaji aliongea.
Baada ya hapo tulitawanyika. Kila mmoja alienda katika shughuli zake.
Siku ile nilifanikiwa kupata marafiki watatu ambao walitokea kunielewa sana. Vijana hawa walikuwa ni Salim, Aboubakar pamoja na Anthony. Sote kwa pamoja tukatokea kuweka urafiki ambao ulikuwa imara sana.
Katika kambi ile kulikuwa na jamaa mmoja ambaye yeye alikuwa ni mbabe sana. Alikuwa na majivuno sana na kujiona kama yeye ndiye kila kitu. Hii ilitokana na kwamba yeye alikuwa akitokea katika familia iliyokuwa na ukwasi sana.
Ndani ya siku chache alizokuwa amekaa pale kambini alikuwa amejitengenezea kundi kubwa sana la watu ambao walikuwa wakimfuata na kumsujudu. Kwa kifupi alikuwa amejitengenezea nguvu kubwa sana pale kambini.
Yeyote ambaye alikuwa akienda kinyume na matakwa yake basi alipata adhabu kali sana ambayo ingemfanya ajute. Watu walianza kumwogopa sana.
Bwana yule alikuwa akiitwa Sajidu Bufa lakini watu wengi walipenda kumwita Jitu na hivyo ndivyo hata yeye alipenda aitwe.
Rafiki zangu wale walinipa habari za Jitu na kunitahadharisha kwamba nikae mbali naye kwani hakuwa mtu mzuri kabisa.
“Usijali Aboubakar, mimi na watu wakorofi niko tofauti nao kabisa. Hao siyo aina ya watu ambao mimi ninaweza kufungamana nao!” nilimjibu Aboubakar ambaye alikuwa akinitahadharisha.
Tuliendelea kufanya maongezi yetu tukiwa tumekaa juu ya nyasi laini ambazo zilikuwa zimeoteshwa kwenye kiunga cha maua mazuri.
Tukiwa tunaendelea na maongezi yetu, kwa mbali alipita Meja Jenerali Cecy. Mimi nilimwangalia mpaka anapotelea katika macho yangu.
“Vipi Wily, mbona wamwangalia kiasi hicho Meja jenerali?” Anthony aliniuliza.
“Mwanamke katili sana yule. Yaani mwonekano wake na roho yake vinatofautiana kabisa!” nilijibu.
“Ha ha ha haaaa! Pole sana rafiki yangu. Inaonekana wamchukia sana!” Salim aliongea.
“Yaani namchukia si kidogo. Unajua mpaka sasa sifahamu kosa hasa la kunipa adhabu ya kikatili kiasi kile ni lipi. Yaani kuchelewa tu kufika kambini ndiyo aniadhibu kutaka kunitoa uhai wangu! Halafu nilimweleza sababu ya mimi kuchelewa lakini hakutaka kunielewa!” niliongea kwa uchungu.
“Lakini inasemekana kwamba sheria za kambi hii ni ngumu sana tofauti na kambi ambazo tumewahi kuzipitia. Na hii ndiyo sababu ikaitwa kambi maalum!” Aboubakar aliongea.
“Hata kama, lakini si kwa unyama ule. Yule mwanamke lazima siku ile alikuwa amekasirishwa huko alikokuwa. Hivyo basi hasira zake zote akaamua kuja kuzimalizia kwangu!” nilijibu.
“Lakini mbona anaonekama kama mwanamke mwema sana!” Anthony aliongea.
“Kwa hiyo waona kama mimi ninaongopa kwa ninayoyaongea juu ya mwanamke yule! We subiri uingie kwenye kumi na nane zake ndiyo utayakumbuka maneno yangu. Usilewe na uzuri w asura yake!” nilimjibu Anthony.
“Oyaaaa! Hebu angalieni kule!” Salim aliongea akiyakatiza malumbano yetu.
Sote tuligeuza vichwa vyetu kutazama upande ambao tulikuwa tumeelekezwa. Macho yetu yaliweza kumwona Jitu akija upande wetu akiwa ameongozana na wapambe wake kama watano hivi.
“Ha ha ha haaaaa! Hebu tazameni hii ng’ombe. Yaani hii ndiyo ilipewa mazoezi mpaka ikazimia!” Jitu aliongea kwa ujivuni mara baana ya kutufikia mahali ambako tulikuwa tumeketi.
“Ha ha ha haaa!” wapambe wake nao walicheka kumuunga mkono.
“Ha ha ha haaaa! Kipo goigoi sana hiki. Au kinaumwa utapiamlo!” Jitu alizidi kuongea kwa dharau na kebehi.
“Kitakuwa kinaumwa UKIMWI! Ha ha ha haaaa!” mpambe wake mmoja aliongea.
Kauli ile ilimghadhabisha sana Salim. Alitaka kusimama na kwnda kumwashia moto kijana yule, lakini mimi nilimzuia kwa kumshika mkono na kumtaka aendelee kukaa.
“Unataka nini wewe dogo, unataka kupigana!” Jitu aliongea.
“Tunaomba mtuache, sisi hatuhitaji ugomvi hata kidogo!” niliongea nikimsihi Jitu.
“Wewe ni nani kwani hata utupangie cha kufanya. Sisi mikono yetu inawasha, ina hamu ya kutembeza kipigo. Halafu nina ham una wewe nikuvunje hata miguu!” Jitu aliongea kibabe huku akinisogelea.
Rafiki zangu walikwishajaa upepo na kutaka kusimama kuliamsha vagi, lakini mimi niliwazuia kwa kuwakonyeza. Niliwaambia kwamba ule haukuwa wakati sahihi.
“Sawa, sisi tumekubali kwamba wewe ni mbabe hivyo hatuhitaji ugomvi!” nilijibu kwa upole.
“Utakubalije bila kupambana. Lazima tupambane aonekane mshindi nani!” Jitu alifoka.
“Mimi sikuwezi hata kidogo, mimi ni goigoi. Halafu pia mimi sipendi ugomvi kwani sicho kilichonileta hapa kambini!” nilijibu.
Mmemwona jinsi alivyo na kebehi. Ana kiburi sana huyu mbuzi. Sasa nakwambia, kaa mbali sana nami. Utaishi maisha magumu sana hapa kambini. Mimi huwa sipendi watu wenye kiburi!” Jitu aliendelea kufoka.
“Halafu unajiona wewe ndo mstaarabu sana. Unajiona kama ndo umeshashinda mafunzo au siyo. Sasa kwa taarifa yako unatakiwa kujua kwamba mimi nimekwishapita kwani baba yangu ni mtu mkubwa sana jeshini. Unapaswa kuniheshimu sana mbuzi wewe!” Jitu aliendelea kufoka.
“Sasa kwani nani ambaye amekudharau. Hayo yote unayoyasema ni sawa wala sisi hayatuhusu. Nadhani hapa kambini kila mtu alikuja kivyake. Naomba usitughasi uende zako kwa amani!” niliongea.
“Wewe inatakiwa nikutafutie muda ili nikufunze adabu. Guys, hebu twendeni. Tutamnyoosha tu huyu mbuzi!” Jitu alifoka.
Baada ya hapo yeye pamoja na kundi lake waliondoka huku wakiwa wamejaa ghadhabu kubwa sana. Waliona kama walikuwa wamedharaulika sana.
ENDELEA
 
Simulizi: GENERAL’S DAUGHTER 04
Mtunzi: Kalmas Konzo
Simu: 0625 646265
“Ungeacha tuwafunze adabu wapumbavu hawa!” Salim alifoka.
“Hapana Salim, ghadhabu siyo njia nzuri ya kupambana na adui yako. Maea zote kumbuka kutumia akili!” nilimtuliza Salim.
“Hebu ruachane na wajinga wale, tumjadili zaidi Meja jenerali!” niliongea nikibadili mada.
“Mh! Nawe humwachi tu MJ akapumua!” Anthony aliongea kwa utani.
“Hivi ninyi hajaona ajabu kwa Meja jenerali?” niliwauliza.
“Ajabu gani?” Aboubakar aliuliza.
“Kumbe ninyi hamko makini. Meja jenerali anaitwa Cecy Knowman wakati Jenerali anaitwa Knowman Bisare. Hivi hamwoni kama pana sadifa hapo?” niliwauliza nikifafanua.
Hapo ndipo rafiki zangu wale wakawa wamefunguka macho, masikio, pamoja na fikra zao. Sasa ndiyo wakaanza kuliwekea umakini jambo lile. Mwanzoni hawakuwa wakiniamini, waliona mimi nilikuwa simpendi Meja jenerali hivyo maneno yangu yalikuwa ni kwa lengo la kumchafua.
“Aiseee! Kweli bwana, yaani mimi sikuliwaza hilo kabisa!” Aboubakar aliongea.
“Haw ani lazima ndugu hawa!” Salim naye akaongezea.
“Tena yawezekana ni mt una binti yake. Halafu si waona jinsi ambavyo wamefanana. Aiseeee! Yaani tulikuwa gizani kabisa!” Anthony yeye ndiyo akakazia kabisa.
“Swali linakuja, wakawa katika kambi moja halafu wote wakawa nav yeo vikubwa kiasi hiki? Kwa mzee Knowman kuwa na cheo kikubwa hiyo haishangazi, ila kwa huyu bidada Cecy sasa. Bado binti mdogo sana. Anawezaje kuwa na cheo kikubwa namna hii?” niliuliza.
“Yule binti anaonekana ni jasiri sana na yuko makini sana katika mambo yake. Pia inaonekana ana uwezo mkubwa sana kijeshi!” Anthony alijibu.
“Ndiyo maana amekuwa katili kiasi kile!” niliongea.
“”Nadhani kwako ilikuwa ni bahati mbaya tu ukawa umeingia kwenye kumi na nane zake!” Aboubakar aliongea.
“Inawezekana, lakini mimi moyoni amenitoka kabisa!” nilijibu.
“Hebu tuachane na hayo, hivi suala la yule Jitu mnalichukuliaje? Mimi kwa upande wangu amenikera sana. Muda ule usingetuzuia tumtie adabu!” Anthony aliongea.
“Anthony, nafahamu ni kwa kiasi gani mlikereka. Hata mimi mwenyewe maneno na vitendo vyake vilinipa ghadhabu. Lakini kumbukeni kwamba hata siku moja huwezi kufanya jambo lenye fanaka ukiwa unaongozwa na ghadhabu. Pia vurugu haijengi, mar azote hubomoa. Vurugu huondoa nidhamu, vurugu huondoa utu pamoja na thamani ya mtu. Sidhani kama sisi tunapenda tuondokewe na hayo yote ambayo ni mambo ya msingi!” niliongea.
“Hapana!” walijibu kwa umoja.
“Basi, acha busara ituongoze. Tuiache hekima ichukue nafasi yake katika maisha yetu!” nilizidi kutema madini.
Rafiki zangu walinishangaa sana kwa maneno yangu. Walizidi kunipenda kutokana na busara na hekima zangu. Kila mmoja aliona fahari kwa mimi kuwa rafiki yake.
“Utakapoonyesha kupambana na mwehu, basi na wewe pia utaonekana mwehu!” nilimalizia.
“Umenena vema hakika!” Salim aliongea akionyesha maneno yangu yalikuwa yamemjenga sana.
******
Ulipofika wasaa wa kupata chakula, sote tulikusanyika katika bwalo la kulia chakula. Kama ilivyo kawaida kwa sisi marafiki tulikaa katika meza moja huku tukikifurahia chakula chetu. Na hivi ndivyo ilivyokuwa kwa wanajeshi wengine. Kila mmoja alikuwa katika kundi la marafiki zake ambao alikuwa amewachagua.
Wakati wote tukiendelea kupata chakula mle bwaloni, wapambe wa jitu pamoja na jitu mwenyewe walikuwa wakitutupia macho ya wizi. Walionekana kuna mpango wa siri ambao walikuwa wakiupanga juu yetu. Kila mara walikuwa hawaachi kunong’onezana huku wakitutazama kisirisiri.
Mimi nililitambua hilo. Nilijua kuna hatari kubwa sana ambayo ilikuwa ikitukabili. Hii ilimaanisha kwamba kuanzia wakati ule tulipaswa kuishi kwa tahadhari pale kambini.
“Ndugu zangu, kuanzia sasa, hakuna hata mmoja miongoni mwetu ambaye atapaswa kutembea peke yake. Kila mahali tuendako tutapaswa kuandamana!” niliongea nikiwajulisha wenzangu.
“Hilo mbona ni kawaida. Sisi ni marafiki hivyo muda mwingi tutakuwa tuko pamoja!” Aboubakar alijibu.
“Ni kweli kabisa!” Salim na Anthony nao wakamwunga mkono Aboubakar.
Rafiki zangu hawakuwa wameelewa ni likuwa nimemaanisha nini kwa kusema vile. Kauli yangu waliichukulia ki wepesi sana. Nilitamani niwaeleze hatari ambayo nilikuwa naiona lakini nilichelea kuwatia hofu mioyoni mwao.
Tuliendelea kula huku tukipiga stori za hapa na pale. Rafiki zangu walionekana ni watu wenye furaha sana. Furaha yao ilitokana na kunipata mimi kuwa rafiki yao ambaye waliamini kwamba nilikuwa na thamani kubwa sana katika maisha yao. Walinifanya kuwa rafiki mwema sana kwao.
Baadaye filimbi ilipulizwa kuashiria kwamba muda wa kula ulikuwa umekwisha. Si wajua jeshini kila kitu kinakwenda na muda. Sote tulisimama na kutoka mle bwaloni.
“Sasa tunaenda wapi?” niliwauliza wenzangu pindi tulipokuwa nje ya bwalo.
“Mi nadhani twende kule nyuma bustanini tukapunge upepo. Kuna kivuli kizuri pamoja na hewa safi!” Salim alishauri.
“Kweli kabisa, tena kwa shibe hii, eneo hilo litatufaa sana!” Aboubakar aliunga mkono na kutufanya sote tuangue kicheko.
Hatukuwa na namna zaidi ya kulitekeleza wazo za mwenzetu Salim kwa sababu lilikuwa ni wazo jema.
Tukiwa njiani kuelekea bustanini, tulipishana na Meja Jenerali Cecy. Sote tulipiga saluti kuonyesha heshima ambapo Cecy naye alijibu saluti yetu.
“Unaendeleaje?” Cecy aliniuliza.
“Kwa sasa sijambo afande!” nilijibu kwa ukakamavu lakini moyoni nikiwa na hofu mzzzzzzzaana muziki wa Cecy nilikuwa naufahamu.
Meja jenerali Cecy alinitazama usoni kwa sekunde kadhaa na baadaye alishuka chini. Sikufahamu ni nini ambacho alikuwa akikikagua mwilini mwangu. Wasiwasi ulizidi kunijaa moyoni kwani sikutaka kabisa nionekane na kasoro yoyote ambayo ingeniingiza tena katika kumi na nane za askari huyu katili.
Meja jenerali Cecy aliitambua hofu ambayo nilikuwa nayo moyoni mwangu. Aliachia tabasamu moja mwanana na kisha akaendelea na safari yake.
Kitendo kile kilinishangaza sana. Tabasamu la afande yule liligonga fikrani mwangu na kuacha athari kubwa sana. Cecy alikuwa ni askari mzuri sana kisura pamoja na kiumbile. Pia alikuwa ni askari nadhifu ambapo katu usingefanikiwa kukuta doa lolote katika sare n ahata mwili wake. Kwa kifupi alikuwa ni mwanamke ambaye alikuwa akijipenda kama mwanamke ukiachilia mbali uaskari wake.
“Hivi tabasamu lile lina maana gani kwangu? Huyu si ndiye ambaye siku ya jana alinipa adhabu ya kikatili ambayo ilipelekea mimi kupoteza fahamu! Sasa mbona leo ananiachia tabasamu utadhani hakuna kitu kibaya ambacho kilikuwa kimetokea siku ya jana” mawazo haya yalitembea haraka haraka kichwani mwangu.
ENDELEA
 
