Advertise here

Kwa nini Mungu aliwapeleka wana wa Israeli katika nchi ya Kanaani ambayo ililaaniwa?

Kwa nini Mungu aliwapeleka wana wa Israeli katika nchi ya Kanaani ambayo ililaaniwa?

Hebu turejee maandiko katika kitabu cha Mwanzo 9:
20 “Nuhu akaanza kuwa mkulima, akapanda mizabibu;
21 akanywa divai, akalewa; akawa uchi katika hema yake.
22 Hamu, baba wa Kanaani, akauona uchi wa baba yake, Nuhu, akawaeleza ndugu zake wawili waliokuwa nje.
23 Shemu na Yafethi wakatwaa vazi, wakalitanda mabegani mwao wote wawili, wakaenda kinyumenyume, wakaufunika uchi wa baba yao; Nuhu, na nyuso zao zilielekea nyuma, wala hawakuuona uchi wa baba yao.
24 Nuhu akalevuka katika ulevi wake, akajua mwana wake mdogo alivyomtendea.
25 Akasema, na alaaniwe Kaanani; Atakuwa mtumwa kabisa kwa ndugu zake”.

Kumbuka hapo mwanzo Kaanani halikuwa jina la Nchi, bali lilikuwa ni jina la Mtu. Na mtu huyo alikuwa ni mtoto wa nne (fourth child) wa Hamu:

Mwanzo 10: 6 “Na wana wa Hamu ni Kushi (Ethiopia), Misri, Putu (Libya), na Kanaani”.

Haijulikani kwa undani mtoto Kanaani alikuwa na tabia gani? Lakini inaelekea kuwa matendo yake yalikuwa kama ya baba yake, Hamu, ndiyo maana Nuhu alimbebesha moja kwa moja laana ya baba yake.

Huyu Kanaani ndiye aliyelaaniwa, na baadaye alikuja kuzaa watoto na uzao wake ukaitwa uzao wa Kanaani, kufuatia jina la baba yao. Walipotawanyika usoni pa nchi yote katika ule mtawanyiko wa Babeli (Mwanzo 11:8-9), ndipo wakaenda kuishi mahali wana wa Israeli walipowakuta.

Kipindi wanaishi, ardhi ile ilijulikana kama nchi ya Wakanaani. Na kilichokuwa kimelaaniwa na Mungu si ile ardhi au nchi, bali ni watu, ambao ndio hao Wakaanani, ikiwa na maana kuwa, hata kama wasingeishi katika ile ardhi na kwenda kuishi katika ardhi nyingine, bado wangekuwa chini ya laana.

Kwa hiyo, wana wa Israeli wakati wanatoka Misri, Mungu aliwatoa Wakanaani kwenye ile ardhi na kuwaweka wana wa Israeli, kwa sababu kilicholaaniwa katika Mwanzo 9:20-25, si ardhi bali ni watu. Hivyo, watu wanaweza kuondolewa na ardhi ikaendelea kutumika na wengine na ikawa nchi ya baraka tu. Ndiyo maana baada ya pale haikuitwa tena nchi ya Wakanaani bali nchi ya Israeli.

Swali la kufikirisha

Swali ni je! Wana wa Hamu hadi leo wamelaaniwa? Maana miongoni mwao kuna Kushi ambaye uzao wake ni watu weusi.

Jibu ni la! Kristo alikuja kuondoa laana zote pale Kalvari, na hivyo hakuna tofauti ya Myahudi na Mmisri, Mkushi, wala Muisraeli, mbele za Mungu. Kama tumeokoka, wote tunahesabiwa sawa mbele zake.

Lakini kama hatutazaliwa mara ya pili kwa maji na kwa roho, wote mbele zake ni kama tuliolaaniwa.

Zingatia kitabu cha Wakolosai 3:
10 “mkivaa utu mpya, unaofanywa upya upate ufahamu sawasawa na mfano wake yeye aliyeuumba.
11 Hapo hapana Myunani wala Myahudi, kutahiriwa wala kutokutahiriwa, mgeni wala mshenzi, mtumwa wala mwungwana, bali Kristo ni yote, na katika yote”.

Kitabu cha Waefeso 2:16 kinasema: “Akawapatanisha wote wawili na Mungu katika mwili mmoja, kwa njia ya msalaba, akiisha kuufisha ule uadui kwa huo msalaba”.

Kwa hiyo, tukumbuke kabisa kuwa nchi ya Kanaani haikulaaniwa, bali ni mtu Kanaani na uzao wake ndio walilaaniwa. Kutokana na mtawanyiko wa watu duniani wakitokea Babeli, baada ya mgongano wa lugha mbalimbali, ndipo yeye Kanaani akaenda kuishi kwenye nchi ambayo iliitwa kwa jina lake la Kanaani. Wakazaliana na kuwa wengi, wakatengeneza jamii/makabila takriban saba, au nchi saba.

Nchi walimoishi Wakaanani haikulaaniwa, ndiyo maana ikaitwa nchi yenye maziwa na asali. Kumbuka kuwa Musa alipotuma wapelelezi 12 kwenye nchi ya Kanaani (Hesabu 13:1-3) walirudi na baadhi ya vyakula. Kwa mfano: mkungu/kichala kimoja cha zabibu kilivyo kikubwa, kilihitaji wanaume wawili wakibebe kwa mti, mabegani mwao (Hesabu 13:27). Hii inadhihirisha kuwa ardhi/nchi ile haikulaaniwa, bali ni watu ndio walilaaniwa. Ardhi ilikuwa inazalisha kikamilifu bila dosari lo lote.

Kwa hiyo, Mungu hakupeleka wana wa Israeli katika nchi ya Kanaani, ambayo ililaaniwa.
La hasha. Nchi ile haikulaaniwa, bali mtu Kanaani na uzao wake waliokwenda kuishi kule, ndio walikuwa wamelaaniwa. Ardhi/nchi ilikuwa na rutuba, na uzalishaji bora wa mazao.
Kutokana na ubora/ufanisi wake, nchi ikaitwa nchi ya maziwa na asali.
 

Similar threads

Back
Top