Simulizi: GENERAL’S DAUGHTER 05
Mtunzi: Kalmas Konzo
Simu: 0625 646265
Baadaye nikaona ngoja niachane na fikra kuhusu mwanamke yule. Nilihisi kama nikiendelea kumweka kichwani mwangu basi maisha yangu pale kambini yatakuwa magumu na ningeweza hata kufeli katika mafunzo yangu jambo ambalo sikulipenda hata kidogo.
“Vipi Willy, mbona umebaki umeduwaa kama umepigwa shoti ya umeme?” Anthony aliniuliza kitendo ambacho kilinifanya sasa nirudi katika akili yangu ya kawaida.
“Ah! Hapana! Hebu twendeni!” nilijibu nikiwahimiza wenzangu kuendelea na safari yetu.
Lakini kila mmoja alitambua kwamba kuna kitu ambacho kilikuwa kikizisumbua fikra zangu. Walijua kwamba kukutana na Meja jenerali Cecy kulikuwa kumekivuruga kichwa changu hasa ukuchukulia kwamba walikuwa wanafahamu kwamba nilikuwa simpendi na namchukia sana askari yule.
Hakuna hata mmoja ambaye aliniongelesha kwani walijua haikuwa vema kufanya hivyo. Waliamua kuniacha ili mawazo yanile kwa muda kwani waliamini kwamba hiyo ilikuwa ndiyo dawa ya kuyapunguza mawazo hayo.
Tulifika katika bustani hiyo ambapo kwangu mimi ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kufika. Wenzangu walikuwa ni wenyeji kwani walikuwa wamenitangulia kuripoti pale kambini kwa siku kadhaa hivyo walikuwa ni wenyeji wa mazingira.
Ilikuwa ni bustani nzuri sana ambayo ilikuwa imesheheni maua ya kila aina. Pia kulikuwa na miti mingi ya vivuli na miti mingine ya maua. Nyasi laini za kijani zilizokuwa zimekatwa vema zilibadili sura ya eneo lile na kulifanya lionekane la kijani. Wadudu mbalimbali wapendao maua kama nyuki na vipepeo walikuwa wakiruka ruka hapa na pale katika kukamilisha uchavushaji.
Hakika nililipenda sana eneo lile. Hewa safi iliyokuwepo eneo lile ilinifanya niburudike mpaka ndani ya moyo wangu.
“Wily, tuna wageni!” Salim aliongea na kunitoa katika burudabi ambayo nilikuwa nikiipata.
Sote tuligeuza vichwa vyetu na kutazama kule ambako Salim alikuwa ametuelekeza. Asalaleee! Hakuwa mwingine bali alikuwa ni Jitu akiwa ameongozana na kampani yake ya wwatu kama saba hivi.
Hapo nikajua sasa kulikuwa kumekucha. Nilimtazama Jitu ambaye alikuwa akija kifua mbele huku akitembea kibabe sana. Sikuwa na pupa, nilimtazama akijongea mpaka alipotufikia akiwa na wenzake.
“Haya wewe mbwa, nadhani muda sasa wa kukushikisha adabu umefika!” Jitu alifoka akiwa amesimama mkabala nami nyuma yake wakiwa wamesimama wapambe wake.
“Unajua mimi sifahamu ni nini hasa ambacho unakitaka kutoka kwetu. Sisi ni watu ambao hatupendi ugomvi. Hivyo nakushauri wachukue watu wako na muondoke hapa!” niliongea nikimtazama Jitu usoni.
“Unaonaaa! Yaani wewe hizo dharau zako ndilo jambo kubwa ambalo linanikasirisha mimi. Hakuna mtu yeyote ambaye anathubutu kunijibu mimi vile anavyotaka!” Jitu alifoka.
“Kwani wewe ni nani bwana! Hebu acha kuwatia hofu watu bwana. Kila mmoja ana haki ya kuishi apendavyo hapa!” niliendelea kufoka.
Kauli yangu ilizidi kumjaza upepo Jitu mpaka akakaribia kupasuka. Alikamata sare yang una kunikunja kisha akataka kunivutia kwake ili anibandike kichwa. Wakati wote huo mimi nilikuwa nausoma mchezo. Nilikuwa nataka nimwache afanye anavyotaka ila mimi ningemuwahi kwenye pointi muhimu na kufanya shambulizi.
“Jitu! Jituuu! Bosi kuna msala!” mpambe wake mmoja aliongea huku akiwa amemshika Jitu na kumzuia asifanye kile alichokuwa anataka kukifanya.
“Hebu niache nimtie displini huyu kenge!” Jitu alifoka.
“Kuna tochi bosi!” mpambe wake alimnong’oneza sikioni.
Taratibu Jitu aligeuza uso wake upande wa kulia. Macho yake yaligongana na macho ya Meja jenerali Cecy Knowman ambaye alikuwa amesimama kwa mbali akiusoma mchezo mzima. Wakati wote huo Jitu alikuwa bado amenikwida sare zangu.
“Shiiiit! Una bahati sana mbwa wewe!” Jitu aliongea kwa hasira akiniachia.
“Tutakutana tena wakati mwingine!” Jitu aliongea akiwaamrisha wapambe wake kuondoka.
Meja jenerali Cecy knowman Bisare alikuwa akiwasindikiza Jitu na wapambe wake kwa macho mpaka walipopotelea upande mwingine. Baada yah apo naye akaondoka kutoka eneo lile alilokuwepo.
Kumbe wakati ule tulipopishana, Meja Jenerali Cecy aliweza kuwaona Jitu na wapambe wake wakitunyemelea kwa nyuma wakiwa wametenganishwa nasi kwa umbali fulani. Wakati huo sisi hatukuwa na habari kama tulikuwa tukifuatiliwa.
Meja Jenerali Cecy akajua ni lazima kulikuwa na shida ambayo ilikuwa inakwenda kutokea. Hii ni kwa sababu alikuwa akimfahamu vema Jitu kwamba alikuwa ni mtu ambaye alikuwa akipenda sana vurugu. Hivyo naye akaamua kuja nyuma ili kuja kuizuia vurugu ambayo ingejitokeza.
“Unajua Wily, hawa wapuuzi tukiendelea kuwafuga watatupanda kichwani!” Salim aliongea akiwa na hasira kweli kweli.
“Hawa ilitakiwa tuwatembezee kichapo cha mbwa koko mpaka waione dunia chungu!” Aboubakar naye aliongea.
“Lakini Wily anawafuga sana hawa. Yaani huyu Jitu tunapozidi kumwacha ndiyo anajiona kama yeye ni yeye na wala hakuna zaidi yake. Anajiona kama kambi yote hii ni yake!” Anthony naye aliongea kwa uchungu.
“Msiwe na hasira ndugu zangu. Muda wote nimekuwa nikiwaasa kwamba msifanye mambo kwa papara wala ghadhabu!” niliwajibu.
“Sawa, ila inauma sana. Yaani Jitu anatuona sisi kama kondoo!” Salim aliongea.
“Mimi sioni haja ya ninyi kuwa na huzuni. Kila jambo lifanywalo huwa na maana zake machoni pa Mungu. Kwa mfano ona leo hii, hivi tungejibu mashambulizi pale mnadhani ingekuwaje? Si mmeona kumbe meja jenerali alikuwa anatutazama. Halafu kwangu ndo ingekuwa mbaya zaidi. Mwanamke yule sasa ndo angejua kwamba mimi ni mkorofi!” niliwaambia kuwapoza rafiki zangu.
“Tunaweza kujichafulia sifa zetu na kutufanya tushindwe kuendelea na mafunzo hapa kambini!” nilizidi kuwaasa.
“Sawa Wily, tumekuelewa!” walijibu wote kwa umoja.
Upande wa pili Jitu na wapambe wake walikuwa na hasira sana. Walikuwa wamekaa kwenye uwanja wa michezo huku hasira zikifukuta ndani ya mioyo yao. Mioyo yao ilikuwa imevimba kwa hasira karibia kupasuka.
“Yaani yule mbwa ana bahati sana. Leo nilipanga nimtoe kabisa meno ya barazani. Nilitaka nimtwange ndoo moja matata ambayo ingefanya anikumbuke katika maisha yake yote!” Jitu alifoka.
“Yaani ashukuru sana Meja Jenerali alifika eneo lile. Sasa hivi angekuwa anapumulia mashine hospitali!” mpambe mmoja alimuunga mkono mwenzake.
“Halafu yule mwanamke amefikaje pale? Unajua hii inashangaza sana!” Jitu aliuliza.
“Yaani hata sisi hatujui. Anajua kunusa kama mbwa mwitu!” mpambe mwingine aliongea.
“Ameniharibia mchongo wangu mpuuzi yule!” Jitu alifoka.
ENDELEA
 
Simulizi: GENERAL’S DAUGHTER 06
Mtunzi: Kalmas Konzo
Simu: 0625 646265
“Lakini kale kajamaa kanaonekana kama kanajiamini sana!” mpambe mmoja wa Jitu aliongea.
“Yaani hata mimi nimeligundua hilo. Ukikatazama machoni na namna kanavyoongea, kanaonekana kama kana kitu fulani hivi cha ziada!” mpambe mwingine aliongea.
“Hebu achene uoga. Yule hana lolote la kututisha. Yule ni uji tu nan do maana alipopewa mazoezi kidogo tu alizimia. Hana lolote yule!” Jitu aliongea.
“Yule inatakiwa tumweke kwenye eneo ambalo halina usumbufu halafu tumpe kichapo cha maana sana!” Jitu aliongezea.
“Sawa tumekuelewa kamanda!” wapambe wake walijibu.
*******
Siku iliyofuata kulikucha vema kabisa. Sote tuliamka na kufanya usafi wa mazingira ikiwemo na vyumba vyetu vya kulala kama ilivyo ada. Baada ya usafi tulipata kifungua kinywa majira ya saa moja kamili.
Baada ya kupata kifungua kinywa tulikusanyika kiwanjani kwa ajili ya kupata matangazo ikiwemo na kusikiliza ratiba nzima ya siku ile.
Tulikuwa tumepanga mistari yetu iliyonyooka vema. Sare tulizokuwa tumezivaa zilitufanya tuonekane nadhifu sana. Siku ile pale kiwanjani hakukuwa na maafisa wengi wa jeshi kama ilivyokuwa kwa siku iliyopita. Walikuwepo maafisa wanne tu pale kiwanjano Meja Jenerali Cecy akiwa mmoja wao.
“Natumaini mmeamka vema kabisa. Karibuni katika siku yenu ya kwanza kabisa ya kuanza mafunzo katika kambi hii yaani Camp 26” Meja Jenerali Cecy alianza kuongea huku sisi tukiwa tumemtegea masikio kumsikiliza.
“Kama ambavyo mlielezwa siku ya jana, mafunzo haya yamegawanyika katika vipengele sita na yatachukua miezi sita mpaka kukamilika kwake. Vipengele hivyo ni kama ifuatavyo; nidhamu, utii, ujasiri, uzalendo, teknolojia na tiba. Kila kipengele kitafundishwa kwa muda wa mwezi mmoja. Na kumbukeni kwamba kila kipengele kitakuwa ni daraja la kukuvusha kwenda katika kipengele kinachofuata” Meja Jenerali Cecy aliendelea kutoa maelezo.
“Nadhani mpaka hapo mmenielewa vema!” Meja Jenerali Cecy aliongea na kumeza funda la mate.
“Ndiyo afande!” tulijibu kwa umoja kwa sauti ya kikakamavu.
“Sasa somo letu la kwanza litakuwa ni nidhamu ambapo rasmi tutaanza kesho. Lakini siku yale itakuwa ni siku ya kuipasha miili yetu moto kwa lengo la kuondoa uchovu. Sasa kila mmoja wenu aende akaingie katika gari alitakalo!” Meja Jenerali Cecy aliongea akituonyesha malori matano ambayo yalikuwa yamepangwa katika upande fulani wa kiwanja kile.
Sote tulitawanyika na kwenda kupanda katika malori yale kama ambavyo tulikuwa tumeelekezwa. Mimi na timu yangu tulihakikisha tunapanda gari tofauti na lile alilopanda Jitu na timu yake. Hii yote ilikuwa ni katika kuepusha shari maana mpaka sasa mimi na Jitu tulikuwa ni kama mafuta na maji. Uadui wetu ulikuwa unazidi kuwa mkubwa sana kadri muda ulivyokuwa ukisonga mbele.
Baada ya kuhakikisha kwamba sote tumeingia ndani ya magari yale, msafara ulianza ukingozwa na Meja Jenerali Cecy. Kila mtu alikuwa na furaha kwa kuona kama mazoezi yenyewe yalikuwa yale ya kupanda magari, basi ilikuwa rah asana.
Msafara ule ulitoka nje kabisa ya kambi na kukamata pori lilokuwa na miti mingi pamoja na nyasi. Magari yaliendelea kuchanja mbuga huko stori za hapa na pale zikiendelea baina yetu.
Takribani kilometa tano kutoka katika kambi ile ya kijeshi msafara wa magari yale ulisimama.
“Haya wote shuka chini!” ilikuwa ni sauti ya Meja Jenerali Cecy ikiamuru.
Sote tulishuka chini na kupanga mistari nyoofu. Tulikuwa kimya tukisubiri kusikiliza maelekezo kutoka kwa Meja Jenerali Cecy.
“Haya, hapa ndipo ambapo tutaianzia program yetu ya siku ya leo!” Meja Jenerali Cecy aliongea huku akitembea huku na kule akimtazama kila mmoja usoni.
“Hakikisha unatumia nusu saa kufika kambini!” Meja Jenerali Cecy aliongea kwa ufupi na baada yah apo yeye na maafisa wengine walianza kwenda kwenye magari.
“Hivi anamaanisha nini?” Aboubakar aliuliza kwa sauti ya chini.
“Ana maana kwamba tunatakiwa kutumia dakika thelathini kutoka hapa mpaka kambini kwa miguu!” nilijibu.
“Inawezekana kweli hii?” Salim aliuliza.
“Inawezekana. Jiandaeni kwani atakayeshindwa atapewa adhabu kali sana!” nilijibu.
“Khaaaa! Sasa tutawezaje kwenda kambini kwa nusu saa? Hapa ni mbali sana!” Jitu alisikika akilalama.
Hakuna ambaye alimsikiliza. Meja Jenerali Cecy pamoja na maafisa wale wengine walipanda kwenye magari na kisha wakaondoka wakituacha pekee pale msituni.
“Huyu mwanamke ni katili sana. Sasa hay ani mazoezi au adhabu?” Jitu aliendelea kufoka.
“Sasa twendeni kwani dakika zinazidi kukata!” niliwaambia wenzangu.
Baada yah apo tuakaanza kukimbia tukifuatiwa na kundi la wanajeshi wengine ambao waikata shauri la kutekeleza amri ile ya kamanda Meja Jenerali Cecy.
Jitu na wenzake walijikuta wakiwa wa mwisho kuondoka pale. Hii ilisababishwa na Jitu ambaye alikuwa akilalama tu pasi kuchukua maamuzi. Pia wenzake wasingeweza kuondoka na kumwacha kiongozi wao pale.
Tuliendelea kukimbia huku tukizidi kupambana na muda. Dakika zilikuwa zikizidi kuyoyoma huku sisi tukiendelea kuufukuza upepo.
Dakika ishirini baadaye wenzangu walikuwa wamechoka sana. Dalili zilionyesha kwamba walikuwa wanaelekea kuzidiwa na kushindwa kuendelea na zoezi lile. Niliamua kuwatia moyo ili tuweze kufanikiwa.
‘Hakuna kukata tamaa, wewe ni askari. Jukumu ulilopewa unaliweza. Usionekane wewe ni dhaifu mbele ya Meja jenerali. Kimbia askari!” niliwahimiza wenzangu kwa kufoka.
Kauli yangu iliwatia moyo na kuwapa ari mpya. Tulizidi kukimbia kwa kasi kwani dakika zilikuwa zimebaki chache sana kabla ya muda tuliokuwa tumepangiwa kuisha.
Nilikuwa najua kile ambacho kingetupata kutoka kwa Meja Jenerali Cecy endapo tungefeli zoezi lile. Hivyo nilizidi kuwahimiza wenzangu wajitahidi kukimbia kwa kasi ili kwa pamoja tuweze kuepukana na kikombe kile ambacho kilikuwa mbele yetu.
Dakika ya ishirini na tisa mimi pamoja na wenzangu watatu tulifanikiwa kuingia kambini na moja kwa moja tulielekea mpaka uwanjani ambako tulimkuta Meja Jenerali Cecy akitusubiri. Dakika ya thelathini wanajeshi wengine kama mia moja na sitini na tatu waliwasili. Hivyo sisi tukawa ndio ambao tumefaulu zoezi lile.
Meja Jenerali Cecy alituambia tuendelee ku warm up kwa kupiga jaramba. Alisema endapo tungeacha ghafla basi tungeweza kukata umeme.
Wanajeshi wengine waliokuwa wakiingia baada ya hapo waliwekwa katika kundi la peke yao.
ENDELEA
 
Simulizi: GENERAL’S DAUGHTER 07
Mtunzi: Kalmas Konzo
Simu: 0625 646265
Nusu saa baadaye kutoka muda uliokuwa umepangwa kufika pale kiwanjani, Jitu pamoja na wapambe wake waliwasili. Walionekana kama walikuwa wamechoka sana. Waliungana na wengine katika kundi la waliofeli zoezi lile mara baada ya kuelekezwa na Meja Jenerali Cecy.
“Haya, tumekwishamaliza hatua ya kwanza ya mazoezi yetu kwa siku ya leo ambapo ilikuwa ni jogging. Aliyevunja rekodi kwa siku ya leo ni Wilson Julius akiwa na wenzake ambao ni Aboubakar, Anthony na Salim ambao wao wamefika hapa dakika ya ishirini na tisa. Wengi miongoni mwenu mlifika dakika ya thelathini kama ambavyo tulikubaliana. Hongereni sana!” Meja Jenerali Cecy alianza kuongea mara baada ya kututaka tusimame.
“Sasa kundi hilo hapo ninyi mmefeli kutekeleza agizo mlilopewa, hivyo basi mtapewa adhabu kali!” Meja Jenerali Cecy aliendelea kuongea.
Maneno ya Meja Jenerali Cecy yalimshangaza Jitu. Hakuamini kama walikuwa wanakwenda kupata adhabu kwa kushindwa kutekeleza jambo ambalo yeye kwa upeo wake aliona kama haliwezekani. Alifyonza sana.
Kwa upande mwingine hasira kali sana iliripuka juu yangu. Aliona kama mimi kwa kufaulu kwangu zoezi lile basi niliwafanya wao waonekane si kitu mbele ya Mj. Aliona kama niliwafanya waonekane ni mayai mdebwedo. Moto wa kisasi ukazidi kuwaka ndani ya kichwa cha Jitu.
“Mtapiga push up elfu moja!” Meja Jenerali Cecy aliongea.
“Khaaaaa! Inawezekanaje hii! Sisi ni binadamu bwana na wala si mashine!” Jitu alilalama kwa sauti ya chini ambayo haikuweza kusikiwa na Meja Jenerali Cecy.
Lakini Meja Jenerali Cecy akawa amemsoma Jitu alichokuwa akikizungumza kwa kumtazama usoni tu. Kwa kuwa alikuwa akimfahamu vema, wala haikumpa shida. Na siku ile akataka kumnyoosha ili awe na hehsima na adabu.
Sisi wengine tukapewa program za mazoezi za kuendelea nazo chini ya usimamizi wa maafisa kadhaa. Meja Jenerali Cecy alienda kudili na wale ambao walikuwa wamefeli zoezi lake yaani akina Jitu.
Unajua wakati Meja Jenerali Cecy akitangaza kwamba wale waliokuwa wamefeli zoezi lake watatakiwa kupiga push up elfu moja alikuwa akidhani ni utani. Hii yote ilitokana na jinsi ambavyo Meja Jenerali Cecy alikuwa akiongea. Alikuwa akiongea kama hamaanishi vile. Ukijumlisha na uzuri, urembo pamoja na utamu wa sauti yake basi ndiyo utadhani kama anakusimulia hadithi tamu ya mahaba.
Hakufahamu kwamba hicho ndicho ambacho kilinikuta mimi siku ya kwanza wakati nawasili pale kambini. Yeye alichokuwa akifahamu ni kwamba mimi nilikuwa goigoi kwa sababu nilizimia katika kufanya mazoezi. Hakujua ni zoezi lipi ambalo nilikuwa nimepewa.
Wanajeshi wengine wakawa wameanza kutekeleza adhabu ile isipokuwa Jitu pamoja na wapambe wake ambao walikuwa bado wamesimama. Meja Jenerali Cecy aliwafuata na kuwatazama kwa zamu kuanzia kichwani mpaka unyayoni.
“Kwa nini hamtekelezi adhabu?” Meja Jenerali Cecy aliuliza akifoka.
“Samahani afande, adhabu uliyotupa haitekelezeki kwa binadamu wa kawaida. Tunaomba utubadilishie adhabu!” Jitu aliongea kwa kujiamini.
Hatujui ni kwa nini Jitu alikuwa akijiamini hivi mbele ya Meja Jenerali Cecy. Lakini kuna siri nzito kati ya wawili hawa ambayo mbele tutakwenda kuifahamu. Haiwezekani kiongozi ambaye kambi nzima ilikuwa ikimwogopa yeye alikuwa akimchukulia kama mdogo wake.
Achilia mbali ile nafasi ya kuwa kiongozi na mwalimu pale kambini lakini Meja Jenerali Cecy alikuwa na cheo kikubwa sana kijeshi. Alikuwa amebakiza nafasi moja yaani kuwa Jenerali kamili ambacho ndicho cheo kikubwa kabisa jeshini. Hivyo Meja Jenerali Cecy alikuwa anapaswa kuheshimiwa, kuogopwa na kunyenyekewa sana na si kupuuzwa kama ambavyo alikuwa akifanya Jitu.
“Haya hebu piteni pale mbele!” Meja Jenerali Cecy aliongea kwa sauti ya upole sana.
Jitu na wenzake walifurahi sana. Waliona kwamba ombi lao lilikuwa limesikilizwa na kukubaliwa na kwamba walikuwa wanakwenda kubadilishiwa adhabu na kupewa adhabu nyepesi zaidi. Kimoyo moyo walimpongeza sana Jitu kwa ujasiri wake na pia sasa ndiyo wakaamini kwamba Meja Jenerali Cecy alikuwa akimwogopa sana Jitu kama ambavyo Jitu alikuwa amewaaminisha.
Walienda mbele kama ambavyo Meja Jenerali Cecy aliwataka kufanya. Baada yah apo Meja Jenerali Cecy aliwafuata na kuanza kuwakagua tena kwa mara ya pili kama alikuwa hawafahamu vile. Yaani utadhani alikuwa ndiyo anakutana nao kwa mara ya kwanza.
“Kwa hiyo mnataka kubadilishiwa adhabu au siyo?” Meja Jenerali Cecy aliuliza.
‘Ndiyo afande!” wote walijibu kwa ukakamavu macho wakiwa wameyatungua mbele.
Hawakuelekewa ni nini ambacho kilikuwa kimetokea, lakini ndani ya dakika moja walijikuta wakiwa wamekaa chini ardhi. Baadaye ndipo akili yao ikakaa sawa na kugundua kwamba walikuwa wamezolewa na mateke makali kutoka kwa Meja Jenerali Cecy ambayo yaliwakalisha chini.
Kwa sasa akawa amebaki Jitu tu aliyekuwa amesimama akiwa anashangaa kwa kile ambacho kilikuwa kimetokea. Hakuamini kama jambo lile linaweza kutokea kwa haraka kiasi kile.
Kabla hajatafakari zaidi alibandikwa ngumi ya shav una kisha akafyatuliwa mtama ambao ulimkalisha chini. Mtoto wa kike yule alikuwa hatari sana.
Macho yakawatoka wakiwa bado wanashindwa kuamini kwa kile ambacho kilikuwa kinatokea. Sasa wakajua kwamba Meja Jenerali Cecy alikuwa ni hatari sana tofauti na vile ambavyo walikuwa wakimchukulia.
“Mnataka kupiga push up elfu mbili?” Meja Jenerali Cecy aliwauliza.
“Hapana afande!” wote walijibu kwa woga na kuanza kupiga push up.
Jitu ambaye mara ya kwanza alikuwa akijifanya kwamba yeye ni jemedari, alikuwa ndiyo wa kwanza kutekeleza adhabu ile. alikuwa akitetemeka sana kwa dhahma ile ya ghafla ambayo ilikuwa imewakumba.
Kitendo kile kilileta woga san ahata katika mioyo ya wanajeshi wengine. Wakaendelea kuitekeleza adhabu ile kwani hawakutaka yawapate kama yale yaliyokuwa yamempata Jitu pamoja na wenzake.
Adhabu ile ilikuwa kali sana. Push up elfu moja hakikuwa kitu rahisi sana kutekelezeka. Kuna wengine walikuwa wakiishia njiani na kubaki wakigaagaa machozi yakiwatiririka.
Hata kwa mwamba mwenyewe Jitu adhabu ile ilikuwa imemlemea. Kwa mara ya kwanza mwanaume aliweza kudondosha machozi akiomba kusamehewa. Lakini Meja Jenerali Cecy alikuwa ameuvaa uso wa mbuzi na kuzidi kuusimamia msimamo wake.
ENDELEA
 
Simulizi: GENERAL’S DAUGHTER 08
Mtunzi: Kalmas Konzo
Simu: 0625 646265
“Mtalia na kutoa machozi, adhabu hii lazima itekelezeke. Hata utoe machozi ya damu usitegemee huruma kutoka kwangu!” Meja Jenerali Cecy alifoka akiwatka kuendelea na adhabu ile.
Meja Jenerali Cecy alikuwa anakimaanisha kile ambacho alikuwa akikiongea. Licha ya kulia na kuomboleza, alihakikisha wanaendelea na adhabu ile. hskiks siku ile Jitu alikuwa ameingia kwenye kumi na nane za Meja Jenerali Cecy.
Mpaka wanamaliza adhabu ile walikuwa hoi wanashindwa hata kunyanyuka. Walikuwa wamechoka sana mikono haina kazi kwa maumivu makali. Jitu alikuwa amekunja sura na kudhihirisha Dhahiri chuki ambayo alikuwa nayo kwa Meja Jenerali Cecy.
Basi hasira za Jitu zikazidi kuwaka juu ya Meja Jenerali Cecy akiapa kimoyo moyo kwamba ni lazima angekuja kulipiza kisasi. Aliona kwamba alikuwa ameonewa sana.
“Yaani huyu mwanamke atakuja kujuta kwa nitakachomfanya. Nitamfanya asinisahau katika maisha yake!” mawazo machafu yalitembea katika fikra za Jitu.
Mawazo ya Jitu yakaendelea kuzitafuna fikra zake. Akaona kwamba mimi nilikuwa ndiye chanzo cha matatizo yale yote. Aliamini kwamba mimi nilikuwa ni mtu mpenda sifa kwa viongozi. Hivyo nami alipanga kunikomesha.
“Huyu mbwa ndiye aliyesababisha yote haya. Sasa naye nitamfanya ajute. Atajuta ni kwa nini alikuja hapa kambini. Mimi ndiyo Jitu bwana katu siwezi kushindwa na pia hakuna hata mtu mmoja ambaye huwa anathubutu kuingia katika njia zangu!” Jitu aliendelea kutafunwa na mawazo.
Mazoezi yaliendelea huku Meja Jenerali Cecy akiyasimamia vema kabisa. Yalikuwa ni mazoezi mbalimbali ya ukakamavu pamoja na kujenga mwili.
Saa sita kamili ndiyo programu ile ya mazoezi kwa siku ile ilifungwa. Tulikuwa hoi sana kwani mazoezi ambayo tulikuwa tumeyafanya yalikuwa ni mazito sana.
“Tumemaliza session yetu kwa siku ya leo!” Meja Jenerali Cecy alianza kuongea mara baada ya sisi sote kupanga mistari nyoofu mbele yake.
“Jambo ambalo ninawasisitiza ni nidhamu. Wewe ni askari, umeletwa hapa kwa kuwa uliaminiwa kwamba u thabiti kabisa. Ukosefu wa nidhamu si jambo ambalo linavumilika katika kambi hii. Mheshimu mwenzako nay eye atakuheshimu!” Meja Jenerali Cecy aliendelea kukongea huku sisi tukimsikiliza kwa makini.
Kesho mtaanza na kipengele chwa kwanza kabisa darasani. Ninaomba kila mtu ahudhurie kwani ni muhimu sana. Pia ninawapa saa moja la kuweza kufanya usafi wa miili yenu. Saa saba kamili mtakwenda mesini kwa ajili ya kupata chakula. Baada ya chakula mtaendelea na ratiba zenu nyingine binafsi!” Meja Jenerali Cecy aliongea na baada yah apo aliondoka akifuatiwa na maafisa wengine.
Nasi tukatawanyika kwa ajili ya kwenda kuoga na kupata chakula.
*********
Siku iliyofuata ikawa ndiyo siku ya kwanza rasmi kuanza mafunzo yetu pale kambini. Ilikuwa ni siku ambayo tulikuwa tukianza kipengele cha kwanza katika mafunzo yetu ambacho kingeenda kwa muda wa mwezi mmoja. Kipengele hiki kilikuwa ni Saikolojia.
Saikolojia lilikuwa ni somo muhimu sana kwa mwanajeshi. Katika somo hili tulikuwa tunakwenda kujifunza namna ya kumtambua mtu mawazo yake na kile ambacho anakipitia katika maisha yake kwa kumtazama tu.
Hii ina maana kwamba, kwa kujifunza somo hili itakuwa rahisi kwetu kumjua adui ndani nan je na kujua namna ya kukabiliana naye.
Tuliingia darasani kwa ajili ya kumsubiri mwalimu wa somo hili. Mimi na kampani yangu kama kawaida tulikaa katika viti vinavyofuatana katika upande tofauti kabisa na ule ambao Jitu na kampani yake walikuwa wamekaa. Isingewezekana kwa sisi kukaa jirani kwa sababu tulikuwa ni mahasimu wakubwa sana.
Dakika mbili baadaye mwalimu wa saikolojia aliingia. Alikuwa ni mwalimu wa kike mwenye umbile jembamba. Sote tulisimama na kumsalimu kwa heshima. Mwalimu alitujibu salamu yet una kisha akaturuhusu tukae.
“Nilikwishafanya utambulisho wangu tayari hivyo hakuna ulazima wa kujitambulisha tena. Kwa kifupi mimi ndiye mwalimu wenu wa saikolojia na nitakuwa nanyi katika somo hili kwa muda wa mwezi mzima huu wa kwanza. Ninachoomba ni usikivu wenu kwani somo hili ni muhimu sana katika tasnia yenu!” mwalimu yule alianza kuongea.
“Saikolojia ni kitu cha muhimu sana kwako wewe mwanajeshi. Hapa utaweza kumtambua adui yako ni nini anachokiwaza na hivyo itakuwa rahisi kwako kukabiliana naye. Unaweza kutambua mawazo na maisha ya adui yako kwa kumtazama maumbile yake, mtindo wa mavazi yake, namna anavyoongea, anavyotazama, anavyopumua na kadhalika!” mwalimu yule aliendelea kutupa somo lile muhimu.
“Sasa hiyo itawezekanaje mwalimu? Mimi naona hapo ni lazima patakuwa na uchawi kidogo. Utawezaje kujua maisha ya mtu kwa kumtazama? Haiwezekani bwana!” Jitu alikurupuka na kumpinga mwalimu.
Mwalimu yule hakujisikia vema kwa maneno yale ya kashfa ya Jitu. Badala yake alimuacha na kuendelea kutoa somo.
“Hii inawezekana, saikolojia imekuwepo kwa muda mrefu na imekuwa ikitumika katika sekta mbalimbali kwa mafanikio makubwa!” mwalimu aliendelea.
Lakini kumbe Jitu alikuwa anasinzia tangu mwalimu alipokuwa ameingia pale darasani na mwalimu alilibaini hilo. Hata mara baada ya kuuliza swali lake la kebehi Jitu aliendelea kuuchapa usingizi na kutomsikiliza kabisa mwalimu.
“Haya, wewe hapo hebu simama!” mwalimu aliongea akimnyooshea kidole Jitu.
Wenzake walimshtua kwani kwa wakati huo alikuwa akiufaidi ubwabwa wa mwana. Alikurupuka na kuyafuta macho yake pamoja na udenda uliokuwa ukimporomoka pasi breki.
“Jina lako ni Sajidu Bufa!” mwalimu alianza.
“Khaaaa! Umelijuaje jina langu wakati wanafunzi tuko wengi sana hapa kambini?” Jitu aliuliza kwa mshangao.
“Nataka nikuonyeshe namna saikolojia inavyofanya kazi. Nimelifahamu jina lako kwa sababu wewe ni mwanafunzi mkorofi sana hapa kambini. Huwa unapenda sana sifa mbele za watu. Hii ikanifanya niweze kulitafuta jina lako na kukufahamu vema!” mwalimu aliongea.
Jitu alibaki kimya akiwa ameumbuka.
“Pili jana ulifanya kazi nzito sana, tatu baba yako ni mtu mwenye nafasi kubwa sana katika nchi hii na anakupenda sana!” mwalimu aliendelea kutema cheche.
“Khaaa! Jamani, umeyajuaje yote hayo kwa sababu ni sahihi kabisa. Au mwalimu unanifahamu kabla?” jitu aliuliza kwa mshangao.
ENDELEA
 
Simulizi: GENERAL’S DAUGHTER 09
Mtunzi: Kalmas Konzo
Simu: 0625 646265
“Hapana Sajidu, mimi sikufahamu hata kidogo. Nimetumia saikolojia kuyafahamu haya. Nimejua kwamba jana umefanya kazi nzito kwa sababu tangu nimeingia darasani wewe umekuwa ni mtu wa kuchapa usingizi mpaka unatoa udenda. Hali hii humpata mtu ambaye ana uchovu mwingi sana”
“Pia nimetambua kwamba wewe una dharau sana, mdhalilishaji na unapenda sifa kutokana na swali uliloniuliza. Swali lako lilikuwa ni la msingi na la muhimu lakini namna ambavyo umeliuliza dhamira yako ilikuwa ni kuniumbua mimi kwa sababu ni mwanamke. Ulifanikiwa kwa hilo kwa sababu wenzako walicheka. Lakini leo nitakufunza kuhusu saikolojia!” mwalimu aliongea na kumwacha Jitu akiwa ameyatoa macho yake kwa aibu mithili ya mjusi aliyebanwa na mlango.
“Pia nimegundua kwamba wazazi wako ni watu wenye nafasi hapa nchini kutokana na wewe jinsi unavyojiona wa thamani kuliko wengine. Na pia jinsi vile unajiamini kwamba hakuna mtu yeyote anaweza kukufanya jambo lolote kwa sababu baba yako anakupenda san ani lazima atakutetea!”
“Haya niambie, lipi si sahihi kukuhusu wewe!” mwalimu alimwambia Jitu.
Jitu akabaki kimya akiwa ameumbuka. Akawa hana la kusema. Akawa amepoa utadhani mtu ambaye alikuwa amelowa na maji ya mvua. Na mwalimu kwa upande wake akawa amefanikiwa somo lake kwa kutoa mfano halisi kabisa. Wanafunzi walimpigia makofi mwalimu na kumshangilia sana.
Hakika siku ile tukawa tumepata somo kubwa sana katika maisha yetu ya kijeshi. Lakini Jitu kwa upande wake yeye alikasirika sana. Alijihisi kuumbuliwa sana siku ile na mwalimu. Alijiona kama thamani yake ilikuwa imeshuka sana kwa wapinzani wake hasa mimi. Akaona kama hilo linaweza kuwa kikwazo sana katika mapambano dhidi yangu. Mwalimu wa saikolojia naye akawa ameingia katika orodha ya watu ambao wanachukiwa sana na Jitu.
Baada ya darasa lile sote tukaenda kupata chakula kwa sababu muda wa chakula cha mchana ulikuwa umekwishafika. Baada ya chakula kila mmoja akawa huru kuendelea na ratiba zake nyingine kwa sababu hakukuwa na ratiba nyingine ya mafunzo kwa siku ile.
Jitu pamoja na wapambe wake wakawa na kikao kizito sana. Kilikuwa ni kikao kizito sana ambacho kilikuwa chini ya uenyekiti wa Jitu ambaye alikuwa ni mwenye ghadhabu sana.
“Ninyi ni jamaa zangu ambao mmekuwa mkinisapoti toka tumefika hapa kambini. Na pia naendelea kuwaahidi maisha mazuri kwa sababu mnanifahamu mimi ni nani pamoja na familia yangu” Jitu alianza kuongea akifungua kikao kile.
“Sasa mpaka wakati huu kuna watu watatu ambao ni maadui zangu wakubwa sana. Mtu wa kwanza ni yule Wily, wa pili ni Meja jenerali Cecy na wa tatu ni huyu mwalimu wa saikolojia. Watu hawa wanajaribu kucheza na maisha yang una wanataka kupiga ili wapate kujua mimi ni nani na nina nini juu yao. Nami nasema kwamba nitawapa kile ambacho wanakitaka!” Jitu alifoka.
Kila mtu kwenye kikao kile alikuwa kimya kwani kwa ghadhabu ile ambayo alikuwa akiionyesha hakuna aliyethubutu kufungua mdogo. Watu walikuwa wakimfahamu Jitu kwamba endapo wangefungua vinywa vyao na kwa bahati mbaya wakapishana katika mazungumzo, basi wangejikuta madhira ya ghadhabu zake wameyabeba wao. Hivyo njia nzuri kwao ikawa ni kufunga vinywa vyao.
“Mbona mko kimya? Ina maana hakuna hata mmoja ambaye yuko nami! Nyote mko upande wa wale wapumbavu au siyo!” Jitu alifoka.
“Hapana bosi, sisi sote tuko pamoja nawe na tunakuunga mkono kwa kila kitu!” wajumbe wale walijibu kwa woga.
Lakini kiuhalisia mioyo ya wajumbe wale ilikuwa ina uoga sana juu ya mwenend wa kiongozi wao. Katika watu wote ambao Jitu aliwataja kama maadui zake waliyemwogopa zaidi alikuwa ni Meja jenerali Cecy.
Walikuwa na hofu juu ya hatima yao kijeshi kwa sababu Meja jenerali Cecy alikuwa ni mtu mzito sana katika jeshi. Cheo chake kilikuwa ni kikubwa sana. Hivyo kujiingiza katika mapambano naye ilikuwa ni kama kuyachezea kamari maisha yao. Cecy hakuwa mtu wa kufanyiwa mzaha hata kidogo.
Lakini hawakuwa na namna nyingine ya kuachana na hatari ile iliyokuwa inawakabili mbele yao kwa sababu Jitu alikuwa ni rafiki yao mkubwa ambaye walikuwa wamekula yamini ya kuwa naye katika kila jambo kwenye maisha yao yote. Hivyo hawakuwa na budi ya kuendelea kuungana naye na kumsikiliza pamoja na kukitekeleza kila ambacho alikisema.
“Safi sana simba wangu. Hakika najivunia sana kuwa nanyi. Mmekuwa mnanifanya niendelee kuwa jasiri kwa sababu ninafahamu kwamba nina simba wangu ambao wapo nami katika hali yoyote ile. Na kila siku umoja wetu ndio ambao ,umetufanya tuwe tunashinda!” Jitu aliendelea kuongea.
“Sasa watu hao ambao nimewataja nitahakikisha nafanya wajute katika maisha yao yote. Nitawafanya wajute ni kwa nini walikutana na Jitu katika maisha yao. Nataka niwafanye kila watakaponiona wanione kama shetani mwenye uwezo wa kuchukua roho zao wakati wowote ule!” Jitu alisita na kumeza funda la mate.
Baada yah apo aliwatazama wajumbe kwa zamu na kisha akaendelea, “Sasa walichokuwa wanakitaka, kinakuja!”
*******
Mfumo wa mabweni ambayo tulikuwa tukiishi pale kambini ulikuwa mzuri sana. Tulikuwa tukiishi katika vyumba ambavyo kila chumba kilikuwa na uwezo wa kuchukua watu watano. Na sisi kwa upande wetu tulikuwa tukiishi wanne katika chumba chetu kimoja. Hii ilisaidia sana katika usalama wetu kutoka kwa adui yetu jitu.
Yalikuwa ni majira ya saa nane adhuhuri, jua lilikuwa kali sana. Sisi kwa wakati huo tulikuwa tumepumzika kule bustanini tukipunga hewa safi pamoja na kukifaidi kivuli. Nilikuwa napapenda sana pale bustanini, na kila mara tunapopata wasaa wa kupumzika nilikuwa nikiwashauri wenzangu kwenda kule. Ikafika kipindi wenzangu wakawa wamejua kwamba bustani ile ilikuwa ni sehemu ambayo nilikuwa nikiipenda sana.
“Vipi Anthony, hivi ulifunga mlango wa bweni?” niliuliza.
Mlango nilifunga na ufunguo huu hapa!” Anthony alijibu akinionyesha ufunguo katika mkono wake.
“Tunapaswa tuwe makini na kila tulifanyalo maana huyu Jitu kwa sasa ni adui yetu mkubwa na akili zake ni fupi sana!” niliongea.
“Tumekuelewa Wily!” jamaa zangu walijibu kwa umoja.
ENDELEA
 
Simulizi: GENERAL’S DAUGHTER 10
Mtunzi: Kalmas Konzo
Simu: 0625 646265
“Lakini ni mpaka lini huyu mwendawazimu ataendelea kusumbua hapa kambini? Kwani nini tusimvamie na kumshikisha adabu?” Salim aliuliza.
“Salim, nadhani bado unakumbuka nilishawahi kuwaambia kwamba jambo lolote jema hupaswi kulifanya kwa pupa. Inapaswa kutanguliza busara mbele ili uweze kutambua unalifanya vipi na kwa ufanisi!” nilimjibu Salim.
“Lakini Wily, tunaposema tuwe wapole na tutangulize busara mbele ndipo ambapo Jitu anatuona maboya. Na tukiendelea hivi anaweza kutuwahi na kututenda jambo baya sana!” Salim aliongea huku moyo wake ukiwa na hofu sana juu ya mustakabali wetu.
“Nikuondoe hofu Salim, hakuna jambo lolote baya ambalo Jitu anaweza kutenda juu yetu. Endeleeni kuniamini!” nilijibu.
Kwa kiasi fulani rafiki zangu wale walianza kuwa na mashaka na uwezo wangu katika mapambano. Walinikubali kwamba nilikuwa ni mtu mwenye akili nyingi pamoja na hekima. Lakini walianza kuamini huenda uwezo wangu katika mapambano ulikuwa hafifu.
Hii yote ilitokana na jinsi ambavyo nilivyokuwa nikiwapa maneno ya kumkwepa Jitu pindi ilipokuwa ikijadiliwa kupambana naye. Walianza kuhisi kwamba nilikuwa ninamhofia Jitu na ndiyo maana nilikuwa nikimkwepa. Walidhani kwamba nilikuwa sipendi kuyaweka wazi madhaifu yangu mbele yao.
Hawakutaka kuniambia hili bali walilimeza na kulifanya liwe siri ya mioyo yao. Lakini kwa sasa wakaanza kunitazama kwa jicho la tofauti la hadhari wakihofia kwamba huenda kuna siku ninaweza nikawauza na kukimbia endapo tukivamiwa na Jitu.
Niliyasoma mawazo yao hayo katika fikra zao. Sikuacha kuendelea kuwapa moyo na kuwataka wasichukue mambo kwa pupa bali watafakari kabla ya kutenda kwani hii ingewaepusha na hatari.
“Hebu tuachane na hayo, vipi kuhusu Meja jenerali, bado unamchukia?” Aboubakar aliongea kuepusha shari ambayo ilikuwa inanukia kwa mbali.
“Mimi katu siwezi kuwa na mazoea na mwanamke yule. Amenitoka kabisa moyoni mwangu!” nilijibu.
“Lakini ni mwanamke mzuri na mrembo sana. Ana mvuto ambao unamfanya kila mwanaume atamani kuwa karibu naye ukiachilia cheo kikubwa alicho nacho na nafasi yake hapa kambini!” Aboubakar aliongea.
“Aboubakar, mwanamke yule ni katili sana. Cecy ni mnyama tofauti na ninyi ambavyo mnamtazama na kumchukulia. Mtakuja kuyasadiki maneno yangu siku ambayo mtaingia katika kumi na nane zake. Hafai kabisa mwanamke yule!” nilijibu.
“Ha ha ha haaaaa! Mimi nadhani hizo ni persona affairs. Wewe wamwona katili kwa sababu alikupigisha kwata mpaka ukazimia. Lakini mwanamke yule ni mwema sana kwa upande mwingine!” Salim aliongea.
“Wema wake uko wapi? Ninyi mnalewa sana na jinsi anavyoongea pamoja na utamu wa sauti yake. Mtakuja kujuta ndugu zangu!” niliwaonya.
“Yaani umekwishasahau siku ile alivyotuokoa kutoka katika mikono ya Jitu hapa bustanini!” Anthony naye alichangia.
“Alituokoa kivipi? Yule hamna lolote!” nilijibu.
“Hivi kwa mfano siku ile aasingetokea, unadhani ingekuwaje?” Aboubakar aliuliza swali la kichokozi kwa lengo la kunipima.
Lakini mimi nilikwishampima saikolojia yake. Rafiki zangu hawa walikuwa bado hawajanifahamu kiundani. Walinichukulia po asana.
“Kingetokea kile ambacho kilitarajiwa kutokea. Meja jenerali Cecy katu siwezi kuja kumpa nafasi japo kwenye mawazo yangu. Yule ni chui hasa!” niliongea kwa kumaanisha.
“Mh! Mimi nadhani hapo nyota zenu haziendani. Huwa unatokea hii katika maisha. Unaweza jikuta unamchukia mtu kwa ajili ya kitu kidogo sana!” Salim aliongea.
“Basi kwa mimi na Cecy naomba ibaki kuwa hivyo hivyo kwamba nyota zetu haziendani. Nitabaki kuwa mbali na mwanamke yule ili kuepusha shari. Namheshimu kwa sababu ni mwalimu wangu. Tofauti nah apo basi sasa hivi tungekuwa tunazungumza mengine!” nilijibu.
Lakini ghafla kabla hatujaendelea na maongezi yetu sauti ya king’ora ilisikika. Sote tulishtuka kwa sababu haikuwa kawaida. Kifaa kitumikacho kwa mwito wa kuwakusanya wanajeshi ni kengele. King’ora hulia kuashiria kwamba kuna jambo la hatari linakuwa limetokea pale kambini.
Basi kwa mlio ule wa king’ora nasi tukajua kwamba kulikuwa na jambo la hatari ambalo lilikuwa limetokea. Sote kwa pamoja tulisimama kutoka pale chini tulipokuwa tumekaa na kuanza kukimbia kuelekea kule ambako tulikuwa tunatakiwa kwenda.
Tulipofika katika sehemu ya kukusanyikia tuliwakuta baadhi ya wanajeshi wakiwa wamekusanyika huku wengine wakiendelea kuja kwa kukimbia. Sote tulipanga mistari minyoofu mbele ya maafisa wa jeshi viongozi wa kambi ile. wao walikuwa tayari wamekwishafika pale kitambo kabla yetu.
Lakini mkusanyiko wa leo haukuwa kawaida. Jenerali Knowman Bisare naye alikuwepo. Kama ambavyo tulidhani nadhani ndivyo ambavyo ilikuwa. Kulikuwa na jambo la hatari ambalo lilikuwa limetokea. Sote tukatega masikio yetu kwa ajili ya kujulishwa jambo hilo.
“Hamjambo askariiiiiii!” Jenerali Knowman Bisare aliongea kwa ukakamavu wenye jazba.
“Hatujambo afande!” sote tulijibu kwa ukakamavu uliokuwa na dalili za woga ndani yake kutokana na hali ya kusanyiko lile.
“Awali tulidhani nyote mu wema, lakini tumekuja kubaini kwamba miongoni mwenu kuna askari ambao si wema. Askari hao hawastahili kuwa askari jeshi kwa sababu wanakosa sifa za kuwa askari jeshi!” Jenerali Knowman Bisare alitulia na kuvuta funda la mate huku akitutazama.
Sisi tulikuwa kimya tumesimama tisti macho tumeyakaza mbele kumsikiliza. Macho yangu ya wizi yaliweza kuwaona wanajeshi wote wakiwa na nyuso za woga. Ila kwa Jitu pamoja na wapambe wake hali ilikuwa tofauti. Wao hawakuwa na nyuso za woga.
Nilijiuliza ni kwa nini iko vile lakini nilikosa majibu. Nikaamua kuendelea kumsikiliza Jenerali Knowman Bisare.
“Adhuhuri hii kuna tukio la wizi ambalo limetokea hapa chuoni. Basi kama wewe unajiona umehusika na tukio hilo nakupa nafasi ya kupita hapa mbele kabla hatujaanza kuchukua hatua stahiki katika kumtafuta mwizi huyo!” Jenerali Knowman Bisare alifoka.
“Kwa maneno mengingine naweza kusema kwamba mwizi huyo asifanye mambo yakawa na mlolongo mrefu wakati yeye mwenyewe anajitambua kuhusika na tendo hilo!” Jenerali Knowman Bisare aliendelea kuongea kwa kufoka.
Alinyamaza kama sekunde kumi hivi kupisha kama kuna mtu akijitokeza pale mbele. Lakini hakuna aliyefanya hivyo.
ENDELEA
 
Simulizi: GENERAL’S DAUGHTER 11
Mtunzi: Kalmas Konzo
Simu: 0625 646265

“Sasa ngoja niliweke jambo hili kwa uwazi. Kuna mtu ameingia katika ofisi yangu wakati mimi nimetoka kidogo na kuiba bastola yangu. Kama umefanya hivyo, tafadhali pita mbele!” Jenerali Knowman Bisare aliongea.

“Haaaa!” sote tulishangaaa maana tukio hilo lilikuwa kubwa sana na wala hatukulitegemea.

“Mnashangaa nini? Mnajifanya hamjui wakati mwizi yumo miongoni mwenu!” Jenerali Knowman Bisare alifoka kwa ghadhabu kuu.

“Meja jenerali Cecy, huyu mwizi yumo humu humu ndani na silaha hiyo bado imo humu kambini. Sasa kila askari akaguliwe katika chemba anayolala!” Jenerali Knowman Bisare aliamuru.

Basi wote tukazuiwa pale kiwanjani huku ukaguzi ukianza kufanyika vyumbani. Wahusika wa chumba kilichokuwa kikikaguliwa ndiyo ambao walikuwa wakiitwa huku wengine wakisubiri pale kiwanjani kusubiri zamu yao. Tendo hilo liliendelea kwa muda mrefu.
Hatimaye zamu ya chumba chetu kukaguliwa ilifika. Mimi na wenzangu tuliitwa. Tulienda kwa kujiamini huku tukiwa na amani moyoni kwa sababu tulijua kwamba sisi hatukuwa wahusika wa jambo lile kwa asilimia zaidi ya mia moja.

Basi tuliingia ndani ya chemba yet una ukaguzi ukaanza kufanyika. Wakaguzi walikuwa makini sana wakiongozwa na Meja jenerali Cecy. Sisi tulisimama tu kwa furaha tukilishuhudia zoezi lile.

“Afande, njoo uone!” askari mmoja aliongea mara baada ya kufunua godoro la kitanda changu.

Askari wote walienda pale kwenda kushuhudia kile ambacho walikuwa wameitiwa. Macho yaliwatoka kwa kile ambacho walikiona.

“Kitanda cha nani hiki?” Meja jenerali Cecy aliuliza kwa ukali.

“Cha kwangu afande!”nilijibu huku nikisogea mbele ya wenzangu.

Kitendo cha kujitokeza tu nilijikuta nimewekwa kati huku mitutu ya bunduki ikinielekea. Cecy aliitoa bastola ambayo ilikuwa imehifadhiwa chini ya godoro la kitanda changu. Ilikuwa ni ile bastola ya Jenerali Knowman ambayo ilikuwa ikitafutwa.

“Khaaaaaa!” ilinitoka bila kutarajia huku wenzangu nao wakishangaa.

“Kumbe wewe ni gaidi!” Meja jenerali Cecy alifoka.

“Hapana afande. Mimi siko kama ambavyo mwanidhania. Jambo hili limepangwa!” niliongea kujitetea.

Licha ya kuongea vile lakini bado moyoni nilibaki na mshangao kwa sababu jambo lile lilikuwa haliwezekani hata kidogo. Mlango wa chumba kile ulikuwa umefungwa na ufunguo tulikuwa nao sisi. Sasa iweje itokee vile!

“Hebu funga pingu hawa wote na kisha twende nao uwanjani!” Meja jenerali Cecy aliongea.

“Hapana afande, naomba hawa ndugu zangu usiwahusihe katika hili. Naomba mzigo wote wa lawama niubebe mimi kwa sababu bastola imekutwa kwenye kitanda changu!” niliongea nikiomboleza.

“Ninyi nyote ni wamoja. Funga wote na kisha twendeni!” Meja jenerali Cecy aliongea akionyesha kuwa anamaanisha kile alichokuwa amekisema.

Niliwaona Dhahiri jinsi ambavyo wenzangu walivyokuwa wakitetemeka pindi walipokuwa wakifungwa pingu. Hakika niliwaonea huruma. Niliona kama nilikuwa nimewaingiza katika balaa ingawa nami sikulitenda kosa lile.

Tulitolewa nje ya chumba kile huku tukiwa tumefungwa pingu mikononi nyuma ya migongo. Mitutu ya bunduki kutoka kwa maafisa wale makini wa jeshi ilikuwa imetuelekea kila kona.

Askari wenzetu walikuwa wakishangaa pindi ambapo tulikuwa tukipelekwa pale kiwanjani. Walijiuliza ilikuwa imewezekanaje ile wakati mimi nilikuwa naonekana ni askari mstaarabu sana na mwenye busara. Walibaki njia panda.
Tulienda kupigishwa magoti mbele ya Jenerali Knowman. Machozi yalikuwa yakinilengalenga kutokana na tukio lile la udhalilishaji. Huruma yangu ilikuwa ni kwa wenzangu.

“Naripoti afande! Bunduki yako imekutwa chini ya godoro katika kitanda cha askari Wilson Julius!” Meja jenerali Cecy aliongea mara baada ya kupiga saluti.

“Wilson Julius ni nani?” Jenerali Knowman aliuliza.

“Ni mimi afande!” nilijibu.

“Sasa nataka wanyooshwe mpaka waeleze wao ni akina nani. Hawa sidhani kama ni askari wa kawaida. Nataka waelezwe wametumwa nan ani na lengo lao ni nini!” Jenerali Knowman alifoka.

Kwa mbali macho yangu yalimwona Jitu akiwa ni mtu mwenye furaha sana. Inaonyesha tukio lile kwake lilikuwa ni faida kubwa sana. Na kweli ilikuwa ni faida kwake kwani nilikuwa nimeanguka mbele yake pasi yeye kutumia nguvu yoyote.

“Meja jenerali Cecy, sasa ni wakati wa kuifanya kazi yako!” Jenerali Knowman alionga na kisha akaondoka.

“Wapelekeni chumba cha giza!” Meja jenerali Cecy aliongea.

Hakukuwa na majadiliano zaidi. Tulichukuliwa mzobemzobe na kuelekezwa huko katika chumba cha giza ambako hakuna hata mmoja wetu aliyekuwa akikufahamu.

Tulipitishwa katika majengo kadhaa na baadaye tukafikishwa katika jengo moja ambalo lilikuwa na uzio wa nyavu. Jengo hili sote tulikuwa tujiua kama ni karakana kwa sababu ndani ya uzio ule kulikuwa kumeegeshwa magari mabovu ambayo yalikuwa yakisubiri kutengenezwa.

Tuliingizwa ndani ya uzio ule na kupelekwa moja kwa moja mpaka katika jengo tulilokuwa tukitazamana nalo mbele yetu. Mlango ulifunguliwa na kisha tukaingizwa ndani.
Ndani ya chumba ambacho tulikuwa tumeingizwa hakukuwa na mwanga. Ilikuwa ni giza totoro. Tulifungiwa mle ndani angali tukiwa bado mikono yetu imefungwa pingu. Hatukuweza kuonana mle ndani.

Tulianza kupiga kelele tukiomba tufunguliwe kwani hatukuwa tumefanya kosa lolote. Lakini hakuna ambaye alizisikia kelele zetu kwani hatukujua askari wale waliotuleta kama walikuwa bado wakitusubiri pale nje.

Tuliendelea kupiga kelele kwa muda mrefu tukiamini kama tutasikilizwa, lakini mambo yalikuwa tofauti. Ukimya wa majibu ukatawala. Baadaye tulichoka na kupandwa na jazba. Tukajikuta tunaanza kutukana matusi ya kila rangi. Lakini nayo haikusaidia.

“Ndugu zangu, yametukuta. Niliwaambia Cecy ni mnyama lakini mlikuwa mnanibishia. Sasa leo tumeingia kwenye kumi na nane zake. Nadhani leo ndiyo mtayathibitisha maneno yangu. Mjiandae kwa hilo!” niliwaambia wenzangu.

“Lakini Wily, tulikwishakwambia kwamba tumshughulikie Jitu kabla hajatuwahi, lakini wewe ukawa mbishi. Ona sasa leo yanayotukuta. Hii ni njama ya Jitu hii!” Salim aliongea.

“Poleni sana ndugu zangu. Haya yatapita!” niliwatia moyo.

Takribani saa moja baadaye mlango ulifunguliwa na kisha taa ikawashwa. Kumbe taa ya chumba kile ilikuwa ikiwashiwa kwa nje. Tuliyafinya macho yetu kwani yaliumizwa na mwanga ule. Hii ni kwa sababu tulikuwa tumekaa gizani kwa muda mrefu.

Baada ya sekunde kadhaa macho yakazoea nuru na mbele yetu tukaweza kumwona Meja jenerali Cecy akiwa na maafisa wengine wa kiume wanne. Nilihisi sasa walikuwa wamekuja kikazi. Hofu ikaniingia.

ENDELEA
 
Simulizi: GENERAL’S DAUGHTER 12
Mtunzi: Kalmas Konzo
Simu: 0625 646265


Mlango ylifungwa kwa ndani na maafisa wale wakasogea mbele kutukabili. Wote mikononi walikuwa wameshika marungu ambayo yalikuwa yametengenezwa maalum. Meja jenerali Cecy alitukagua kila mmoja na kututathmini.

“Hebu mfungueni huyu hapa!” Meja jenerali Cecy aliongea huku akimwonyeshea Aboubakar rungu lake.

“Tafadhali mheshimiwa, hao hawahusiki na lolote. Naomba uwaachie tafadhali na ubaki na mimi!” niliongea huku machozi yakinilengalenga kwani nilikuwa najua kile ambacho kilikuwa kinakwenda kumpata Aboubakar punde.

“Hawa nao wana makosa. Kosa lao kubwa ni kukutambua wewe kama gaidi na kuendelea kukuhifadhi chumbani na kambini kwa ujumla!” Meja jenerali Cecy aliongea.

“Tafadhali mheshimiwa, hili jambo sivyo kama ambavyo unadhani. Jambo hili limepangwa kwa sababu zake binafsi. It is a trick!” niliongea huku nikipiga kelele kwa nguvu kujaribu kama Meja jenerali Cecy anaweza kuwasamehe wale wenzangu.

Meja jenerali Cecy alifunga masikio yake. Aliamuru Aboubakar apelekwe kwake. Kitendo kile kiliniuma sana kwani nilijua wenzangu hawa wataumizwa vibaya sana.

Ghafla Meja jenerali Cecy na maafisa wenzake wakaanza kumtembezea kipigo kikali sana Aboubakar. Kilikuwa ni kipigo cha hali ya juu mithili ya kipigo cha mbwa koko. Na kipindi chote wakishusha kipigo hicho hawakuwa wakizungumza chochote.

Dakika saba zilitosha kumfanya Aboubakar awe amechakaa kabisa. Kwa sasa alikuwa akilia huku akikoroma mithili ya kondoo. Hakika kipigo kilikuwa kimeingia mahali pake.

“Haya sema, ninyi ni akina nani? Ni kwa nini mliiba silaha ile?” Meja jenerali Cecy aliuliza maswali mfululizo.

“Tafadhali kamanda, mimi sjui chochote. Hatujui silaha ile imeingiaje chumbani mwetu!” Aboubakar aliongea kwa maumivu na machungu sana.

“Hebu muwekeni kwanza kando, tutarudi naye baadaye. Fungua hao wengine!” Meja jenerali Cecy aliamuru.

Salim na Anthony walifunguliwa ping una kisha wakasogezwa mbele ya Meja jenerali Cecy. Aliwatazama usoni kila mmoja kwa zamu.

“Nadhani mmekiona kile ambacho kimempata mwenzenu. Sasa nisingependa kupoteza muda. Ninyi ni akina nani na mko hapa kambini kwa lengo gani!” Meja jenerali Cecy aliuliza.

“Majibu yetu ni kama ya Aboubakar!” Anthony alijibu.

“Ndiyo kamanda, sisi hatujui lolote kuhusu hili!” Salim naye alikazia.

“Ohooo! Safi sana. Inaonekana mmeiva kwa mafunzo ya kigaidi. Mmekula yamini ya kutosema ukweli katika hali yoyote au siyo. Sasa niwaambie kwamba mmekosea njia. Mtautapika ukweli wote!” Meja jenerali Cecy alifoka.

Baada yah apo kilichofuata kilikuwa ni kama kile ambacho kilimpata Aboubakar hapo awali. Jamaa walichapika hasa. Miili yao ilijaa majeraha kila kona. Damu zilikuwa zikiwavuja mithili ya bomba. Niliwaonea huruma sana. Nilipatwa na uchungu sana moyoni kuona wenzangu wakipata adhabu kwa kosa ambalo hawajalifanya.

Hasira zangu juu ya Meja jenerali Cecy ndiyo zikazidi kuongezeka.

Sasa nikaona kwamba huenda mwanamke huyu alikuwa na kisasi nami. Lakini nikajiuliza zaidi kwamba iweje awe na kisasi nami wakati hakuna lolote baya ambalo nimemtendea?
Zaidi pia mimi na yeye hatukuwa tukifahamiana kabla, tumekutana tu pale kambini. Hakuna anayeijua historia ya mwenzake. Sasa iweje awe vile kwangu. Nilimlaani sana mwanamke huyu.

Baada ya kuhakikisha kwamba wenzangu wamekuwa nyang’anyang’a waliamua kuachana nao. Hii ilikuwa ni kwa sababu hakuna lolote la maana ambalo walikuwa wamelipata kutoka kwao. Waliona kama wakiendelea kuwapiga basi wangeweza kuwaua na hilo lingekuwa ni tatizo kubwa sana kwao.

Baada ya kuachana nami, sasa walikuja kwangu mimi ambaye nilikuwa ndiye mlengwa wao mkuu. Waliamini kwamba ni lazima wataupata tu ukweli ambao walikuwa wakiuhitaji intake nisitake.

Ajabu ni kwamba waliniponifikia haakunifungua pingu kama ambavyo waliwafanyia wenzangu hapo awali. Badala yake walininyanyua na kunipeleka katika kiti maalum ambacho nilikuwa nikikifahamu vema kazi yake.

Kiti hiki maalum kilikuwa ni kiti cha umeme. Kiti hiki kilikuwa kikitumika kuwatesea watu kwa kuwapiga shoti. Si kila mmoja alikuwa akiteswa katika kiti hiki. Aliyekuwa akiteswa katika kiti hiki ni yule mhalifu ambayo alikuwa amegoma kutoa siri mara baada ya kupitia mateso mbalimbali ya kijeshi.

Nilifungwa kwa mikanda maalum ambayo ilikuwa katika kiti kile. Baada yah apo afisa mmoja alienda katika swichi ambayo ilikuwa ukutani. Aliishika na kusubiri maelekezo kutoka kwa Meja jenerali Cecy.

Nilitetemeka sana. Mateso ya shoti ya umeme yalikuwa hayavumiliki. Niliwaza sana hatma yangu kutoka kwa maafisa hawa wa kijeshi ambao walikuwa na roho za kinyama sana.
“Tafadhali kamanda, jambo hili limekuwa framed. Naomba unisikilize na kunielewa pamoja na kuniamini kwa hili. Tafadhali usinifanyie hivyo!” niliomboleza nikisisitiza.
Meja jenerali Cecy hakunisikiliza badala yake alitoa ishara kwa kichwa kwa afisa yule aliyekuwa ameishika swichi kwamba aiwashe. Afisa yule pasi kusita akaiwasha swichi ile katika pointi namba moja.

Maumivu ambayo niliyapata hayakuwa yakimithilika. Shoti ya umeme si mchezo. Nilijikuta nikipiga kelele huku nikikukuruka kutaka kujiokoa kutoka katika kiti kile.

Afisa yule alizima swichi ile mara baada ya kuelekezwa kwa kichwa na Meja jenerali Cecy.

“Haya niambie, wewe ni nani na lengo lako ni nini hapa kambini?” Meja jenerali Cecy aliuliza.

“Heee! …. Heee! ……eeee! … mimi …. Si … siju …..iiiiiii chochote!” nilijibu kwa shida sana.

“Weka namba mbili!” Meja jenerali Cecy alifoka.
Afisa yule kwenye swichi aliwasha swichi ile katika pointi namba mbili. Hatua hii ilileta umeme mwingi zaidi ya ule uliokuwa ukiletwa katika pointi namba moja. Safari hii nilijikuta nikijikojolea pasi mimi mwenyewe kujua. Niliteseka sana mpaka rangi ya Ngozi yangu ikaanza kubadilika na kuwa nyeusi kutokana na shoti ile.

“You are the animal!” nilifoka huku nikimtazama Meja jenerali Cecy kwa jicho kali mara baada ya swichi ile kuzimwa.

Meja jenerali Cecy Cecy alinisogelea mara baada ya kuyasikia maneno yale kutoka katika kinywa changu. Alikishika kidevu changu na kunifanya tutazamane.

“Umesemaje?” Meja jenerali Cecy aliuliza.

“Shetani mkubwa wewe!” nilifoka.

Uso mzuri wa mrembo yule ulijikuta umechafuliwa kwa mate mengi ambayo nilimtemea. Kwa sasa nilikuwa nimekwishakata tamaa, hata hamu ya kuendelea na kambi ile sikuwa nayo. Nikaona lolote liwalo na liwe lakini kwanza lazima nifanye kitu katika kuwaokoa wale jamaa zangu ambao walikuwa hawajiwezi pale chini.

ENDELEA
 
Simulizi: GENERAL’S DAUGHTER 13
Mtunzi: Kalmas Konzo
Simu: 0625 646265

Sasa jamaa zangu wale ndiyo walikuwa wameyaamini na kuyathibitisha maneno ambayo nilikuwa nikiwaambia hapo awali kwamba Meja jenerali Cecy ni mnyama. Leo hii walikuwa wameingia katika kumi na nane zake na kuuona moto wake.

“Shiiiit!” Meja jenerali Cecy aliongea huku akusonya.

“Hebu mtoeni hapo!” Meja jenerali Cecy aliamuru.

Nilitolewa kutoka pale kitini na kupelekwa eneo lingine ambalo lilikuwa na uwazi. Meja jenerali Cecy alikuwa amejawa ghadhabu sana kutokana na kutemewa mate usoni.

Nilikuwa nimefanya vile kwa lengo maalum. Nilikuwa nataka kumfanya aghadhibike ili ajae katika kumi na nane zangu.

Meja jenerali Cecy akaamuru kwamba nipigwe mpaka nichakae. Hakuwa na utani kabisa kwa sasa.

“Pigaaa, vunja kila kiungoooo!” Meja jenerali Cecy alifoka.

Basi bwana, maafisa wale wakawa ni mithili yam bwa mwitu ambao walikuwa wamekabidhiwa mzoga. Walianza kunishushia marungu kila pahala katika mwili wangu. Meja jenerali Cecy yeye alikuwa ni zaidi. Alinishambulia na kunicharaza kwa rungu akiwa na jazba.

Katika shambulio lile nilikuwa nikikinga kichwa pamoja na uso wangu kwa kukiingiza chini ya kiti ambacho kilikuwa pembeni yangu. Niliona ile ilikuwa ndiyo sehemu nyeti katika mwili wangu. Niliamini kama endapo ikishambuliwa basi yaweza kuniletea madhara makubwa san ahata kupelekea kupoteza maisha.

“Stooop! Please stoooop!” niliongea kwa hasira kali.

“Haya, una lipi la kuongea?” Meja jenerali Cecy aliniuliza mara baada ya kuwaamuru maafisa wale kusitisha kipigo kile.

“Hivi, ni nini ambacho unakitaka kutoka kwangu wewe mwanamke? Toka nimefika katika kambi hii umekuwa ukinitendea ukatili. Kama hunitaki mimi kuwepo hap ani bora ungesema!” niliongea kwa machungu.

“Ninachohitaji ni ukweli kwamba wewe ni nani na upo hapa kwa lengo gani?” Meja jenerali Cecy alifoka.

“Sasa inafika kipindi inabidi nianze kuwa na mashaka na utimamu wa ubongo wako. Mimi nakueleza ukweli kwamba jambo lile liko framed lakini wewe huamini na unakazania kupiga watu wasio na hatia na kuwajeruhi. Hivi ukituua hapa, maisha yako yatakuwaje katika dunia hii?” niliamua kutema cheche.

Maneno yale yalimuingia Meja jenerali Cecy. Alinitazama pasi kunimaliza.

“Kwa hiyo wanitisha au siyo!” Meja jenerali Cecy alifoka.

“Siyo nakutisha. Siku ya kwanza ulinitesa mpaka nikazimia. Leo hii umenipiga mpaka kuvuja damu. Sasa kama nikisema wewe una ajenda ya siri na mimi nitakuwa nimekosea? Kutokana na matendo yako ndo maana nakufanisha na mnyama!” nami nilifoka.

“Kamanda, haiwezekani mbwa huyu akakuvunjia heshima kwa kukutusi namna hii!” afisa mmoja aliongea huku wenzake wakinitazama kwa jazba.

“This dude is a jerk. Let us beat him to death!” Meja jenerali Cecy alifoka huku akinisogelea tayari kwa kunishambulia.

Sasa hilo ndilo kosa ambalo alilifanya Meja jenerali Cecy nami nilikuwa nikiusubiri sana wasaa ule.

Nikiwa pale chini mikono ikiwa imefungwa pingu kwa nyuma, nilimfyatua teke Meja jenerali Cecy na kumchota. Ndani ya sekunde akajikuta amenilalia juu huku nyuso zetu zikitazamana. Nami pasi kupoteza muda niliitumia fursa ile kuuchomoa ufunguo wa pingu uliokuwa kiunoni na kujifungua mikono yangu.

Baada yah apo maafisa wale walishangaa kumwona bosi wao akipaa juu baada ya mimi kumsukuma kwa nguvu huku mimi nikiwa nimesimama.

Kabla Meja jenerali Cecy hajafanya uamuzi wowote nilimkandika Makonde mawili ya shavuni pamoja na kumbadika teke la tumbo. Maafisa wengine walichomoa bastola zao na kutaka kunishambulia. Lakini walikuwa wamechelewa. Kwa kasi ya umeme nilimvamia Meja jenerali Cecy na kuichomoa bastola yake na kumwekea kichwani. Nilikuwa nimemteka.

Kitendo kile kiwashangza san ahata wenzangu ambao walikuwa wamelala pale chini wakiwa hoi kwa maumivu. Siku zote hawakuwa wamewahi kufikiri kwamba nilikuwa na uwezo mkubwa kiasi kile katika mapigano. Wenyewe walikuwa wakinidhania kwamba nilikuwa ni mdebwedo na nilikuwa nikimwogopa sana Jitu.
Walikuwa wamekosea. Mimi nilikuwa na uwezo mkubwa sana katika mapambano na mbinu mbalimbali za kijeshi. Hii ndiyo sababu hata ilipokuja nafasi ya uteuzi wa askari wa kuja kujiunga katika kambi hii, mkuu wa kituo changu cha kazi hakusita kuniteua mimi.

Kwa upande wake Meja jenerali Cecy hakuwa akiamini kile ambacho kilikuwa kimenitokea. Uwezo ambao nilikuwa nimeuonyesha mbele yake ulikuwa umemtisha sana. Hakujua aniweke katika kundi gani, la binadamu au mzimu.
********
Mhusika mkuu wa tukio lile la upotevu wa silaha ya Jenerali Knowman alikuwa ni Jitu kama ambavyo mimi nilikuwa na uhakika. Kuna funguo za akiba za vyumba vyetu vya kulala ambazo zinatunwa katika ofisi moja ambayo ilikuwa ni kama stoo. Ofisi hii ilikuwa ikisimamiwa na kuangaliwa na askari mmoja ambaye alikuwa ni mmoja wa wapambe wa Jitu.

Akamwamuru kijana yule ampe ufunguo wa chumba chetu. Baada yah apo akaenda katika ofisi ya Jenerali Knowman. Akasubiri kwa kujificha mpaka pale Jenerali Knowman alipotoka ofisini kwake.

Kwa uangalifu mkubwa Jitu aliingia mle ofisini na kuanza kufanya upekuzi. Katika pekua pekua yake hatimaye akakutana na bastola ya Jenerali katika droo. Aliichukua na kisha kwa uangalifu mkubwa uleule akatokomea.

Akaenda katika chumba chetu na kuiweka bastola chini ya kitanda changu. Hakuwa akijua kama kile kilikuwa ni kitanda changu lakini bahati nzuri ilikuwa upande wake. Alikuwa sawa sawa na dhamira yake. Akaufunga mlango na kutokomea.

Wakati huo sisi tulikuwa kule bustanini tukipiga stori mbili tatu.
********
Meja jenerali Cecy alikasirika sana. Aliona kama nilikuwa nimemtia aibu kubwa sana mbele ya maafisa ambao walikuwa chini kicheo. Niliihisi Dhahiri ghadhabu yake kupitia mhemo wake.

Nilikuwa nikifahamu kwamba kitendo kile nilichokifanya kilikuwa ni kosa kubwa sana kijeshi. Nilikuwa nafahamu kwamba baada yah apo nitachukuliwa adhabu kubwa sana ikiwa ni pamoja na kifungo cha muda mrefu gerezani. Lakini mimi sikujali hili. Nilitaka kumwonyesha kwamba alikuwa akikosea. Nilijitoa mhanga kuwanusuru wenzangu.

“Meja jenerali Cecy, nilikwishakwambia toka awali kwamba mimi si mhusika wa jambo hili lakini fikra zako zimekumbwa na ukungu, hutaki kuamini kabisa. Ni kweli bastola imekutwa katika kitanda changu lakini nimeshasema kwamba jambo hili limepangwa. Unachotakiwa kufanya ni kuchunguza nani mhusika kwa mbinu nyingine na si hizi mbinu za mateso!” niliongea.

“Nina uwezo wa kufanya lolote lakini mimi si mtu wa hasira hivyo siwezi kufanya chochote. Ninachokushauri, fanya uchunguzi. Adui mnaishi naye!” nilimalizia.

Baada yah apo nilimkabidhi bastola ile Meja jenerali Cecy. Hakuamini kama nilikuwa nimefanya vile. Alishangaa.

Aliipokea bastola ile na ghafla akaielekeza kichwani kwangu. Sasa ndiyo niliweza kuiona ghadhabu aliyokuwa nayo kwa sababu nilikuwa nikitazamana naye.

“Usifanye hivyo, utajilaumu katika maisha yako yote. Please calm down!” niliongea mara baada ya kukiona kidole chake kikitaka kusukuma trigger.

Haikuwa kama ambavyo nilimsisitiza. Meja jenerali Cecy alifyatua trigger na risasi ikazama kifuani mwangu. Nilianguka chini na habari ikawa imeishia hapo. Sikuelewa lichoendelea.

ENDELEA
 
Simulizi: GENERAL’S DAUGHTER 14
Mtunzi: Kalmas Konzo
Simu: 0625 646265


Mtikisiko wa kidle changu ulimfanya nesi akaribie katika kitanda ambacho nilikuwa nimelazwa na kuniwekea uangalizi wa karibu. Ile ilikuwa ni ishara kwamba nilikuwa ninapata fahamu. Uso wa muuguzi yule ulitamalakiwa na tabasamu la faraja.

Niliyafumbua macho yangu taratibu. Nuru iliyokuwa imetapakaa chumbani mle iliyaumiza macho yangu na kunifanya niyafunge tena. Dakika moja baadaye nikayafumbua tena. Safari hii ikawa afadhali kidogo kwa yalijitahidi kuizoea nuru ile ingawa bado yalikuwa yakiuma.

Sikuwa nafahamu pale palikuwa ni wapi na ni nini ambacho kilikuwa kimenitokea. Nilifikiri haraka haraka na baadaye nikaona nisiendelee kuumiza kichwa kwa maswali ambayo hayakuwa na majibu ya wazi.

Niliuinua mkono wangu kwa lengo la kujaribu kuinuka pale kitandani kwa kuishikiza katika nguzo za kitanda. Maumivu ambayo niliyapata kifuani yalinifanya nipige kelele. Yalikuwa ni maumivu ambayo hayamithiliki.

Zaidi ya maumivu yale, kuna jambo lingine ambalo lilinistaajabisha zaidi. Mkono wangu ule ulikuwa umefungwa pingu ambayo ilikuwa imefungiwa kwenye mfumbati wa kitanda.

Nilirejea kujilaza pale kitandani huku bado nikiwa naugulia maumivu makali kifuani. Mpaka wakati huo bado sikuwa natambua ni nini ambacho kilikuwa kikiendelea.

“Tulia upumzike, ukijitikisa utazidi kujiumiza. Unahitaji mapumziko ya muda mrefu!” muuguzi yule aliongea.

“Kwani hap ani wapi n ani nini ambacho kimenipata?” nilimwuliza muuguzi yule kwa shauku.

Nilitambua kwamba yule ni muuguzi kutokana na mavazi yake. Na pia hisia zangu kwa asilimia fulani zilikuwa zikiniongoza kuhisi kwamba eneo lile huenda ilikuwa ni hospitali.
“Hapa ni hospitali!” muuguzi yule alijibu.

Wakati huo huo daktarin akawa ameingia ndani ya chumba kile.

“Vipi amezinduka?” daktari aliuliza.

“Ndiyo dokta!” muuguzi yule alijibu.

“Kwa nini niko hapa hospitali? Ni nini ambacho kimenipata?” niliuliza maswali mfululizo.

“Kuna shida kidogo ambayo uliipata. Ulipata jeraha kifuani lililopelekea kufanyiwa upasuaji. Kwa sasa unapaswa kutulia!” daktari alijibu.

“Jeraha!”

Kauli hii ilitembea katika fikra zangu na kunifanya nianze kuvuta kumbukumbu. Nikakumbuka namna ambavyo Meja jenerali Cecy na wenzake walivyotuchukua na kutupeleka katika chumba cha mateso. Nikakumbuka namna ambavyo walitutesa. Pia nikakumbuka namna ambavyo Meja jenerali Cecy alivyonipiga ba risasi. Nilichoka kabisa.

“Wenzangu wako wapi?” niliuliza.

“Wenzako wako salama. Wako wodini nao wanaendelea na matibabu. Hali zao zinaendelea vizuri!” daktari alinijibu.

“Niko hapa hospitali kwa muda gani?” niliuliza tena.

“Upo hapa hospitali siku ya pili sasa!” daktari alijibu.

Sasa ndiyo nikajua kwamba nilikuwa nimepoteza fahamu kwa muda wa siku mbili. Na pia kuhusu pingu niliyokuwa nimefungwa nayo mkononi nilikuwa nafahamu kwamba kuna msala mkubwa sana nilikuwa nakwenda kukumbana nao.

Kumshambulia Meja jenerali lilikuwa ni kosa kubwa sana kijeshi. Na kwa zile ghadhabu ambazo alikuwa amezionyesha siku ile nilipomshambulia, nilifahamu kwamba ilikuwa ngumu sana kwangu kutoboa katika kisanga kile. Jambo la msingi nilikuwa namwomba Mungu wenzangu waachiwe na wasihusishwe kabisa katika kesi hii.
******
Siku tatu baadaye wenzangu waliruhusiwa kutoka pale hospitali kwani hali zao zilikuwa na afadhali. Lakini jambo ambalo lilinishangaza ni kwamba wenzangu walikuja kuchukuliwa na wanajeshi wakiwa wamefungwa pingu. Hapo nikajua kwamba msala ule bado ni wa moto. Na nilishuhudia hili kwa sababu kwa sasa nilikuwa nimeletwa katika wodi ambayo wenzangu walikuwa wamelazwa.

“Sasa kwa nini mnawafunga pingu jamani?” niliuliza kwa ghadhabu.

“Huna ruhusa ya kutuhoji!” mwanajeshi mmoja ambaye alikuwa ndiye inchaji wa zoezi lile alijibu kwa kiburi.

"Jamani toka awali nilikwishawaambia kwamba mnakosea sana. Waacheni hao kwani hawahusiki kwa lolote!” niliongea kwa uchungu.

“Tulia wewe! Hawa wanakwenda selo. Tunasubiri tu wewe uruhusiwe kutoka hapa hospitali ndipo jambo hili lifike tamati!” mwanajeshi yule alijibu.

“Naona mnazidi kuyafanya mambo kuwa magumu!” niliongea.

“Yaani nakushauri umwombe sana Mungu. Yaani wewe unajaribu kumwua Meja jenerali! Kijana lazima ushughulikiwe ipasavyo!” mwanajeshi yule aliongea.

“Kumwua Meja jenerali!” niliuliza kwa mshangao.

“Sasa nini ambacho hukifahamu? Acha kujitoa ufahamu!” mwanajeshi yule alijibu.

Yaani nilichoka kabisa. Nikajua tayari Cecy alikuwa amekwishafanya yake. Alikuwa amelisuka jambo lile kitaalam kabisa ambapo kwangu kuponyoka ilikuwa ni ngumu sana, lakini pia kwa upande wake alikuwa amesafishika na kuonekana hana hatia kabisa. Hakika Cecy alikuwa ni hatari sana.

Baada yah apo mwanajeshi yule aliwaamuru wenzake kuondoka na wale wenzangu wakiwa na pingu mikononi. Kitendo kile kiliniuma sana. Nikazidi kumchukia zaidi Cecy. Nikaona ugomvi wake nami ulikuwa umeanza kuleta athari mpaka kwa watu ambao hawahusiki kabisa.

Kwa upande mwingine nikamuonea huruma sana mwanamke yule. Nilichokuwa nawaza kumfanya nadhani kwa wakati ule anekuwa anamwomba Mungu nisipone.

Kwa sasa nilikuwa nimekwishakata tamaa kabisa ya kuendelea na mafunzo katika kambi ile. Meja jenerali Cecy alikuwa ameniharibia mustakabali wangu pale kambini. Alikuwa ameyavuruga kabisa maisha yang una kuyaharibu. Sasa kwa sababu alikuwa amefanya vile, basi nami sikuwa na budi ya kumharibia nay eye. Nilitaka nimfanye asinisahau katika maisha yake.

Jitu yeye ndiye alikuwa chanzo cha masahibu haya yote. Akili zake za kijinga na kitoto zimesababisha maafa makubwa pale kambini. Sasa huyu naye alikuwa katika orodha yangu ya watu ambao nilikuwa ninapaswa kushughulika nao.

Huyu Jitu alikuwa akiyafanya mambo yake yale ya kijinga kwa sababu hakuwa akinifahamu vema. Sasa huyu niliapa kumfanya awe akiijutia siku ambayo alikutana na mimi kwa mara ya kwanza. Yaani atajuta kunifahamu.

Kwa sababu alikuwa ameyaharibu maisha yangu na wenzangu wasio na hatia, basi nami nilipanga kuyaharibu maisha yake mpaka familia yake. Yaani naye kwa kipindi kile alikuwa anatakiwa amwombe Mungu amwepushie kimbunga ambacho kilikuwa kinakuja mbele yake.

Kwa sasa nilikuwa nimetibuka katika moyo na fikra zangu. Mustakabali wa maisha ya rafiki zangu ambao ulikuwa umeharibiwa ulikuwa ukiniuma sana. Machozi ya uchungu yalinitoka.

“Nitawafanya wajute mashetani hawa. Yaani wamegusa mahali pengine kabisa ambako hawakustahili. Siku zao zinahesabika!” niliongea kwa sauti ya chini huku machozi ya uchungu yakizidi kunibubujika.

Baadaye daktari alikuja na kunichoma sindano ya usingizi kwa sababu nilikuwa naleta vurugu sana nikidai wenzangu waachiliwe. Daktari aliona ile ilikuwa ni mbaya sana kwa afya yangu. Hivyo aliona ni bora anitulize kwa kunipiga nusu kaputi.

ENDELEA
 
Simulizi: GENERAL’S DAUGHTER 15
Mtunzi: Kalmas Konzo
Simu: 0625 646265

Lakini hebu turudi nyuma kidogo. Ilikuwaje mpaka mimi na wenzangu tukaweza kusalimika katika kizaazaa kile kwa sababu Meja jenerali Cecy na wenzake walipotuacha katikajengo lile, tulikuwa tukiogolea katika dimbwi la mauti. Basi mambo yalikuwa kama ifuatavyo;

Risasi ile niliyopigwa ilizama kabisa katika kifua changu lakini kwa bahati nzuri haikuwa katika upande wa kushoto mahali ambako moyo upo. Meja jenerali Cecy alikuwa amenipiga risasi katika upande wa kulia wa kifua changu.
Risasi ile ilipekea mimi kupoteza fahamu. Wenzangu nao kwa kipindi kile walikuwa wamepoteza fahamu hivyo hakuna ambaye alijua kilichoendelea.

Askari jeshi wale waliwakamata wenzangu na kuwafunga mikono yao nyuma mgongoni ambako yaliwekwa matairi ya gari. Yaani wakawa kama wameyabeba. Mimi sikufanyiwa vile kwa sababu waliona kuwa hawakuwa na haja ya kujishughulisha nami ambaye nilikuwa tayari nimekufa.

Hii ilikuwa ni katika kuhakikisha kwamba wale wenzangu hata wakizinduka wasiweze kujisaidia.

Kutokana na ujasusi nilioufanya ni kwamba Meja jenerali Cecy alipotoka katika jengo lile aliwaambia walinzi wanaolinda wafunge mlango ule na waendelee kulinda. Aliwaambia kwamba wasifungue kwa vyovyote vile.

Basi tukawa tumeachwa pale tukiwa tumechungulia kaburi. Msaada ulikuwa mbali sana kwetu.

Wenzangu walipokuja kuzinduka baadaye walijikuta katika hali mbaya sana ya kudhibitiwa na matairi yale. Walipiga kelele kuomba msaada lakini ilikuwa ni kazi bure. Walilia sana na kukata tamaa kwani walijua kwamba walikuwa wamenipoteza. Walijua kwamba nilikuwa nimepigwa risasi na nimekufa.

Siku ya kwanza ikapita. Hali ikazidi kuwa mbaya sana kwa wenzangu. Afya yao ilizidi kudorora kutokana na majeraha ambayo walikuwa nayo. Mimi kwa upande wangu sikuwa nikitambua chochote kwani bado nilikuwa nimepoteza fahamu.

Afisa mmoja alimfuata Meja jenerali Cecy na kumpa ushauri wa busara sana.

“Kamanda, nimekaa nimefikiri nikaona kuna tatizo ambalo linatukabili mbele yetu endapo hatutachukua hatua Madhubuti!” afisa yule aliongea.

“Tatizo gani?” Meja jenerali Cecy aliuliza.

“Ni kuhusiana na ile mizigo tuliyoiacha kule karakana. Mmoja tayari amekufa, na hilo ni tatizo kubwa sana ambalo tunatakiwa tujipange katika kutoa ripoti. Lakini hebu tuepushe vifo vya wale wengine ili kupunguza matatizo!”

“Kifo cha yule mmoja ni rahisi kukitolea maelezo. Ni kwamba alikuvamia na kutaka kukuua. Kilichofuata basi ilikuwa ni katika kukuokoa!” afisa yule alihitimisha.

Maneno yale yalimwingia Meja jenerali Cecy. Basi akafanya mpango wa kuja kutuchukua na kutupeleka hospitali.

Hapa hospitali ikaja kugundulika kwamba kumbe hata mimi sikuwa nimepoteza maisha. Hivi harakati za kunusuru maisha yangu zilianza.

Habari ile haikuwa njema kabisa kwa Meja jenerali Cecy. Yeye alitaka niwe nimekufa kabisa ili kupoteza Ushahidi wa namna alivyonipiga risasi. Aliamini kwamba utetezi nitakaoutoa utamweka matatani.

Akabaki akiwa amechanganyikiwa. Na hivi ndivyo ilivyokuwa.
********
Niliendelea kulazwa pale hospitali kwa muda mrefu sana. Hatimaye mwezi mmoja ukawa umekatika. Hali yangu kwa sasa ikawa imetengemaa kabisa. Nikawa nimepona jeraha langu na sikuwa na maumivu tena.

Wazo la kwanza katika kuelekea kulipiza kisasi nikaamua nitoroke pale hospitali kisha nikamteke Jitu pamoja na Meja jenerali Cecy na kutoweka nao pale kambini. Huko nitakakowapeleka ndiyo nitakwenda kuwashikisha adabu.

Wazo lile nililiona ni la msingi sana kwani niliamini kwamba angalau kidogo lingeweza kupunguza machungu ambayo ninayo. Lakini pia ningekuwa nimekwishafanikiwa kuyaharibu pia maisha ya hawa adui zangu kwani ambacho nilipanga kuwafanyia ni lazima kingegeuza mustakabali mzima wa maisha yao.

Lakini kadri nilivyokuwa nikiendelea kuwaza nikaja kuona kwamba kwa upande mwingine wazo lile halikuwa jema kabisa. Ni kweli ningefanikiwa kuwateka wale adui zangu na kuondoka nao, lakini je nini hatma ya wale rafiki zangu ambao bado walikuwa wakiteseka selo kwa takribani mwezi sasa?

Nikaona hapana, nilitakiwa nitumie mbinu na hekima katika kulitatua tatizo lile. Rafiki zanmgu walitakiwa wawe huru. Ilikuwa imetosha sasa kwa unyama ule wa Cecy.

Wakati wa kumvua nguo Cecy ulikuwa umefika. Nikiwa pale hospitali nilituma ujumbe kwa Meja jenerali Cecy nikiomba kukutana naye. Ujumbe wangu ulisema kwamba ilikuwa ni muhimu sana.

Ujumbe ulipomfikia Meja jenerali Cecy kwanza kabisa alishtuka. Hakutaraji kama mimi ningeweza kuomba kukutana naye. Kwa namna nyingine akahisi huenda ule ulikuwa ni mtego kwani kwa sasa alikuwa akinifahamu namna ambavyo nilikuwa hatari.

Hakuwa na jinsi, akaamua kukutana nami.
Ugeni mzito wa maafisa wa jeshi uliwasili pale hospitali ya kijeshi. Meja jenerali Cecy alikuwa ndiyo kiongozi wa wanajeshi wale. Askari aliokuwa nao walikuwa ni askari wenye uwezo mkubwa sana kijeshi. Alikuwa amekwishawapanga kwamba mtu ambaye alikuwa anaenda kuonana naye alikuwa ni hatari sana hivyo walipaswa kuwa makini.

Kwa wanajeshi wale aliokuja nao pamoja na wale ambao walikuwa wakinilinda pale hospitali Meja jenerali Cecy alijiona yu salama kabisa. Hakudhani kama ningeweza kutenda lolote la hatari na nikabaki salama pasi kudhibitiwa.

“Haya unasemaje?” Meja jenerali Cecy aliuliza mara baada ya kuingia katika wodi ambayo nilikuwemo akiwa na walinzi wake.

“Nina mazungumzo nyeti, naomba walinzi wako wasubiri hapo nje!” niliongea.

“Nitakuaminije?” Meja jenerali Cecy aliuliza.

“Na hilo ndilo tatizo lako. Wewe ni mgumu sana wa kumwamini mt una ndiyo maana huwa unashindwa kufanikiwa katika baadhi ya mambo!” niliongea.

“Hebu nisubirini hapo nje mlangoni!” Meja jenerali Cecy aliamuru na walinzi wake wakatoka nje.

“Mimi na wewe ni maadui wakubwa sana mpaka sasa. Najua ulikuwa ukiwaza kuniangamiza hapa hospitali ukihofia kwamba nitaeleza namna ulivyonipiga risasi. Hilo achana nalo kwani katu sitafanya hivyo” nilianza kuongea.

“Kinachoniuma mimi ni namna ambavyo maisha yangu yameharibika wakati mtu ambaye amesababisha yote haya yuko huru akishangilia. Rafiki zangu wanateseka selo mpaka sasa kwa kosa ambalo hawajalifanya. Wewe ambaye ni mwenye dhamana tunakueleza ukweli lakini wala hata hauzingatii, badala yake unafanya mambo pasi kutumia akili na kusababisha madhara makubwa” niliamua kumpa vidonge vyake.

“Ukitoka hapa nenda kamshukuru sana Mungu kwamba sikufa siku ile kwani damu yangu ingekutesa sana katika maisha yako. Ungekuwa umemwua mtu asiye na hatia kwa uzembe!” niliendelea kuongea.

“Kwa hiyo hilo ndilo uliloniitia?” Meja jenerali jina Cecy aliuliza.

“Hapana, hiyo ilikuwa ni utangulizi tu!” nilimjibu.

ENDELEA
 
Back
Top